Vifahamu vivutio sita vya utalii vya bei rahisi Dar es Salaam

July 26, 2022 11:25 am · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Vivutio hivyo vinaeleza historia ya jiji hilo linalokuwa kwa kasi Afrika Mashariki.
  • Baadhi yake huihitaji kulipia ili kuviona.

Dar es Salaam. Uwapo jijini Dar kuna maeneo mengi unayoweza kutembelea na kupumzika na familia, marafiki au hata peke yako.

Kutemelea ufukweni kupata upepo, migahawani hata katika hoteli za kifahari kupata chakula ni moja ya mambo yatakayokufarahisha katika jiji hili linalokua kwa kasi barani Afrika.

Wakati ukiwaza hivyo, vipo vivutio vya utalii vinavyohusiana na historia ya Tanzania kabla na baada ya uhuru ambavyo unaweza kuvitumia kama sehemu ya kupumzisha akili.

Hili linawahusu wakazi na hata wageni wanaotembelea hili lililopo mashariki mwa Tanzania na mwambao wa bahari ya Hindi huku bandari ya Dar es Salaam na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNNIA) vikiwa ni milango na taswira ya jiji hilo.

Kwa mujibu Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Jiji la Dar es Salaam lina vivutio vingi vya utalii ikwemo makumbusho ya Taifa, kijiji cha makumbusho, mapango ya Kunduchi, visiwa vya Mbudya na Bongoyo

Vivutio vingine vya utalii ni nyumba za kale za ibada , ikiwemo Msikiti wa Mtoro na Nyamwezi, Kanisa la  St. Joseph’s na Kanisa la KKKT Azania Front.

Vivutio hivi kuna ambavyo utahitaji kutoboa mfuko
ili uweze kuvitembelea na vingine ni bure, kinachohitajika ni uwezo wako wa kuvifikia.

Makumbusho ya Taifa

Makumbusho ya Taifa, ni moja ya vivutio vya utalii  vikongwe vilivyopo jijini hapa. Ndani ya kituo hicho utaweza kujionea historia ya mwanadamu wa kale, michoro mbalimbali ya kwenye miamba, magari yaliyowahi kutumika na baadhi ya viongozi wa Tanzania pamoja na mkusanyiko wa sanaa za asili za jamii mbalimbali.

Ili kutembezwa na kujionea yaliyomo katika kivutio hicho, ulazimika kutoboa mfuko wako licha ya kuwa gharama siyo kubwa. 

Kivutio hiki  kipo katikati ya jiji la Dar es Salaam, mita 900  tu kutoka kituo cha daladala cha Posta mpya. Unaweza kutumia magari yaendayo haraka (BRT) kutokana kona mbalimbali za jiji hilo na ukaweza kufika.

Kijiji cha Makumbusho 

Hiki ni kivutio cha utalii kilichobeba historia za utamaduni wa makabila mbalimbali yalipo Tanzania, vyakula vyao, nyumba za kiutamaduni  na ngoma za asili.

Ukiwa katika Kijiji cha Makumbusho utafurahia kuona nyumba zaidi ya 30 kutoka tamaduni mbalimbali nchini Tanzania ikiwemo nyumba za tembe na msonge.

Pia utafurahia ngoma za kitamaduni kutoka jamii yoyote ile uipendayo kutoka hapa nchini.

“Timu yetu yenye uzoefu itakupa usafiri kwenda nchi nzima chini ya paa moja na ndani ya dakika chache. 

“Chukua wakati wako kutazama nyumba za kitamaduni na vitu vya zamani, bustani za kitamaduni na njia za asili, maduka ya wazi ya curio tajiri katika kazi za mikono za Tanzania,” inaeleza sehemu ya maelezo kuhusu kijiji yanayopatikana katika tovuti ya Makumbusho ya Taifa (NMT).

Ukimaliza ziara yako na kuhisi uchovu na njaa utakaribishwa katika mkahawa na uagize chakula au vinywaji vya kiasili kutoka kwa kabila lako unalopenda au utazame ngoma ya kitamaduni ya moja kwa moja kutoka kwa makabila waliyoyachagua. 

Kivutio hiki kinapatikana  eneo la Makumbusho, mita 600 kutoka kituo cha daladala cha Makumbusho. Unaweza  kutumia kufika kituo hiki kwa kutumia usafiri wa gari binafsi au usafiri wowote wa kukodi kutoka pembe zote za jiji la Dar es Salaam. 

Gharama zake zinafanana na zile utakazolipa ukitembelea Makumbusho ya Taifa Posta.

Kijiji cha Makumbusho kina zaidi ya nyumba 30 za asili ambazo ni somo kwa utamaduni wa Tanzania. Picha| 7 Toucans.

Mapango ya kunduchi

Kivutio hiki kinapatikana eneo la Kunduchi mita chache tu kufikia ukingo wa bahari Hindi. Ukiwa hapo unaweza kufurahia upepo mwanana na mandhari nzuri ya kihistoria ya eneo hili.

Kufika katika kivutio hiki unaweza kutumia usafiri wa daldala za moja moja kutoka kituo cha mabasi  makumbusho, mwenge au mawasiliano jijini hapa.

