Namna umeme vijijini unavyoweza kutumika kuchochea maendeleo

Daniel Mwingira 0110Hrs   Machi 19, 2018 Habari

  • Wengi waliofikiwa na umeme vijijini bado wanatumia zaidi kuwasha taa na kuchaji simu badala ya kufanya shughuli za uzalishaji.

Arusha. Wakati wanawekewa umeme kwa mara ya kwanza, wananchi wengi wa vijijini huamini ujio wa nishati hiyo huja na fursa lukuki zinazopatikana kirahisi lakini siyo wote hufanikiwa kutimiza fikra hizo.

Ukiachana na matumaini ya wananchi, Mtaalamu wa dhana ya umeme kwa matumizi ya uzalishaji mali  kutoka  Energy Change Lab, Fredrick Mushi anaeleza kuwa hapo awali  hata sehemu kubwa ya  wawekezaji nao walifikiri hivyo pia.

“Wawekezaji binafsi au REA (Wakala wa Nishati Vijijini) walifikiri wanapopeleka   umeme vijijini basi  shughuli za uchumi zingejitokeza zenyewe kama ilivyo mjini.

Lakini imeonekana sehemu kubwa ya matumizi ya umeme ni ya mwanga, kuchaji simu, kuwasha radio au Television,” anasema Mushi kando ya tamasha la Energy Safari 2018 lililofanyika hivi karibuni jijini Arusha.

Pamoja na matumaini makubwa juu ya fursa za kiuchumi zinazojitokeza kutokana na upatikanaji wa umeme, wajasiriamali wengi wa vijijini hukumbana na changamoto katika kuchangamkia fursa hizo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo uelewa hafifu wa namna ya kutumia nishati hiyo na kuongeza thamani ya bidhaa zao.

Ripoti ya Hali ya Upatikanaji wa Nishati ya mwaka 2016 iliyotolewa na Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inaeleza kuwa mwaka huo theluthi moja (asilimia 32.8) ya kaya zote nchini ilikuwa ikipata huduma ya umeme. Kati ya kaya hizo zinazopata umeme, tatu kwa kila nne (asilimia 74.9) zimeunganishwa na umeme kutoka katika gridi ya Taifa, takribani robo (asilimia 24.7) zinapata kutoka katika umemejua na asilimia 0.3 tu zinapata umeme kutoka vyanzo vingine vya nishati hiyo.

Kwanini fursa hazitumiki ipasavyo?

Wataalamu wa masuala ya nishati wanaeleza kuwa jamii zinazonufaika na umeme vijijini maendeleo yao yamekuwa wakati mwingine yakisuasua kutokana na uelewa hafifu wa kuunganisha fursa za kiuchumi na nishati hiyo.

“Hali hiyo kwa sehemu kubwa husababishwa na elimu duni ya ujasiriamali na kukosekana kwa vitendea kazi pamoja na ujuzi wa kutumia vitendea kazi hivyo vinavyotumia umeme,’’ anasema Mushi

Mushi, ambaye hufanya tafiti za masuala ya nishati na maendeleo vijijini, anasema watu wengi  vijijini hawana mazingira rafiki ya  kupata vitendea kazi bora  vinavyotumia  umeme na hata pale wanapofanikiwa kuvipata inakuwa ni changamoto sana kupata huduma za  matengenezo  ikitokea vifaa hivyo  vimepata hitilafu. 

Hawajui wapi pakupata mitaji na namna bora ya kuendesha biashara. Matokeo yake sehemu kubwa ya watumiaji wa umeme vijijini wameshindwa kuzalisha.’’

Hadi Agosti 2016 Serikali ilikuwa imefanikiwa kufikisha umeme katika vijiji 4,395 ikiwa ni zaidi ya theluthi (asilimia 36) ya vijiji 12,268 vilivyopo Tanzania bara kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Nishati.  Vijiji 7,873 vilivyosalia vitafikiwa na umeme ifikapo mwaka 2020.


Njia za kuhamasisha uzalishaji kwa kutumia umeme

Changamoto hizo zimewafanya wawekaziji waliopeleka umeme vijijini kutafuta njia mbadala zitakazochochea ukuaji wa shughuli za uzalishaji katika maeneo wanayohudumia.

