Kilichonivutia zaidi nilipotembelea Zanzibar
- Ni pamoja na ukarimu wa watu na mandhari nzuri ya historia ya visiwa hivyo.
- Usafiri wa umma wa Zanzibar ni marufuku kubanana.
- Gari aina ya Alphard na pikipiki za Vespa ni maarufu visiwani humo.
Dar es Salaam. Baada ya takriban saa moja na nusu ya kuelea kwenye mawimbi nikitokea jijini Dar es Salaam, nilikaribishwa na harufu ya karafuu iliyotokea kwenye shehena ya mzigo uliokuwa kwenye kenta iliyopita mbele yangu.
Mmmmmmh!, hewa ya Zanzibar iliyojaa marashi ya udi ni ya aina yake. Sura nilizoziona mbele yangu zilikuwa sura zinazosema “Karibu Rodjazz, hapa ndiyo Zanzibar yenyewe.”
Majengo ya kale, sauti ya mawimbi ya bahari na mchanganyiko wa watu wa mataifa mbalimbali katika ardhi moja ni tofauti na sehemu zote nilizowahi kukanyaga na kiatu changu.
Mara yangu ya kwanza kutembelea Zanzibar ilikuwa mwaka 2018. Hata hivyo, sikupata muda wa kuzunguka kisiwani humo kwani nilienda kikazi na ilikuwa ni “shaa shaa” kama vijana wa mjini wasemavyo kumaanisha haraka haraka.
Licha ya kuwa awamu hii pia ilikuwa kikazi, walau zilihusisha uzuraraji wa hapa na pale ili kukutana na watu kwa ajili ya mahojiano.
Muonekano wa fukwe safi za Zanzibar. Picha| Rodgers George.
Sijatembelea Zanzibar yote lakini hivi ndiyo vitu nilivyovipenda katika siku nne nilizochangamana na watu wa visiwani humo:
Usafiri wa umma
Ni tofauti na Dar es Salaam. Tena tofuati kubwa sana. Mbali na kuwa foleni ni za kutafuta kwa darubini, usafiri wa umma kwa zanzibar ninaweza sema ni usafiri ambao nimeupenda kuliko kote ambako nimewahi kufika. Ni pamoja na Arusha, Dodoma na Mwanza.
Kwa Zanzibar, basi zinasafiri kwa “level seat na kila basi limewekewa kikomo cha idadi ya abiria. Mara zote nilipotumia usafiri huu nilikaa tena vizuri na mara kwa mara nilikuwa nikijibu “Wa-Alaikum-Salaam” kwani takriban kila aliyeingia, alisalimia tena kwa sauti, “Salam Alaikum”
Tumezowea jijini Dar es Salaam, konda kusema sogea mlangoni ushuke lakini kwa Zanzibar, hakuna kusogea mlangoni. Ni utasubiri gari lisimame na utatoka kwenye kiti chako na kushuka.
Ukiwa Zanzibar, utakutana na pikipiki nyingi za Vespa kwani ndiyo usafiri binafsi wa wakazi wengi wa visiwa hivyo. Mji huo pia umepambwa na gari za Toyota Alphard ambazo hutumika kwa ajili ya usafiri wa kukodi.
Usafiri maarufu wa abiria wa ‘chai maharage’ visiwani Zanzibar. Picha| Rodgers George.
Ukarimu wa watu wa visiwani
Hauwezi ukakaa umeshangaa shangaa ukiwa Zanzibar na mtu asikuulize kama una tatizo. Ni kana kwamba wakazi wa visiwani hawapendi kuona mtu una mawazo. Kwa mara kadhaa nilizojikuta nimeuma midomo yangu kuonesha sijui wapi naelekea, alijitokeza mtu na kuulizia changamoto yangu.
Nilipomwambia nimepotea, alinipeleka hadi nilipotaka kwenda na bila kuomba pesa ya kunielekeza. Kwa Dar esSalaam, huenda utanyooshewa vidole au kuambiwa panda boda boda. Hahaha natania tu. Lakini kuna ukweli ndani yake.
Kwenye shughuli zangu za kila siku, ipo siku nilipanda basi ndogo huko zinaitwa “chai maharage” kwa mimi ambaye ni mrefu na siyo mzoefu wa gari hizo, nilijigonga kichwani wakati wa kushuka na gari zima lilinipatia pole na kwa aibu, nilijibu “asante”.
Usalama wa mali zako
Kwa sehemu zingine, huenda ukapaki gari yako ukiwa kwenye mgahawa na kukuta kioo cha pembeni kimebebwa. Wenyeji wa Zanzibar, waliniambia kuwa unaweza kuacha pikipiki barabarani na ukaikuta hapo hapo asubuhi.
Niliona magari yakiwa yamepaki nje ya kumbi za starehe bila hata ya kuwepo walinzi. Watu wakiwa wameanika nguo kwenye nyumba zisizo na fensi bila ya wasiwasi na viatu vikiwa nje ya nyumba.
Ukifika Zanzibar, utaona pikipiki nyingi aina ya Vespa. Picha| Rodgers George.
Maneno mapya niliyojifunza
Hakika Kiswahili cha bara na visiwani ni tofauti, siyo tu kimatamshi bali mantiki pia. Kwa Zanzibar, mabomba ya maji yanaitwa mfereji, karanga zinaitwa njugu na ukitaka kumwambia dereva akushushe mahala fulani, basi utamwambia “niweke”.
Mbali na mahaba yote niliyoyajenga na Zanzibar, yapo yaliyonipa shida. Kati ya yote ni gharama ya usafiri hasa wa pikipiki. Kwa baadhi ya sehemu imezoeleka kuwa usafiri wa pikipiki ni usafiri wa bei nafuu hasa kama mtu una haraka.
Mbali na kutokuwepo kwa kampuni za usafiri zinazoendeshwa na programu tumishi yaani Apps kama Uber na Bolt, umbali ambao Dar es Salaam ningetumia Sh1,500 nililazimika kutumia Sh3,000. Tusiongelee gharama za usafiri wa taxi sasa.
Kwa sasa nimefika Unguja tu, nategemea siku za usoni nifike na Pemba pia. Hadi siku hiyo itakapofika, wacha nipambane na hali yangu hapa Dar es Salaam.