Wawili wapona Corana Zanzibar, wagonjwa wakifikia 12

April 13, 2020 12:22 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Wagonjwa wote watatu wapya ni vijana, Watanzania na hawana historia ya kusafiri nje ya nchi siku za hivi karibuni.
  • Mpaka sasa Zanzibar imefikisha idadi ya wagonjwa 12 kati ya 49 waliopo Tanzania

Dar es Salaam.Waziri wa Afya wa Zanzibar, Hamad Rashid Mohamed ametangaza kupona kwa wagonjwa wawili na ongezeko la wagonjwa wapya watatu wa virusi vya Corona (COVID19) na kufanya visiwa hivyo kuwa na wagonjwa 12 mpaka sasa.

Mohamed katika taarifa yake iliyotolewa leo (Aprili 13, 2020) amesema wagonjwa hao wawili waliopona walikuwa wakipatiwa matibabu katika kituo maalum cha Kidimni.

Amesema wameruhusiwa kurudi nyumbani na watatakiwa kubaki ndani na kutochangamana na watu kwa siku 14.

Aidha, amesema kati ya sampuli walizopeleka jana maabara tatu zimekutwa na maambukizi ya virusi vya Corona.

“Hii inafanya idadi ya wagonjwa wetu jumla kuwa 12 baada ya ongezeko la wagonjwa watatu wapya,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Ongezeko la wagonjwa hao watatu wa Zanzibar linafanya Tanzania sasa kuwa wagonjwa na 49 wa Corona ambapo watatu wamefariki dunia huku saba  wakipona.


Zinazohusiana:


Mapema leo asubuhi, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alitangaza ongezeko la wagonjwa 14 wapya wa COVID-19.

Mohamed amesema wagonjwa wote watatu ni Watanzania na hawana historia ya kusafiri nje ya nchi siku za hivi karibuni.

“Hii inathibitisha kuwa maradhi haya yamo kwenye jamii yetu (Community transmission) na hivyo kuongeza hatari ya kuambukizana wenyewe kwa wenyewe endapo tahadhari za ziada hazitachukuliwa,” amesema Waziri huyo.

Mgonjwa wa kwanza ni mwanaume, Mtanzania (30) mkazi wa Mwanakwerekwe aliripotiwa Aprili 10 na alikuwa karibu sana mmoja wa wagonjwa waliolazwa katika kituo cha Kidimni.

Mgonjwa pili ni mwanamke, Mtanzania (22) mkazi wa Jang’ombe Zanzibar aliyeripotiwa Aprili 8 kuwa ana homa kali na kikohozi na baada ya kipimo aligundulika ana maambukizi na anaendelea kupatiwa matibabu.

Mgonjwa wa tatu ni mwanamke, Mtanzania (19) mkazi wa Bumbwisudi Zanzibar aliyeripotiwa Aprili 10 kuwa ana homa kali na kikohozi na baada ya kipimo aligundulika naye ana maambukizi.

Mohammed amesema Serikali inaendelea kuwafuatilia watu wa karibu waliowahi kukutana na wagonjwa hao ili kudhibiti kuenea kwa maambukizi mapya.

Amebainisha kuwa hadi kufikia jana (Aprili 12, 2020) watu 164 waliokutana na watu walioambukizwa Corona wanafuatiliwa huku wengine 232 waliorudi nchini kutoka nje ya Tanzania wamewekwa karantini Pemba na Unguja.

“Wengine 264 wameruhusiwa kutoka karantini baada ya kukaa siku 14 na kutoonyesha dalili za maradhi hayo,” amesema waziri huyo.

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imewaomba wananchi kuendelea kuchukua tahadhari kwa kunawa mikono mara kwa mara, kuepuka kugusa pua, mdomo au macho, kutumia tishu wakati wa kukohoa au kupiga chafya.

Pia wanakumbushwa kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima hasa katika masoko na vituo vya daladala.

Enable Notifications OK No thanks