Yaliyojificha ndani ya programu mpya endeshi ya iPhone

June 24, 2020 11:58 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni kizazi kipya cha mfumo endeshi wa wa simu (IOS14) ambao unatumika na simu za iPhone. 
  • iOS14 ina maktaba ya app yenye muonekano ulioboreshwa zaidi pamoja na wiji za takwimu.
  • Kisaidizi cha sauti nacho kimeboreshwa kiasi cha kukuruhusu kufanya mambo mengine wakati ukiwa unawasiliana nacho.

Dar es Salaam. Kampuni ya Apple imetangaza ujio wa kizazi kipya cha mfumo endeshi wa wa simu (iOS14) ambao unatarajiwa kutumika na simu za iPhone zinazotengenezwa na kampuni hiyo.

Mfumo huo unaotarajiwa kuzinduliwa mwishoni mwa mwaka huu utawapatia watumiaji wa simu za iPhone vitu vipya ambavyo havikuwepo katika matoleo ya mifumo iliyopita. 

“Tutaendelea kubuni na kuvumbua vitu vipya vya kuwafurahisha watumiaji wetu,” inaeleza sehemu ya taarifa ya Apple. 

Ni nini kipya kinachokuja na mfumo wa  iOS14?

Maktaba ya app (App Library) yenye muonekano mzuri

Kwa mtu ambaye simu yake ina programu tumishi nyingi, huenda anapata tabu kutafuta programu moja kati ya nyingi alizonazo.

iOS14 inaondoa tabu hiyo kwa kuziweka programu tumishi zote zinazohusiana katika kundi moja. Hivyo utapunguza muda unaotumia kutafuta programu tumishi ya WhatsApp kwa kuikuta ikiwa kwenye kundi la programu tumishi zote za burudani.

Pia utapunguza kurasa za programu tumishi zako kutoka kurasa nne na kufikia walau kurasa mbili au moja za skrini ya kioo chako.

Pia intelijensia ya simu ikikuwekea programu (Apps) ambazo unazitumia mara kwa mara katika kundi moja na apps ulizoziongeza karibuni katika kundi lingine na yote hayo, yapo katika ukurasa wa kwanza.

iOS14 inaondoa tabu hiyo kwa kuziweka programu tumishi zote zinazohusiana katika kundi moja. Picha| Cnet.

Widgets zilizo na utajiri wa takwimu

Kwa mujibu wa Apple, widgets (wiji) kwenye iOS14 zinakuja na takwimu ili kumsaidia zaidi mtumiaji kufanya maamuzi.

Mbali na kuja katika saizi tofauti zinazochangamana na apps kwa urahisi, Apple imesema Widget ya “Smart stack” inatabiri ni kipi utakuwa unahitaji kwa wakati huo.

“Asubuhi itakuonyesha habari muhimu, mchana itakuonyesha vitu ulivyopanga kufanya vikiwemo vikao,” ameeleza Makamu wa Rais wa kitengo cha uhandisi wa programu wa Apple, Craig Federighi.

Programu ya “Picture in picture”

Hii ni mpya ambayo inawezesha mtu kutumia apps zake wakati akitazama video au akiwa kwenye simu za video za programu ya “Face Time”.

“Picture in picture” inakusaidia kuendelea na shughuli zako za video huku ukiendelea kufanya mambo mengine na app zingine. Siyo lazima kuacha.

Kama wewe ni mtumiaji wa Netflix, hii inaweza isiwe ngeni kwako kwani pale unapotoka kwenye mtandao huo, video huendelea kuonekana kwenye skrini yako japo kwa udogo. 

Pia, unaweza kuiweka sehemu unayoona inafaa kuwepo yaani juu, katikati, kulia na hata kushoto.

Maboresho ya siri ambaye ni msaidizi wa sauti

Katika kizazi kilichopita cha iOS 13.5.1, Siri ililazimika kuziba skrini yako yote wakati inakusikiliza. Hiyo iliweka ugumu katika kufanya kazi zako kama ulikuwa unasoma.

Kwa iOS14, Siri ambayo ni msaidizi anayeamuliwa kwa sauti kufanya mambo mengi kama kuseti alamu ya asubuhi na kukusomea taarifa ya habari hazibi tena skrini yako yote na hivyo anakuacha uendelee na kazi zako zingine na hata kufanya mrejeo wa majibu yako.


Zinazohusiana


Mbali na hayo, Apple imesema kupitia iOS14, kamera yako itakuwa na nguvu za kupiga picha kwa haraka zaidi na kutafsiri (Kama ilivyo kwa google translate) kupitia Siri.

Kizazi cha iOS14 kinaweza kufanya kazi kwenye simu za iPhone 6s, Iphone SE ya mwaka 2016 na matoleo yaliyofuatia baada ya hapo yakiwemo iPhone 7,  X na Pro.

Siyo simu tu. Apple imefanya maboresho kwenye iPad, saa, kompyuta na hata televisheni. Unahitaji kufahamu kipi? Tuandikie kupitia mitandao yakijamii.

Enable Notifications OK No thanks