Kisimiri sekondari inavyozikimbiza shule kongwe, binafsi Tanzania

September 1, 2018 2:20 pm · Zahara
Share
Tweet
Copy Link
  • Ilijengwa kwa nguvu za wazazi na wafadhili kutoka Switzerland.
  • Shule hiyo ni tishio kwa shule kongwe za serikali na binafsi ambapo imekaa kwenye 10 bora kitaifa kwa miaka saba mfululizo.
  •  Nidhamu, motisha na kujituma kwa walimu na wanafunzi kunaibeba shule hiyo.

Dar es Salaam. Ni mwendo wa kilomita 62.5 kutoka Arusha mjini hadi katika kijiji cha Kisimiri wilaya ya Arumeru karibu na hifadhi ya Taifa ya Arusha.

Hapo ndipo inapatikana shule ya sekondari ya vipaji maalum ya Kisimiri iliyoanzishwa mwaka 2002. Ina mkondo wa kidato cha kwanza hadi cha sita.

Shule za vipaji maalum ni zile ambazo huandikisha wanafunzi waliofanya vizuri kutoka shule mbalimbali za eneo husika, mfano wa shule hizo ni shule ya sekondari Mzumbe ya Morogoro na Ilboru ya Arusha. 

Kisimiri ni shule ya Serikali iliyojengwa kwa nguvu za wananchi. Upekee na sifa yake ni kuwa kinara wa 10 bora katika matokeo ya kidato cha sita kwa zaidi ya miaka sita ikichuana na shule kongwe na binafsi zenye majina makubwa kama Feza Boys, Mzumbe, Marian Girls, Kibaha na zingine nyingi.

Mathalani mwaka 2018 katika matokeo ya kidato cha sita ambapo ilikuwa shule ya pili kitaifa chini kidogo ya Kibaha ambayo ilishika nafasi ya kwanza. 

Umaarufu wa Kisimiri ulianza kujitokeza zaidi mwaka 2012 ambapo ilishika nafasi ya tatu na tangu wakati huo haijawahi kutoka nje ya 10 bora.

Mwaka 2016 haikufanya makosa hata kidogo na ikafanikiwa kupanda kileleni hadi kuwa shule ya kwanza Tanzania kwa ufaulu mzuri. 

Ipo siri iliyojificha ya katika shule hii ambayo ina miaka 16 tangua kuanzishwa kwake.

Mafanikio ya Kisimiri siyo ya kubahatisha

Licha ya shule hiyo kuanzishwa na wanakijiji wa Kasimiri lakini mafanikio yake yamechangiwa zaidi na watu kutoka nje ya nchi ambao wameguswa na elimu ya watoto wa Tanzania. 

Prof. Emil Kalafiat, raia wa Switzerland ni mmoja wa watu waliowahi kuishi karibu na kijiji hicho alipokuwa mdogo na aliweza kusaidia kujenga madarasa na kuweka vifaa muhimu vya kusomea na kuifanya shule hiyo kuwa na mkondo wa kitado cha kwanza hadi cha nne.

Baadaye alijitokeza Mwanamama Prof. Nava Setter ambaye ni mmoja wa rafiki wa Prof. Kalafiat kupitia shirika lake la Talented Foundation akaamua kujenga majengo ya kidato cha tano na sita shuleni hapo pamoja na kuweka  nyenzo  mbalimbali yakiwemo madawati, meza, makabati ya kuhifadhia vitabu.

Nidhamu, motisha na kujituma kwa walimu na wanafunzi kunaibeba Kisimiri.

“Siri kubwa ni motisha binafsi, kwa wanafunzi na walimu kwa kutaka kuwa bora na kufanya vizuri zaidi,” anaeleza Valentine Tarimo, Mkuu wa Shule ya Sekondari Kisimiri.  

Shule ya Kisimiri haina tofauti sana na shule nyingine za serikali katika kukabiliana na changamoto mbalimbali katika ufundishaji lakini bado walimu wa shule hiyo wanajitolea ili wanafunzi waweze kufanya vizuri.

“Japo tuna uhaba wa walimu wa hesabu na fizikia lakini haijaturudisha nyuma huwa tunakodi walimu waje kufundisha wanafunzi vilevile kipindi cha likizo wanafunzi hubaki shuleni kujisomea na walimu wanakuja kuwafundisha,” anaeleza Tarimo.

Nidhamu na ushirikiano umezidi kuing’arisha Kisimiri, kwasababu wanafunzi wakifika shuleni hapo wanaacha historia za walizotoka na kusoma kwa ushirikiano.

Licha ya Kisimiri kufanya vizuri Mkuu wa shule hiyo ameiambia Nukta kuwa anafuraha kuona wanafunzi wa kike katika shule yake wanazidi kupeperusha bendera katika ufaulu.

Tangu kuanzishwa kuwa shule ya vipaji Kisimiri imekuwa shule bora ambayo kila mzazi au mwanafunzi mwenye ndoto ya kufaulu vizuri anaitazama shule hiyo kwa jicho la kipekee.

“Najivunia kusoma Kisimiri, ni shule ambayo inakufanya usome kwa bidii na ufaulu ili usiaibishe shule, halafu pale kila mkiingia kumi bora kidato cha sita mtakaobaki kuna safari ya kutembea vivutio vya utalii kama zawadi na motisha ya kusoma kwa bidii,” anasema Deus Lubacha mmoja wa wanafunzi waliowahi kusoma Kisimiri.

“Pale shuleni wanafunzi wote wanakuwa katika hali ya ushindani na huwa tunawaangalia sana shule nyingine kongwe za vipaji na kama Kibaha, Ilboru, Mzumbe au Tabora na lengo letu kubwa ni kuwa wanafunzi bora.”

   Uboreshaji wa miundombinu katika shule ya sekondari Kisimiri wachangia kuongezeka kwa ufaulu.Picha| Valentine Tarimo.

Enable Notifications OK No thanks