Yakufahamu kuhusu dhamana ya bidhaa, huduma

September 22, 2021 12:18 pm · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Hutumiwa na wafanyabiashara kuhakikisha ubora wa bidhaa zao.
  • Dhamana hizo zinatakiwa kusainiwa ili kukidhi vigezo kisheria.
  • Hakikisha unapata dhamana ya maandishi kama bidhaa unayonunua ina huduma hiyo.

Dar es Salaam. Unaposikia matangazo ya bidhaa mpya, bila shaka neno “warentii” kama watangazaji wanavyosema huambatana na matangazo yao.  Wapo wanaosema “warentii” na wanaosema “garentii” yote yakiwa ni maneno ya kuhakikisha ubora wa bidhaa.

Hata hivyo, garantee (guarantee) na warantii (warrantee) ni maneno ya Kiingereza ambayo maana yake ni dhamana. 

Muuzaji anayekuuzia bidhaa yenye dhamana ya muda fulani, maana yake ni kuwa unaweza kubadilishiwa kitu hicho pale kinapokuwa na mushkeri ndani ya kipindi ulichopewa.

Mbali na kubadilishiwa, endapo kitu hakitokuwa na ubora uliotangaziwa, kitatengenezwa pale kitakapoharibika na pia kukirudisha kwa muuzaji wako ili upatiwe kingine.

Ya muhimu kuzingatia

Katika matangazo ya biashara, wapo wauzaji ambao hutamka tu dhamana za bei hizo kwa maneno ya kuwa “ina guarantee ya miaka mitatu” lakini kama mteja, unakuwa hauna ushaidi baada ya kununua bidhaa hiyo.

Tovuti ya masuala ya kisheria, Find Law  inaeleza kuwa, pale dhamana hiyo inapokuwa inatolewa kwa mdomo pekee, kama mteja unatakiwa kuidai kwa maandishi ili iwe ushahidi pale inapotokea bidhaa imeharibika ndani ya muda uliopewa kama dhamana na mtoa huduma akakataa kukutengenezea.

Endapo muuzaji amekuhakikishia kuwa friji linagandisha barafu ndani ya nusu saa kwa hadi miaka mitatu na ukanunua likafanya kazi kwa wiki moja kisha likawa haligandishi ndani ya muda huo, fahamu kuwa ahadi yake ni dhamana na friji kushindwa kufikia kile kilichotangazwa ni mushkeri.

Unatakiwa uwe na ahadi yake kwenye maandishi na uirudishe bidhaa hiyo kwa ajili ya matengenezo (ya bure) au kubadilishiwa kabisa kulingana na makubaliano ya dhamana.

Inatakiwa iwe bayana kwenye kadi au waraka wa dhamana yako kuwa endapo kifaa kitaharibika ni nini kitafanyika aidha kubadilishiwa au kutengenezewa bila malipo.

Unaponunua bidhaa yenye dhamana, hakikisha dhamana yako inasainiwa na mtoa huduma. Picha| Deposit Photos.

Dhamana inatakiwa kuwa na nini?

Ili dhamana yako ikidhi vigezo vya kisheria kwenye madai yako, kuna vitu inatakiwa kuwa navyo. Vitu ivyo ni pamoja na ukomo wa dhamana na nini kitafanyika pale kifaa kinapoharibika na tarehe uliyonunua bidhaa pamoja na sahihi na majina ya mtoa huduma.

Tovuti ya Terms feed imeandika kuwa, dhamana inatakiwa kuanisha ukomo wa huduma zake ikiwa ni matengenezo na aina ya matengenezo yatakayofanyika. 

Mathalan, umedondosha bidhaa, dhamana yako inaweza isifanye kazi kwani kimeharibika siyo kimfumo bali kutokana na matumizi yako.

Pia, dhamana inatakiwa kuweka wazi ya nini kitafanyika kama ni matengenezo, au kubadilishwa kwa bidhaa.

Pamoja na hayo, dhamana inatakiwa kueleza hali zitakazo sababisha huduma iliyolengwa na dhamana hiyo kutokutolewa mfano endapo bidhaa imeharibika baada ya kufunguliwa na fundi mwingine, kuibiwa au kufanyiwa maboresho.

Baadhi ya watu hununua bidhaa zenye dhamana lakini kushindwa kuzingatia dhamana zao kwa kusainiwa na mtoa huduma aliyewauzia bidhaa hizo.

Fahamu kuwa, endapo umenunua bidhaa kutokana na hakikisho ulilopewa na mtoa huduma, ni muhimu kupata dhamana ili endapo mambo yataenda kombo na bidhaa yako, uweze kuokoa pesa zako. 

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW