EU yaipatia Tanzania msaada wa Sh455.2 bilioni miradi ya maendeleo

July 4, 2023 11:50 am · admin
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni sehemu ya utekelezaji wa awamu ya kwanza ya ushirikiano kati ya EU na Tanzania
  • Zitasaidia Serikali katika utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2023/24

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imepokea Sh455.22 bilioni kutoka Umoja wa Ulaya (EU) kwa ajili ya kutekeleza miradi mitatu ya maendeleo ukiwemo wa uchumi wa bluu utakaogharimu Sh279.2 bilioni.

Miradi mingine iliyosainiwa hii leo Julai 4, 2023 ni pamoja na mradi wa usimamizi wa mifumo ya fedha na kukuza sekta binafsi wenye gharama ya Sh160.79 bilioni pamoja na mradi wa kuimarisha mahusiano kati ya EU pamoja na Tanzania wenye thamani ya Sh15.23 bilioni.

Kutolewa kwa fedha hizo ni utekelezaji wa awamu ya kwanza ya makubaliano ya ushirikiano wa miaka saba kati ya Tanzania na EU yaliyosainiwa mwaka 2020 na kuanza kutekelezwa mwaka 2021.

Miongoni mwa vipaumbele ni pamoja na rasilimali watu pamoja na ajira, uongozi bora pamoja na mapinduzi ya kijani.

Fedha hizo zitaisaidia Tanzania kutekeleza bajeti yake ya Sh44.39 trilioni kwa mwaka 2023/24 iliyoanza Julai Mosi 2023, ambapo asilimia 12 ya bajeti hiyo yaani Sh5.47 trilioni ni kutoka kwenye misaada na mikopo nafuu.

Ili kutekeleza miradi itokanayo na vipaumbele hivyo, EU imetenga Euro milioni 703 sawa na Sh1.81 trilioni ambapo kwa awamu ya kwanza itakayokamilika 2024 Serikali ya Tanzania itapokea Sh1.07 trilioni sawa na asilimia 60 ya fedha iliyotengwa.

Mpaka sasa tayari Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Fedha na Mipango imekwisha andaa miradi sita yenye thamani ya Sh998.57 bilioni itakayotekelezwa kwa kipindi cha miaka miwili.


Soma zaidi


‘Ni mshirika muhimu’

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan aliyekuwa akizungumza katika hafla ya kupokea fedha hizo leo Julai 4, 2023 amewaambia washiriki kuwa ushirikiano kati ya EU na Tanzania umesaidia kuboresha baadhi ya sekta kama miundombinu, maendeleo ya teknolojia, usawa wa kijinsia pamoja na ukuaji wa uchumi.

“Kwa miongo sasa EU amekuwa mshirika wetu muhimu kwenye maendeleo, hii inathibitishwa na misaada ya kifedha ambayo Tanzania tumepokea tangu mwaka 1975…Tanzania mpaka sasa imepokea jumla ya Sh5.9 trilioni kama msaada  pamoja na kiwango kikubwa cha fedha kama mikopo nafuu,” amesema Rais Samia jijini Dodoma.

Ushirikiano kati ya Tanzania na EU umeimarika tangu Rais Samia alipoingia madarakani ambapo Februali 18 mwaka 2022 alikutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Kamisheni ya  EU Ursula von der Leyen jijini Brussels  nchini Ubelgiji.

Mazungumzo hayo yalifungua fursa ya Tanzania kuanza kufaidi misaada iliyokwama kutoka EU mara baada ya uhusiano baina ya pande mbili kuwa ya kusuasua katika awamu ya tano.

Rais Samia ameuomba umoja huo kufadhili miradi mingine ambayo haikuwepo katika makubaliano ya awali ambayo ni mradi wa Kujenga Kesho Bora (BBT), pamoja na kuongeza uwanja wa ndege wa Mwanza katika mradi wa uboreshaji wa viwanja vya ndege vya pembezoni.

EU kuendelea kutoa misaada ya kibajeti

Kwa upande wake Balozi wa EU nchini  Manfredo Fanti amewaambia washiriki wa hafla hiyo kuwa umoja huo utaendelea kushirikiana katika maeneo ya kimkakati kufanikisha utekelezaji wa miradi jambo litakalochochea ukuaji wa uchumi.

“Msaada wa kibajeti utaendelea kutolewa kuchochea mapinduzi ya kisekta, maendeleo vijijini, kukuza teknolojia, kilimo, uchumi wa bluu pamoja na nishati,” amesema Fanti.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW