Zaidi ya Sh469 bilioni za EU zitakavyoboresha maisha ya Watanzania

March 23, 2022 6:04 am · Herimina
Share
Tweet
Copy Link
  • Fedha hizo ni msaada kutoka Umoja wa Ulaya (EU)
  • Zitatumika kuimarisha masuala ya kijinsia, kuboresha miji ya Tanga, Mwanza na Kisiwa cha Pemba.
  • Pia zitaendeleza mradi wa kidijitali wa Serikali Mtandao.

Dar es Salaam. Ni dhahiri Watanzania wataboresha maisha yao katika masuala ya kidijitali na kijamii baada ya ushirikiano wa Tanzania na Umoja wa Ulaya (EU) kuimarika katika siku za hivi karibuni. 

Tanzania imepokea msaada wa Euro milioni 180 sawa na zaidi ya Sh469 bilioni kutoka Umoja wa Ulaya (EU) kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo.

Miradi hiyo ni pamoja na kuimarisha masuala ya kijinsia, kuboresha miji ya Tanga, Mwanza na Kisiwa cha Pemba, pamoja na kuendeleza mradi wa kidijitali wa Serikali Mtandao.

Mikataba ya msaada huo imesainiwa Machi 22 Jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali Emmanuel Tutuba pamoja na Balozi wa Ulaya nchini Tanzania Manifredo Fanti.

Tutuba amesema kuwa fedha hizo ni sehemu ya ufadhili wa Euro milioni 703 (zaidi ya Sh1.8 trilioni) ambazo Umoja wa Ulaya umetenga kwa ajili ya kutekeleza miradi mitatu, ikiwa ni makubaliano ya ushirikiano wa miaka 7 kati ya Tanzania na Umoja huo kuanzia 2021 hadi 2027.

“Mradi huu pia ambao utoaji wake wa fedha utapitia utekelezaji wa kibajeti, unahusisha kuwawezesha wanawake kiuchumi, ikijumuisha fursa endelevu za teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama) pamoja na kuimarisha usawa katika uongozi na maamuzi ikiwemo haki, amani na usalama,” amesema Tutuba.


Zinazohusiana:


Kati ya fedha hizo, Sh195 bilioni zimeelekezwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), kwa ajili ya kuboresha mazingira ya miji ya Tanga, Mwanza na Kisiwa cha Pemba ili kuwezesha upatikanaji wa mapato ya ndani na maendeleo jumuishi ya uchumi katika maeneo ya mijini kwa makundi ya wanawake na vijana.

Mradi wa kidijitali wa Serikali Mtandao umetengewa Euro milioni 35 sawa na zaidi ya Sh90 bilioni zitakazotumika kuboresha huduma za mitandao serikalini, kuongeza huduma za mitandao mijini na pembezoni mwa miji na kuendeleza sekta ya huduma za kifedha hapa nchini na kikanda.

“Serikali inathamini msaada huu ambao umetumika kutekeleza miradi ya vipaumbele vya Serikali ikiwemo sekta ya miundombinu ya usafiri, viwanja vya ndege, nishati, kilimo, pamoja na miradi ya mazingira inayolenga kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi,” amesema Tutuba.

Uwekezaji wa umoja huo hapa nchini tangu mwaka 1975, umefikia thamani ya Euro bilioni 2.7 sawa na Sh6.6 trilioni.

Balozi wa Ulaya nchini Tanzania Manifredo Fanti amesema kuwa miradi iliyosainiwa itafungua fursa za kiuchumi kwa wanawake na vijana na kuboresha mazingira ya biashara kwenye maeneo yanayoguswa na miradi hiyo, pamoja na kuboresha haki kwa makundi mbalimbali.

Fanti ameongeza kuwa kurejea kwa Benki ya Uwekezaji ya Umoja wa Ulaya kufanya shughuli zake Tanzania kwa kushirikiana na sekta ya umma na binafsi ni kielelezo cha ushirikiano imara uliopo kati ya pande hizo mbili na kwamba umoja huo utaongeza ufadhili kwa Tanzania.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW