Zifahamu nauli mpya mabasi yaendayo haraka, teksi mtandao
- Nauli mpya kwa mabasi yaendayo haraka ni Sh750 kutoka Sh650.
- Teksi mtandao zenye uwezo wa kubeba abiria wasiozidi sita, nauli ni Sh4,000 hadi Sh5,000.
- Zitaanza kutumika siku 14 baada ya tangazo kutoka.
Dar es Salaam. Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imetangaza nauli mpya za teksi mtandao, pikipiki mtandao na mabasi yaendayo haraka (BRT) zitakazoanza kutumika kuanzia siku 13 zijazo.
Nauli mpya kwa mabasi yaendayo haraka ni Sh750 kutoka Sh650 iliyokuwa awali kwa njia kuu na Sh500 kutoka Sh400 kwa njia mlisho sawa na ongezeko la Sh100.
Abiria watakaounganisha njia kuu na njia mlisho watalipia Sh900 na kwa njia ya Kimara hadi Kibaha watalipia Sh700.
Mkurugenzi Mkuu wa LATRA Habibu Suluo amesema teksi mtandao zenye uwezo wa kubeba abiria wasiozidi sita, nauli ni Sh4,000 hadi Sh5,000 kwa safari isiyozidi kilomita moja.
“Nauli ya kuanzia safari ni Sh800 hadi Sh1,300, nauli kwa kilomita ni Sh1,000 hadi Sh1,200, nauli kwa dakika ni Sh80 hadi Sh150,” amesema Suluo jana Januari 3,2022 jijini Dodoma.
Kwa upande wa pikipiki mtandao, pikipiki za abiria wawili nauli itakuwa Sh1,000 hadi Sh1,500. Pipipiki za abiria wasiozidi watatu nauli itakuwa Sh2,000 hadi Sh2,500 ndani ya kilomita moja.
Safari ikizidi itaongezeka kwa Sh300 hadi Sh600 kwa kila kilomita moja na kama kutakuwa na vikwazo kama foleni nauli itaongezeka kati ya Sh50 hadi Sh90 kwa kila dakika.
Akizungumza na Wanahabari, CPA Suluo amesema, tangazo hilo ni kwa mujibu wa Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini Sura ya 413, ambapo LATRA imepewa jukumu la kupanga nauli za vyombo vinavyotoa huduma za usafiri ardhini kibiashara.
“Mapendekezo haya ni kwa mujibu wa sheria lakini kama kuna mdau yeyote ana malalamiko au hakubaliani na haya alete malalamiko yake ndani ya siku 14 kutoka leo,” amesema Suluo,” amesema.
Suluo amesema bado wapo kwenye vikao vya masikilizano na wadau kuhusu nauli za treni ya mwendokasi (SGR) na tayari wamepokea mapendekezo kutoka kwa Serikali na bei kamili ya nauli hizo itatangazwa mwezi ujao baada ya kuwasili kwa mabehewa nchini.
Hata hivyo, LATRA imelikataa ombi la kuongeza nauli kwa wanafunzi na kubakia Sh200 iliyokuwepo.