Watumiaji wa ving’amuzi wapungua kwa asilimia 3.2 Tanzania
- Watumiaji hai wa ving’amuzi kwa mwaka jana walikuwa milioni 2.68 ambapo wameshuka kutoka watumiaji milioni 2.76 milioni waliokuwapo mwaka juzi.
- watumiaji wa ving’amuzi vinavyotumia madishi wameongezeka hadi kufikia milioni 1.1 mwaka 2019 kutoka 985,594 iliyorekodiwa mwaka juzi.
- Wachambuzi wasema hali hiyo inasababishwa na mabadiliko ya teknolojia na hali ya hewa.
Dar es Salaam. Idadi ya watumiaji wa ving’amuzi kwa ajili ya kutazama luninga imeshuka kwa asilimia 3.2 ndani ya kipindi cha mwaka mmoja uliopita, huku wachambuzi wa mawasiliano wakieleza kuwa watu wanatumia teknolojia nyingine ikiwemo simu kupata habari.
Takwimu za Robo ya Mwisho ya Mwaka 2019 (Oktoba – Disemba) zilizotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) hivi karibuni zinaeleza kuwa watumiaji hai wa ving’amuzi kwa mwaka jana walikuwa milioni 2.68 ambapo wameshuka kutoka watumiaji milioni 2.76 milioni waliokuwapo mwaka juzi.
Hiyo ina maanisha kuwa ving’amuzi 84,328 havitumiki tena na watu kutazama luninga nyumbani au sehemu za kazi.
Tangu mwaka 2014, idadi ya watumiaji wa ving’amuzi imekuwa ukiongezeka kila mwaka hadi kufikia mwaka 2018 kabla haijapungua hadi milioni 2.68 mwaka uliofuata.
Matumizi ya ving’amuzi hutumika na vyanzo mbalimbali ikiwemo antena, madishi (satellite) na waya (cable) ambazo huunganishwa nyumbani.
Licha ya kuwa watumiaji wa ving’amuzi wakipingua kwa mwaka mmoja uliopita, ving’amuzi vinavyotumia madishi vimeongezeka.
Takwimu hizo za TCRA zinaonyesha kuwa watumiaji wa ving’amuzi vinavyotumia madishi wameongezeka hadi kufikia milioni 1.1 mwaka 2019 kutoka 985,594 iliyorekodiwa mwaka juzi.
Hata hivyo, wakati watumiaji wa ving’amuzi vya waya wakibaki 158,224 kwa miaka minne mfululizo kutokea mwaka 2016, watumiaji wa ving’amuzi vinavyoendeshwa na antena wamepungua kutoka watumiaji milioni 1.62 mwaka 2018 hadi milioni 1.43 mwaka jana.
Wachambuzi wa masuala ya teknolojia na mawasiliano wameiambia Nukta (www.nukta.co.tz) kuwa kupungua kwa matumizi ya ving’amuzi ni mchanganyiko wa sababu mbalimbali ikiwemo ukuaji wa teknolojia ya simu zinazotumia intaneti, jambo linalowafanya wapate taarifa kwa haraka katika viganja vya mikono yao.
Zinazohusiana
Akizungumzia kuongezeka kwa ving’amuzi vya madishi, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Tumaini kampasi ya Dar es Salaam (TUDARCo), Richard Ngaiza amesema teknolojia ya madishi ya “satellite” ni imara zaidi ikilinganishwa na ya antena kwani madishi yanaweza kuhimili mabadiliko ya hali ya hewa ikiwemo upepo na mvua zaidi ya antena.
Ngaiza ambaye amebobea katika fani ya teknolojia ya mawasiliano na habari, amesema madishi humfanya mtu kupata chaneli anazozitaka kwa sababu dishi likifungwa vizuri linatulia.
Miongoni mwa makampuni yanayotoa huduma ya ving’amuzi vya dishi ni pamoja na DSTV, Zuku, Azam na Startimes.
Naye Mhitimu wa masomo ya uhandisi wa Mawasiliano pepe, Alfred Kitulla amesema antena hukumbana na changamoto nyingi kwenye utendaji kazi wake zikiwemo changamoo asilia na zile za binadamu kama majengo, na milima.
“Kama kuna mlima au jengo refu kati ya antena yako na mnara wa matangazo, lazima utapata changamoto kwenye kufurahia televisheni yako.
“Dishi hupata matangazo moja kwa moja kutoka kwenye satelaiti hivyo majengo na milima kushindwa kuwa changamoto kwake,” amesema Kitulla.
Latest