Pia unaweza kufika kwa kutumia usafiri binafsi,kivutio hiki kinapakana na kunduchi beach hoteli. 

Ukiwa kwenye mapango ya Kunduchi unaweza kufurahia kuona makaburi ya masultani wa kiarabu na historia yao.

Pia Mibuyu mikubwa iliyokuwepo tangu karne 7 zilizopita, ambayo inatumika na wakazi wa maeneo hayo kwaajili ya matambiko.


Kisiwa Mbudya na Bongoyo

Visiwa hivi ni vivutio maarufu sana jijini  hapa. Katika visiwa hivi kuna utulivu utakaoweza kupumzisha masikio yako kutokana na kelele za jijini Dar es salaam.

Pia utaweza kufurahia shughuli mbalimbali kama kuogelea, kuona samaki wa aina mbalimbali, na msitu tulivu uliotawaliwa na rangi ya kijani.

Katika visiwa hivi kuna vyakula vya baharini (seafood) kama samaki wa aina mbalimbali.

Visiwa hivi vipo umbali wa takriban kilomita tatu kutoka pembezoni mwa bahari, boti ni usafiri pekee wa kufika katika visiwa hivi.

Unachotakiwa kufanya  ni kukata tiketi ya boti kwenye kituo cha slipway Jijini Dar es Salaam, kisha kupanda boti ambapo itakuchukua dakika 30 kufika katika vivutio hivyo.


Soma zaidi: 


Nyumba za kale za ibada

Dar es Salaam ina nyumba za kale za ibada zilizokuwepo tangu enzi za ukoloni ambazo zinaweza kuwa kivutio kizuri kwa wageni na wenyeji wa jiji hili.

Jengo la Kanisa Kiinjili la Kilutheri la Azania Front, ni moja ya nyumba za ibada zenye historia ndefu yenye kuvutia tangu kujengwa kwake miaka ya 1900 na Wamisionari wa Kijerumani.

Ukiwa kanisani hapa unaweza kutembelea na kujionea teknolojia ya ujenzi wa jengo hilo na historia iliyojificha nyuma yake huku ukipulizwa na upepo mwanana wa bahari ya Hindi.

Kanisa la Mtakatifu Joseph ambalo kwa sasa linatumiwa na waumini wa Kanisa la Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam nalo ni kivutio kingine.

Kanisa hilo lipo katikati ya jiji na mwambao wa bahari ya Hindi, Mtaa wa Sokoine Drive, pembezoni mwa bahari ya hindi. Kanisa hili lilijengwa na wamisionari mwaka 1898 kwa umahiri mkubwa.

Ukitembelea kanisa hili unaweza kufahamu historia ya kanisa hilo lakini kujua mengi kuhusu dini na sababu za ujenzi wa kanisa hili, sambamba na kufurahia madhari nzuri ya kanisa hili.

Makanisa haya unaweza kutembelea bila kiingilio chochote kwa sababu ni sehemu ya kufanyia ibada.

Kanisa Kiinjili la Kilutheri la Azania Front jijini Dar es Salaam. Picha| Manispaa ya Kinondoni.

Sanamu ya askari

Sanamu ya Askari au Askari Monument ni sanamu iliyopo penye kitovu cha jiji la Dar es Salaam mahali ambapo mitaa ya Samora na Azikiwe (zamani  Maktaba) zinakutana.

Kwa mujibu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, sanamu hiyo inamwonyesha askari Mwafrika katika sare ya kijeshi ya wakati wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia (1914-1918) akishika bunduki yenye kisu cha kando na kutazama upande wa bahari.

Iliwekwa hapo 1927 na Waingereza kama kumbukumbu ya askari na wapagazi Waafrika waliopigania vita hii katika Afrika ya Mashariki hasa kati ya Uingereza na Ujerumani ambao wengi wao walifariki dunia

Katika sanamu hiyo kuna maandishi ya kumbukumbu kwa Kiingereza na Kiswahili kilichondikwa kwa herufi za Kiarabu na herufi za Kilatini pia. Maneno yake kwa Kiswahili ni kama yafuatayo:

“Huu ni ukumbusho wa askari Waafrika wenyeji waliopigana katika vita kuu na ni ukumbusho pia kwa wapagazi ambao walikuwa miguu na mikono ya majeshi. Ni ukumbusho pia kwa watu wote waliotumika wakafa kwa ajili ya mfalme na nchi yao katika Afrika ya Mashariki kwenye vita kuu toka mwaka 1914 mpaka 1918 . Ukipigania nchi yako ujapo umekufa watoto wako watalikumbuka jina lako.”

Kabla ya kuwekwa sanamu hiyo iliwahi kuwekwa sanamu ya Meja Hermann Von Wissmann aliyekuwa gavana wa kwanza wa Afrika ya Mashariki ya Kijerumani na sanamu hii ilibomolewa na Waingereza walipoteka mji mwaka 1916

Kuiona sanamu hii ni bure kwa sababu kwenye makutano ya barabara ambapo kila anayepita awaweza kuiona.

Sanamu ya askari iliyopo jijini Dar es Salaam. Picha| Nukta.

 

Enable Notifications OK No thanks