WHO: Viatu havisambazi virusi vya Corona

June 13, 2020 7:18 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Uwezekano wa viatu kukusababisha maambukizi ya Covid-19 kwa mujibu wa WHO ni mdogo.
  • Shirika hilo limeshauri viatu viwekwe mbali na watoto wanaotambaa. 

Dar es Salaam. Kutokana na mizunguko ya hapa na pale ili kukamilisha majukumu ya kila siku, huenda unapokuwa unarudi nyumbani unajiuliza kama haujabeba virusi vya Corona (Covid-19) kwenye mavazi na viatu vyako kwani vimekanyaga sehemu nyingi.

Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema uwezekano wa mtu kuambukizwa virusi vya corona kupitia viatu vyake ni mdogo sana.

Hata hivyo, WHO imesema kwenye nyumba ambazo zina watoto wadogo wanaotambaa wanaweza kugusa viatu hasa vikiwa ndani na kujiweka katika hatari ya kupata maambukizi ya Covid-19. 

Imeshauri viatu viwekwe mbali na watoto baada ya wanafamilia kurudi nyumbani ili kuendelea kujikinga na ugonjwa huo. 

“Kama tahadhari, hasa majumbani ambapo watoto wanatambaa na kucheza kwenye sakafu, unashauriwa kuviacha viatu vyako nje,” imesema WHO

Zaidi, kwa kufanya hivyo itasaidia kuepusha uchafu na taka ambazo unaweza ukawa umezikusanya kwenye soli ya kiatu chako kuchangamana na watu.

Enable Notifications OK No thanks