Zaidi ya Sh118 bilioni za Sweden kupambana na umaskini Tanzania
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Emmanuel Tutuba na Balozi wa Sweden nchini Tanzania, Anders Sjoberg wakisaini Hati ya makuliano ya msaada wa Sh118 bilioni zilizotolewa na nchi hiyo kwa ajili ya Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini kupitia Mfuko wa TASAF, katika Ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania, Jijini Dar es Salaam. Picha| Wizara ya Fedha na Mipango.
- Zitaongeza fursa za kiuchumi na kijamii kwa kaya maskini.
- Lengo ni kupunguza ufukara katika kaya maskini
- Watoto na wanawake kufaidika na fedha hizo.
Dar es Salaam. Huenda idadi ya Watanzania wanaoishi katika kaya maskini wakapungua mwaka huu, baada wadau wa maendeleo kuipatia Serikali fedha kwa ajili ya kuziinua kaya hizo kiuchumi na kijamii.
Serikali ya Sweden imeipatia Tanzania msaada wa Sh118 bilioni kwa ajili ya utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini Awamu ya Pili kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).
Hati za makubaliano ya msaada huo zimetiwa saini Jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Emmanuel Tutuba na Balozi wa Sweden nchini Tanzania, Anders Sjöberg.
“Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini Awamu ya Pili ulianza kutekelezwa mwaka 2020 na unatarajiwa kukamilika mwaka 2023, umepangiwa kutekelezwa kwa gharama ya dola za Marekani milioni 883.3 sawa na Sh2.02 trilioni na Sweden imesaidia jumla ya dola na Marekani milioni 237 sawa na Sh542.2 bilioni,” amesema Tutuba.
Mpango huo umelenga kuongeza fursa za kiuchumi na kijamii kwa kaya za walengwa pamoja na kulinda na kuimarisha rasilimali watu kwa kutoa ruzuku kwa kaya zilizoko kwenye mpango huo.
“Hadi kufikia Desemba 2020 zaidi ya kaya milioni 1 zilihakikiwa Tanzania Bara na Zanzibar na kuingizwa katika mpango huo huku kaya 56,800 kazi ya kuzihakiki inaendelea ili nazo ziweze kuingizwa kwenye mpango huo ulioonyesha mafanikio makubwa,” amesema Tutuba.
Kuanzia mwezi Julai 2020 hadi Julai 2021, kaya za walengwa 871,654 zililipwa Sh171.8 bilioni na matokeo yake ni kuwa ufukara ulipungua kwa asilimia 8 kwa walengwa.
Aliyataja baadhi ya mafanikio mengine ya mradi huo kuwa ni kuongezeka kwa idadi ya watoto wanaoandikishwa shule kutoka kaya za walengwa kwa asilimia 6, kuongezeka kwa mahudhurio ya watoto wenye miezi 0 hadi 24 kwenye vituo vya afya na kuongezeka kwa walengwa wenye nyumba bora za kuishi.
“Kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa Serikali ya Sweden kwa msaada huu muhimu ambao unaendana na Mapango wetu wa Maendelo wa Miaka Mitano,” amesema Tutuba.
Latest