Rais Samia amlilia DC Mahawe
- Rais Samia asema atakumbukwa kwa uchapakazi hodari, ukweli na msimamo thabiti katika utendaji.
Arusha. Rais Samia Suluhu Hassan amesema amepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Mkuu wa Wilaya ya Mbozi Esther Mahawe, kilichotokea leo Januari 14, 2025 katika hospitali ya KCMC, mkoani Kilimanjaro.
Kupitia taarifa yake iliyochapishwa kwenye mitandao ya kijami Rais Samia ametoa pole kwa Mkuu wa Mkoa wa Songwe Daniel Chongolo, ndugu, jamaaa na marafiki walioguswa na msiba huo pamoja na kumshukuru Mungu kwa utendaji wa kiongozi huyo.
“Nawapa pole familia ya marehemu, Mkuu wa Mkoa wa Songwe, ndugu, jamaa na wote walioguswa na msiba huu. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa maisha ya Bi. Esther na utumishi wake kwa umma ambao uliongozwa na uchapakazi hodari, ukweli na msimamo thabiti katika utendaji,” amesema Rais Samia kupitia ukurasa wake wa Instagram.
Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu imebainisha kuwa Marehemu Mahawe amefariki leo tarehe 14 Januari, 2025 katika hospitali ya KCMC mkoani Kilimanjaro ambako alikuwa akipatiwa matibabu.
Enzi za uhai wake Ester alitumikia nafasi mbalimbali katika Serikali ikiwemo ubunge wa Viti Maalum kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kuanzia mwaka 2015 hadi 2020.
Mwaka 2021 aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kigoma na baadae kuhamishiwa Wilaya ya Mbozi iliyopo Mkoa wa Songwe mwaka 2023 nafasi aliyoitumikia hadi alipofikwa na umauti.