Zoezi uwekaji alama za mipaka Loliondo lakamilika

June 22, 2022 12:13 pm · admin
Share
Tweet
Copy Link
  • Serikali yasisitiza hakuna mtu binafsi anay miliki eneo hilo.
  • Eneo lililowekwa alama ni kilomita za mraba 1500 kati ya 4000.
  • Sasa kutambulika kama Pori Tengefu la Poloreti.

Dar es Salaam. Serikali imesema kuwa zoezi la uwekaji alama ili kuainisha mipaka ya Pori Tengefu la Poloreti katika Tarafa ya Loliondo limekamilika kwa asilimia 100 ili kuhifadhi eneo hilo ambalo ni mazalia ya wanyamapori.

Hatua hiyo imekuja wakati kukiwa na mjadala mpana kuhusu madai ya kuondolewa kwa wananchi jamii ya Wamasai waaoishi katika tarafa hiyo.

Baadhi ya wanaharakati wamekuwa wakidai kuwa wananchi katika eneo hilo wanaondolewa kwa nguvu huku Serikali ikisisitiza kuwa hakuna jambo kama hilo na inachokifanya ni kuweka alama za mipaka na kuimarisha shughuli za uhifadhi.

Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Dk Pindi Chana amesema jumla ya vigingi 422 vimewekwa kutenga eneo la kilomita 1,500 za mraba ambazo ni Pori Tengefu la Poloreti (Loliondo).

Balozi Chana aliyekuwa akizungumza katika mjadala wa mtandaoni uliohusu maendeleo ya zoezi la uwekaji alama za mipaka Tarafa ya Loliondo na zoezi la uhamaji wa hiari wa wakazi Ngorongoro leo Juni 22 amesema hatua hiyo imechukuliwa ili kutunza eneo hilo nyeti ambalo ni mazalia ya wanhyamapori na chanzo muhimu cha maji. 

“Kabla ya hapo eneo hili lote lilikuwa pori tengefu kilomita za mraba 4,000, lakini sasa Serikali ikasema hizi 2,500 tuwaachie wananachi, hili eneo la kilomita 1500 la hifadhi tulitunze.

 “Kwa hiyo kwa tangazo la Serikali namba 421 la tarehe 17 Juni 2022  sasa linatangazwa kuwa Pori Tengefu la Poloreti na eneo hili ndipo mapito ya nyumbu, wanapita eneo hilo, wanazaliana eneo hilo, kuna vyanzo vya maji na maji haya ndiyo yanasaidia hata upande wa Serengeti,” amesema Waziri Dk Chana. 

Uwekaji wa alama za mipaka unatokana na uamuzi wa Serikali hususani Baraza la Mawaziri liloketi mwaka 2019 wa kuhakikisha alama zote za mipaka katika eneo hilo zinazoonekana zinawekwa katika maeneo yote ya hifadhi ili kuepusha wananchi kuvamia na kuzuia migogoro isiyo ya lazima.

“Unaposema hii ni hifadhi lazima kuwe na kigingi (beacon) pamoja na majina nukta yake (coordinate) kwa hiyo hili ni zoezi la kawaida kabisa,” amesisitiza Chana. 

Tarafa ya Loliondo ni sehemu ya Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha. Wilaya hiyo ina jumla ya tarafa tatu ikiwemo  Sale na Ngorongoro ambayo inajumisha Mamlaka ya Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro ambayo ni kivutio muhimu cha watalii.


Zinazohusiana:


Mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongela amesema uwekezaji wa alama za mipaka Loliondo ulikuwa na umuhimu mkubwa ili kudhibiti watu kuvamia maeneo ya pori tengefu lilipo katika tarafa hiyo.Amesema wakati wa utekelezaji wa zoezi hilo haki za binadamu zimezingatiwa na limekamilika vizuri, licha ya kuwepo kwa madai ya baadhi ya Wamasai kujeruliwa.

Mongella amekanusha madai ya baadhi ya watu wanaosema kuwa eneo hilo limeuzwa kwa mwekezaji.

 “Pori la Loliondo halijawahi kumilikiwa na mtu binafsi ni mali ya umma chini ya usimamizi wa Serikali….mimi nataka ushahidi wa mtu ambaye atasema pori hili ni mali ya mtu.

“Mimi kama mkuu wa mkoa sijapata huo ushahidi na usimamizi wake uko chini ya mamlaka za mfumo wa  serikali ambazo wanasimamia maeneo mengine mengi nchini,” amesema Mongella.

Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa katika ofisi ya Geneva, Uswizi, Balozi Hoyce Temu amesema jumuiya ya kimataifa zinapaswa kuelewa kuwa zoezi la kuweka alama ni la kawaida katika shughuli uhifadhi na wananchi hawajaondolewa katika eneo la Loliondo.

“Wamerudi katika kanuni za malengo endelevu ambazo ni kuheshimu sayari, kujali jamii, kujenga jamii ya kidemokrasia na kutoacha mtu  myuma ndo kilichotokea kuonekana kwamba sisi Tanzania tunafanya kwa ajili ya wananchi wetu,” amesema Balozi Temu.

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks