Yafahamu majengo ya kihistoria jijini Dar es Salaam
- Lipo jengo la Old Boma, ukumbi wa Nkurumah.
- Yanatumika kama vivutio vya utalii.
Dar es Salaam. Jiji la Dar es Salaam linasifika kuwa kitovu cha shughuli za viwanda na biashara nchini Tanzania na Afrika Mashariki.
Sifa hizo ni kutoka na jiji hilo kuwa na rasimali mbalimbali ikiwemo bandari ya Dar es Salaam na reli ya kisasa (SGR).
Jiji hilo lililopo mashariki mwa Tanzania, limesheheni vivutio vya kihistoria ambazo vinalifanya kuwa la kipekee.
Kama umechoshwa na shughuli za kikazi na kiofisi na unahitaji kubadilisha mazingira, basi tembelea majengo haya ya kihistoria yaliyopo jiji hilo lilipo katika mwambao wa bahari ya Hindi.
Kwa mujibu wa Makumbusho ya Taifa (NMT), haya ndiyo majengo unayoweza kutembelea ukiwa jijini hapa:
Jengo la Old Boma
Jengo hili linapatikana barabara ya Sokoine karibu na Taasisi ya Bahari ya Dar es Salaam (DMI). Lilijengwa mwaka 1860 na Sultani Seyyid Majid ambapo alilItumia kama hoteli maalumu kwa ajili ya wageni na watumishi wake aliokuwa akifanya nao kazi.
Ukiwa katika jengo hili utafurahia historia yake kutoka kuwa hoteli binafsi mpaka kuwa ofisi za Umoja wa Mataifa (UN).
Utaweza kushuhudia aina ya ujenzi wa zamani kama mlango wa mbao uliochongwa kwa mtindo wa Kizanzibari, kuta za matumbawe na maonyesho ya kudumu juu ya mageuzi ya usanifu wa Dar es Salaam.
Jengo hili lipo umbali wa mita 900 kupitia barabara ya Samora kutoka kituo cha daladala cha Posta.

Jengo la Old Boma lilipo katikata ya Jiji la Dar es Salaam ambalo limekuwa kivutio cha utalii kwa wengi. Picha| Africantourer.com
Ukumbi wa Nkurumah
Jengo hili lipo Wilaya Ubungo jijini hapa ndani ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), limebeba historia pana ya elimu nchini Tanzania.
Jengo hili limejengwa kwa paa liliyofunukwa kwa shaba lenye umbo la mwamvuli. Ukitembelea jengo hili hautahitaji feni ukiwa ndani kwani jengo hili lina kuta pana zenye kuzuia joto na uwazi wa kuruhusu hewa safi kuingia ndani.
Kwa mujibu wa Makumbusho ya Taifa, jengo hili lilipewa hadhi kuwa urithi wa Taifa mwaka 2015. Hakuna gharama za kiingilio, ila utahitajika kufuata utaratibu zilizowekwa na chuo kama mtalii.
Jengo lipo umbali wa kilomita 2.6 kutoka kituo cha mabasi cha Ubungo kupitia barabara ya Chuo Kikuu.
Cosy Cafe
Ni mgahawa wa kale unaopatikana Mtaa wa Mkwepu, karibu na hoteli ya Golden Tulip Dar es Salaam lililobeba historia ya chama cha viongozi wa TANU (Tanganyika African National Union) hususan baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere.
Ukiwa katika mgahawa huu unaweza kufurahia vyakula vya asili, vilivyokuwepo tangu wakati wa uhuru, vinywaji pamoja na muziki wa Pwani.
Mgahawa huu upo kilomita 1 kutoka daraja la Selander kupitia barabara ya Ali Hassan Mwinyi.
Soma zaidi
-
Mfahamu Mtanzania aliyeandika kitabu cha kwanza kwa mkono Afrika
-
Vifahamu vivutio sita vya utalii vya bei rahisi Dar es Salaam
Jengo la Forodhani
Jengo hili la kihistoria lililopo maeneo ya Posta, barabara ya Kivukoni kwa sasa linatumika kama Mahakama ya Rufaa, lilijengwa na utawala wa Wajerumani mnamo 1890.
Ufikapo katika jengo hili utajifunza historia ya namna ambavyo mwanzoni lilitumika kama nyumba ya klabu ya Wajerumani katika utawala wake.
Baadaye lilichukuliwa na utawala wa Waingereza hususani maafisa waliokuwa katika ngazi za juu.
Baada ya uhuru jengo hilo lilitumika kama nyumba ya Taasisi ya Mafunzo ya Serikali ya Forodhani, mgahawa wenye hadhi na baa.
Jengo hili lipo makutano ya barabara ya Kivukoni na Ohio, umbali wa mita 700 kutoka kituo cha mabasi cha Posta.
Jengo la Forodani nalo ni kivutio kingine cha utalii Dar es Salaam ambalo lina historia ya kina. Picha| Makumbusho ya Taifa (NMT).
Magofu ya Msasani
Hapa utapata nafasi ya kushuhudia magofu ya msikiti na makaburi ya karne ya 18 hadi 19 yaliyokuwa makazi ya Waswahili wa zama za kati.
Utajifunza kuhusu historia ya jumuiya ya wafanyabiashara Waswahili waliojenga miji ya Kiafrika katika zama za kati, na kuunda sehemu ya mtandao wa biashara katika pwani ya Afrika Mashariki, Uarabuni, India na Uchina.
Magofu ya mabaki haya yapo umbali wa kilomita 6 kutoka stendi ya mabasi ya Makumbusho, ambapo pia unaweza kupata usafiri wa umma kukufikisha.
Latest