Zawadi 3 za kushangaza siku ya wapendanao
- Ni pamoja na maua, mlo pamoja na manukato.
- Vitu vinavyodumu kama nguo, au vito vyatajwa zaidi
Dar es salaam. Ni utaratibu tu ambao watu waliamua kujiwekea na kuufuata, wa kuifanya Februari 14 kuwa siku ya kuwaenzi, au kuwatendea jambo mahususi au maalumu wale wawapendao.
Utamaduni huu ulianzia nchini Roma na kuenea duniani kote. Ulianzishwa ili kumuenzi Padri Valentino ambaye alikiuka katazo la mtawala wa Roma wakati huo Mfalme Claudius II, aliyezuia vijana kufunga ndoa bali kujiunga na jeshi na kwenda vitani.
Padri huyo aliendelea kufungisha ndoa kisiri ndipo mfalme akaamuru akamatwe na anyongwe. Miaka kadhaa badaaye Warumi wakaamua kuiteua siku hii kuadhimisha maisha ya mtetezi wa wapendanao.
Siku hii imekuwa ikitafsiriwa tofauti na watu kulingana na mitazamo na tamaduni za eneo husika. Baadhi wanadai ni siku maalum kwa ajili ya wapenzi pekee na wengine wakidai ni siku ya kuonyesha upendo kwa mtu yeyote awe ndugu, jamaa au rafiki.
Zawadi ni miongoni mwa mambo ambayo hutupiwa macho na wengi katika kuadhimisha siku hii, jambo ambalo huwaumiza vichwa baadhi huku wakiwaza ni zawadi ipi itamfaa yule ampendaye.
Kama wewe ni miongoni basi ondoa shaka, Nukta Habari (www.nukta.co.tz) imefanya utafiti mdogo kuhusu aina ya zawadi ambazo zinaweza kukufaa kwa ajili ya yule umpendaye.
Mlo wa pamoja
Ndio! Unaweza kuifanya siku hii kuwa ya kipekee kwa kuandaa mlo wa pamoja na umpendaye, inaweza kuwa nje kidogo ya mji au sehemu ambayo ni mpya machoni pake. Zingatia chakula chake pendwa kwenye mlo huo, utakuja kunishukuru.
Zinazohusiana
- Tofauti na ngono, haya ndiyo unayoweza kufanya kulinda penzi lako
- Unakutana na mpenzi wako kwa mara ya kwanza? Zingatia haya
Vitu vinavyoweza kudumu
Usishangae, ni neno la jumla lakini ni rahisi tu hapa unaweza kununua nguo, kiatu, hereni, bangili au mkufu. Nia ni kutengeneza kumbukumbu ya kudumu kwa sababu watu wengi hupenda kuwa na kumbukumbu nzuri walizotengeneza na wawapendao.
“Ningependa anipe kitu ambacho naweza kukaa nacho kwa mda mrefu, itakuwa inanikumbusha upendo wangu kwake, “ amesema Beatrice Wangoma, mkazi wa jijini Dar es Salaam.
France Kibassa ambaye ni mjasiriamali wa mkoani Dodoma ameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kuwa maua ni miongoni mwa zawadi ambayo mtu anaweza kumpatia mpendwa wake lakini ni vizuri ikasindikizwa na zawadi nyingine kama pesa, simu, peremende au chokuleti.
“Maua na mishumaa ni zawadi nzuri zinazopendwa sana na wanawake, unaweza kuyaambatanisha na zawadi nyingine kama uwezo unaruhusu, itamfanya ajisikie vizuri zaidi, “ amesema Kibassa.
Usisahau manukato
Mshangaze mpendwa wako kwa kumtafutia manukato mazuri ayapendayo au ambayo umeyafanyia utafiti na kubaini yanavutia. Atakuwa anajisIkia vizuri kila mara anapoyatumia.
tembelea wataalam wa manukato wakushauri yanayoweza kumfaa mpendwa wako kama huna utaalamu wa kutosha.
Umemuandalia nini mpenzi wako siku ya kesho? Una zawadi tofauti na tulizoaorodhesha hapo juu?