Kukosekana kwa shughuli za uzalishaji mali kunawafanya wawekezaji hao kukosa uhakika juu ya uendelevu wa miradi yao. Ili kukabiliana na hali hiyo kwa wakati wa sasa, wawekezaji hao wamekuwa wakiibua miradi mbali mbali na wajasilimali katika maeneo walio wekeza ili umeme utumike kuboresha maisha ya watu ,kuchochea shughuli za kiuchumi mbali ,matumizi ya kawaida ya kuwasha taa na kuchaji simu.

Ensol Tanzania wamefanya jitihada za kuzalisha miradi inayotumia nishati  katika vijiji 11 mkoani Mtwara kwa kupeleka pampu za maji zianazotumia sola na zenye uwezo wa kusambaza lita 50,000 za maji kwa siku. Katika miradi hiyo, kila kijiji kina kamati ambayo itakuwa na ikikusanya mapato kama njia ya uzalishaji mali.

Rafiki Power na Power Corner ni kampuni zingine ambazo zimechukua jukumu la kupeleka vitendea kazi  vya uzalishaji mali katika maeneo wanayozalisha umeme na kuwakopesha wajasiriamali ili watumiaji wa umeme  waweze kuongeza uzalishaji, kupanua huduma na kuzalisha ajira

Kampuni  ya Rafiki Power vile vile imetoa kompyuta zaidi ya 20 zinazotumia umeme unaozalishwa na jua kwa wanafunzi kwenye shule ya msingi katika Kijiji cha Komolo wilayani Simanjiro mkoa wa Manyara ambapo wanafunzi zaidi ya 500 wananufaika na mradi huo.

Hata hivyo, tatizo kuu lilosalia ni  namna ya kutengeneza vifaa hivyo vitakapoharibika kutokana na umbali uliopo kati ya eneo la uwekezaji na mafundi walipo.

Nguzo za umeme zikipita katika moja ya vijiji nchini. Wakazi wa vijijini hawajatumia ipasavyo fursa za umeme uliowafikia kufanya shughuli za maendeleo. Picha ya Mtandao.


Bado kuna fursa lukuki

Mushi anasema njia pekee ni kutafuta wadau ambao wanaweza kutengeneza mazingira rafiki ilikufanya jamii hizo ziweze kunufaika ipasavyo na nishati hiyo ya umeme (Miradi ya umeme vijijini) ili kukuza vipato, kuzalisha ajira na kuboresha hali zao za maisha.

“Wadau kama (Branch International) taasisi ya kifedha inayofikisha hudumaya fedha  maeneo ya vijijini, SIDO, VETA  na wengine waongezeke na wafikishe huduma zao maeneo hayo  ili  kuwasadia hawa wawekezaji kubaki na jukumu moja tu la kuzalisha na kusambaza umeme pekee huku wadau wengine wakijikita katika kuchochea matumizi ya umeme huo kwenye shughuli za uzalishaji mali.

Ili kutatua changamoto hizo  Energy Change Lab pia  imejikita kushirikisha wadau wengi zaidi chini ya mradi wake wa matumizi ya umeme katika shughuli za uzalishaji mali kwa kuanza na miradi ya mfano katika kijiji cha Chang’ombe wilayani Kiteto na Barikiwa wilayani Liwale.

Mushi anasema anatamani vijana wa kitanzania waone ukubwa wa fursa hizi huko vijijini  zinazochochewa na uwepo wa umeme wa uhakika na waache kupoteza muda mijini baada ya masomo yao.

 ”Sio lazima wawekeze kwenye kuanzisha miradi ya umeme bali wanaweza kuingia ubia na kampuni zinazozalisha nishati hiyo ili kuamsha vivutio vingine vya kiuchumi,kama kusambaza vifaa na vitendea kazi, kutoa elimu ya ujasilimali, kutoa huduma ya matengenezo ya vifaa au kujikita katika shughuli za kuongeza thamani kwenye mazao kama vile kusindika maziwa, kukamua mafutaba  kutengeneza mikate ”anaesema Mushi

Related Post