Watumiaji wa huduma za simu benki wazidi kupaa Tanzania, wafikia milioni 23

January 28, 2019 5:40 pm · Nuzulack Dausen
Share
Tweet
Copy Link
  • Ndani ya mwaka mmoja watumiaji wa huduma za kifedha kupitia simu wameongezeka kwa takriban milioni 1.5.
  • Tanzania sasa ina watumiaji wa huduma hizo za kibenki zaidi ya milioni 23 kutoka milioni 21.88 Desemba 2017.
  • Vodacom yazidi kuongoza sokoni kwa kuweka kibindoni wateja zaidi ya milioni tisa sawa na asilimia 39 ya soko zima.
  • TTCL imekuza watumiaji wake wa huduma za T-Pesa zaidi ya mara 10 ndani ya mwaka mmoja.

Dar es Salaam. Idadi ya watumiaji wa huduma za kifedha kupitia simu za mkononi inazidi kupaa kwa kasi nchini baada ya takwimu mpya za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kubainisha ongezeko la watumiaji milioni 1.47 ndani ya mwaka mmoja.

Ongezeko hilo la asilimia 6.8 sasa linafanya watumiaji wa huduma za kifedha kupitia simu za mkononi Tanzania kufikia milioni 23.36 hadi Desemba 2018 kutoka milioni 21.88 iliyorekodiwa mwaka 2017.

Wataalam wa masuala ya uchumi na fedha wanaeleza kuwa takwimu hizo zinaonyesha mwenendo mzuri kuwa sasa Watanzania wengi wanazidi kufikiwa na huduma za kifedha hadi maeneo ya vijijini na kuchangia kwa kiwango kikubwa mapato ya Serikali.

Katika takwimu mpya za mawasiliano za robo ya mwisho ya mwaka 2018 (Telecom statistics December 2018) zilizochapishwa na TCRA mwishoni mwa juma lililopita, zinabainisha kuwa takriban asilimia 92 ya watumiaji wote wa huduma za kifedha kwa njia za simu wanatumia M-Pesa, Tigo Pesa na Airtel.

Kampuni zilizosalia zinagawana asilimia nane ya watumiaji hao wa huduma za kifedha.

Katika mchuano huo, M-pesa ndiyo inayotawala soko nchini baada ya kuweka kibindoni watumiaji zaidi ya milioni tisa sawa na asilimia 39 ya soko zima ikifuatiwa kwa karibu na Tigo Pesa (32) na Airtel Money ikiwa na asilimia 21.

Vodacom kupitia M-Pesa imezidi kuongeza wateja wake ndani ya mwaka mmoja licha ya ushindani mkali baada ya takwimu hizo mpya kuonyesha kuwa ilivuna watumiaji zaidi ya 928,000 ndani ya mwaka kutoka watumiaji milioni 8.08 Desemba 2017.

Made with Flourish

Kampuni ya simu ya umma, TTCL ambayo ilianza kutoa huduma za kifedha mapema mwaka 2017 imeanza kuchomoza baada ya kuongeza watumiaji wa T-Pesa zaidi ya mara 10 hadi watumiaji 30,394 Desemba mwaka 2018 kutoka 3,135 waliorekodiwa Desemba 2017. 

T-Pesa hadi Desemba mwaka jana ilikuwa inamiliki asilimia 0.13 ya soko kutoka asilimia 0.01 Desemba 2017.

Profesa wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Michael Ndanshau ameiambia www.nukta.co.tz kuwa matumizi ya simu za mkononi katika kutoa huduma za kifedha kunaongeza wigo wa huduma za fedha kwa kila mwananchi (financial deepening) ambao huchochea katika maendeleo.

“Kuongezeka kwa watumiaji wa huduma za kifedha kupitia simu ya mkononi ni fursa kwa Serikali kukusanya kodi. Kwa wenzetu wa Ethiopia kampuni nyingi zipo chini ya Serikali wanapata fedha sana lakini hata huku kwetu bila kupepesa macho, mwenendo huu ni mzuri na neema kwetu,” amesema Prof Ndanshau ambaye tafiti zake nyingi zimejikita katika masuala ya uchumi ikiwemo huduma za kifedha


Zinazohusiana: 


Amesema kwa sasa hadi wakazi wa vijijini ambao hawana matawi ya benki wanaweza kutuma fedha kupitia simu ya mkononi na kwamba jambo hilo linasaidia kupunguza makali ya maisha.

“Wakazi wa vijijini wenye watoto au ndugu na jamaa waliopo mjini wanatumiwa pesa kwa ajili ya matumizi, uwekezaji…kwa sasa huduma za kifedha zinakuwa rahisi sana kutuma fedha na kuchochea maendeleo,” amesema.

Kuhusu kupaa kwa gharama za tozo katika matumizi ya huduma za kifedha mtandaoni, mtaalamu huyo wa uchumi amesema Serikali inapaswa kuwalinda walaji hususan kampuni za simu kutoza fedha nyingi kwa walaji.

“Lengo la Serikali ni kuhakikisha wananchi wapate ‘financial services’ (huduma za kifedha) hivyo kodi haitakiwi kuwa kikwazo cha watu kupata huduma hizo za kifedha. Tunaomba Serikali isimamie suala hili la utozaji kwamba kodi inazotoza zisiwe kubwa mno na makampuni ya simu nayo yasitoze toza kubwa kwa walaji,” amesema.

Takwimu hizo zinakuja ikiwa ni takriban majuma mawili tangu Rais John Magufuli ashuhudie makabidhiano ya mtambo wa kudhibiti mawasiliano nchini (Telecommunication Traffic Monitoring System) uatakosaidia kuhakiki takwimu za mawasiliano na kuzuia kuvuja kwa mapato katika sekta hiyo inayokua kwa kasi nchini.

Enable Notifications OK No thanks