Shule zinavyochuana kubaki katika 10 bora kidato cha sita

May 9, 2019 11:51 am · Daniel
Share
Tweet
Copy Link
  • Shule hizo ni zile zilizoingia katika orodha ya 10 bora zaidi ya mara mbili katika kipindi cha miaka saba iliyopita. 
  • Katika orodha hiyo, shule ya sekondari Kisimiri na Feza Boys hazijawahi kutoka katika orodha ya 10 bora kwa miaka saba mfululizo.   
  • Shule za Serikali na binafasi zimeendelea kuchuana kuhakikisha kila mwaka zinabaki katika kundi hilo.

Dar es Salaam. Kila mwaka matokeo ya kidato cha sita yanapotangazwa, masikio ya watu hujielekeza zaidi kusikia shule zilizoingia katika orodha ya shule 10 bora au za mwisho kitaifa. 

Kutajwa kwa makundi hayo mawili kunatoa fursa kwa wazazi kufanya tathmini ya kina kuhusu shule wanazoweza kuwapeleka watoto wao. Lakini unazifahamu shule zilizodumu kwenye orodha ya 10 bora kwa muda mrefu?

www.nukta.co.tz inakuletea shule hizo kutokana na uchambuzi iliofanya wa matokeo ya kidato cha sita yaliyotolewa na Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta) kwa miaka saba iliyopita yaani kuanzia 2012 hadi 2018. 

Miongoni mwa shule hizo ni zile ambazo hazijawahi kutoka kabisa katika orodha hiyo na zile zilizoingia zaidi ya mara moja katika orodha hiyo ya dhahabu katika mpangilio wa ubora wa ufaulu wa shule nchini. 

Katika orodha ya shule hizo zinazotawala 10 bora; tano ni za Serikali na zinazobaki ni za watu binafsi ambazo zimekuwa na mchuano mkali kubaki katika kundi hilo.   

Shule hizo ni Kisimiri iliyopo Arusha, Kibaha (Pwani), Mzumbe (Morogoro), Iliboru (Arusha) na shule ya Tabora Boys (Tabora). Shule nyingine ni 

Feza Boys (Dar es Salaam) na Marian Girls (Pwani), Feza Girls (Dar es Salaam) na Marian Boys (Pwani)  pamoja na Mazinde Juu (Tanga).


Zinazohusiana:


Katika orodha hiyo, shule za Kisimiri na Feza Boys hazijawahi kutoka katika katika 10 bora kitaifa kwa miaka saba mfululizo, licha ya kupata ushindani mkali wa shule zingine kongwe ikiwemo Kibaha ambayo imefanikiwa kuingia mara sita katika orodha hiyo katika kipindi hicho.  

Ni mwaka 2015, Kibaha ambayo ilianzishwa mwaka 1965 ilitolewa nje ya orodha hiyo ambapo ilishika nafasi ya 22 kitaifa lakini mwaka uliofuta wa 2016 ilikaza na kung’ang’ania katika kundi hilo hadi mwaka jana. 

Kutokana na mchuano mkali, shule za Mzumbe, Mazinde Juu na Marian Girls zenyewe zilifanikiwa kuingia katika 10 bora mara tano katika kipindi hicho. 

Mathalan, Mzumbe sekondari ambayo ni shule kongwe haikuingia kwenye 10 bora miaka miwili mfululizo yaani mwaka 2014 na 2015 lakini miaka mitatu iliyofuta haikuchomoka katika orodha hiyo. 

Mazinde Juu nayo iliondolewa katika orodha ya 10 bora mwaka 2014 na 2016 huku ikitamba kwa miaka iliyobaki ambapo mwaka 2013 na 2015 ilishika nafasi ya sita kitaifa.  

Marian Girls ya mkoani Pwani nayo ilikuwa ni miongoni mwa shule zilizoingia mara tano katika orodha ya 10 bora. 

Kundi la mwisho ni shule za Iliboru, Tabora Boys na Marian Boys zimefanikiwa kuingia mara tatu katika orodha hiyo muhimu Tanzania.

Shule hizo 10 zinazotawala 10 bora zitaweza tena kuendeleza ubabe wake wa kutawala orodha hiyo katika matokeo ya kidato cha sita mwaka huu ambayo mitihani yake inafanyika nchi nzima?

Mwanafunzi Francis Thomas aliyemaliza kidato cha Sita katika shule ya Wavulana ya Feza akiwa amebebwa juu na wanafunzi wenzie wa shule hiyo baada ya kuibuka Mwanafunzi bora kitaifa katika Masomo ya Sanaa na Biashara katika matokeo yaliyotangazwa na baraza la mitihani Julai 15, 2017.Picha na Michuzi.

Mafanikio ya shule hizi ni ya kubahatisha?

Mafanikio ya shule hizo kufanya vizuri katika matokeo ya kidato cha sita siyo ya kubahatisha. Zimefanikiwa kuwekeza katika miundombinu ya kufundishia na kujifunzia na kuboresha maslahi ya walimu ambao wana mchango mkubwa katika elimu ya wanafunzi.

Mwalimu Mkuu wa shule ya Kisimiri Valentine Tarimo ameimbia nukta(www.nukta.co.tz) kuwa kufanya vizuri kwa shule hiyo ya Kisimiri sio uchawi bali ni jitihada za pamoja kati ya wanafunzi na walimu.

“Ufaulu wetu unachagiwa na ushirikiano mkubwa ulipo kati ya walimu na wanafunzi kwa kufanya kazi kwa bidii bila kupoteza muda kama mheshimiwa Rais Magufuli anavyosema hapa kazi tu sisi tunatasfri kwa vitendo”amesema Tarimo.

Pia ameleza sababu nyingine ni kila mwaka kuwa na darasa linalotaka kuweka historia yake yenyewe ama kuongoza kishule au ufaulu wa madaraja hivyo kufanya kila mwananfunzi wa kila darasa kuweka jitihada zake binafsi na sambamba na hilo darasa.

Tarimo ameileza nukta kuwa katika mitihani ya kidato cha sita inayoendelea wamefanya jitihada na maandalizi ya kutosha.

“Ni kama vita kila mtu anajindaa kupambana  na sisi tumejianda vizuri kama shule nyingine zote tunatumani kufanya vizuri lakini tusuburi matokeo yatakabotolewa na necta yatakuaje……”amesema Mkuu huyo wa shule ya Kisimiri.

Enable Notifications OK No thanks