Youtube yampoteza “Grandpa Kitchen” aliyewapikia yatima, wasiojiweza

November 5, 2019 8:35 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link

Maisha ya Reddy, yanaonyesha kuwa umri siyo kikwazo cha mtu yeyote kufikia ndoto zake. Picha| Mtandao.


  • Ni mzee Narayana Reddy, raia wa India aliyefariki akiwa na miaka 73.
  • Ameacha akaunti ya YouTube ikiwa na wafuasi zaidi ya milioni 6.
  • Atakumbukwa kwa mapishi na moyo wake wa kuwasaidia watu wasiojiweza wakiwemo yatima.

Dar es Salaam. Wakati wazee wengi waliostaafu wakigeukia kilimo na ufugaji, na wengine wakiwa ni watu wa kukaa nyumbani, wapo wazee waliochagua kuwa tofauti ambao kati yao ni mzee Narayana Reddy raia wa India aliyefariki hivi karibuni. 

Amefariki akiwa na umri wa miaka 73 mwaka huu, lakini historia yake kwenye ulimwengu wa mapishi haitafutika kirahisi katika mioyo ya watu wasiojiweza duniani. 

Reddy ambaye licha ya umri wake kumtupa mkono, aliushangaza ulimwengu kwa mapishi yake na zaidi uwezo wake wakutumia mitandao ya kijamii kwa ajili ya kubadilisha maisha ya watu wanaomzunguka.

Unaweza kufikiri alikuwa akipika kwa ajili ya biashara au kujinufaisha mwenyewe, ajabu ni kwamba mzee huyo alifanya hivyo kwa ajili ya kuwalisha watoto yatima na ambao hawana uwezo wa kujinunulia chakula.

Kudhihirisha kuwa utoaji ni moyo na siyo utajiri, Reddy halikuwa hana jiko la kisasa ama vyombo vya kisasa kwa ajili ya kupikia. Ili kuhamasisha umoja na ushirikiano, Reddy alipakua chakula chake kwenye masinia makubwa ambayo watoto walikula pamoja baada ya chakula kuiva.

Mbali zaidi, hata jiko alilopikia Reddy lilikua la mafiga matatu huku akitumia njia za asili za kihindi katika kupika vyakula hivyo ambavyo viliwawezesha watu wasiojiweza kujiona wana thamani kwenye jamiii.


Soma zaidi:


Pia alitumia mtandao wa Youtube kuonyesha ufundi wa kupika na kuhamasisha watu kuwasaidia watu wasiojiweza hasa yatima kwa kuwapatia chakula bora. 

Reddy alitumia mtandao huo kwa kufundisha namna ya kupika vyakula mbalimbali vikiwemo biriani, vitafunwa kama donati na hata kuku kama wanavyopikwa kwenye migahawa ya Kentucky Fried Chicken (KFC).

Hata wakati aliokuwa akiwasaidia wakidhani angeishi miaka mingi ili waendelee kumfaidi, Oktoba 27, 2019 ilikuwa tarehe ya majonzi kwa wafuasi wake na hata watoto ambao alikuwa akiwahudumia kwani wakati baadhi ya wahindi wakigawa pipi na kuwasha mishumaa kusherehekea sikukuu ya Diwali, mzee huyo alivuta pumzi yake ya mwisho.

Maisha yake yanafundisha wazee wengi ambao huona muda wao umeisha na hivyo kushindwa kufanya kile wanachopenda kwa kuona kuwa wamechelewa. 

Maisha ya Reddy, yanaonyesha kuwa umri siyo kikwazo cha mtu yeyote kufikia ndoto zake hasa ikizingatiwa kuwa mzee huyo mpaka anafariki alikuwa na wafuasi milioni 6 katika mtandao wa Youtube.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW