Watumiaji wa huduma za kifedha kwa njia ya simu wapaa

February 17, 2020 1:01 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Watumiaji wa huduma za kifedha kupitia simu za mkononi Tanzania kufikia milioni 25.86 hadi Desemba 2019 kutoka milioni 23.36 iliyorekodiwa mwaka 2018.
  • Asilimia 89 ya watumiaji wote wa huduma za kifedha kwa njia za simu wanatumia M-Pesa, Tigo Pesa na Airtel Money.

Dar es Salaam. Idadi ya watumiaji wa huduma za kifedha kupitia simu za mkononi inazidi kupaa nchini Tanzania baada ya takwimu mpya za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kubainisha ongezeko la watumiaji milioni 2.5 ndani ya mwaka mmoja.

Ongezeko hilo la asilimia 10.7 sasa linafanya watumiaji wa huduma za kifedha kupitia simu za mkononi Tanzania kufikia milioni 25.86 hadi Desemba 2019 kutoka milioni 23.36 iliyorekodiwa mwaka 2018.

Takwimu hizo zinaonyesha mwenendo mzuri kuwa sasa Watanzania wengi wanazidi kufikiwa na huduma za kifedha hadi maeneo ya vijijini na kuchangia kwa kiwango kikubwa mapato ya Serikali.

Katika takwimu mpya za mawasiliano za robo ya mwisho ya mwaka 2019 (Telecom statistics December 2019) zilizochapishwa na TCRA hivi karibuni, zinabainisha kuwa asilimia 89 ya watumiaji wote wa huduma za kifedha kwa njia za simu wanatumia M-Pesa, Tigo Pesa na Airtel Money.

Kampuni zilizosalia zinagawana asilimia 11 ya watumiaji hao wa huduma za kifedha.

Katika mchuano huo, M-pesa ndiyo inayotawala soko nchini baada ya kuweka kibindoni watumiaji zaidi ya milioni 10 sawa na asilimia 39 ya soko zima ikifuatiwa kwa karibu na Tigo Pesa (30) na Airtel Money ikiwa na asilimia 20.

Hata hivyo, kutokana na mchuano mkali, watumiaji wa Tigo Pesa na Airtel Money wamepungua kwa viwango tofauti ikilinganishwa na mwaka juzi. Mwaka 2018, waliokuwa wanatumia Tigo Pesa walikuwa asilimia 32 na wale wa Airtel Money walikuwa 21.

Enable Notifications OK No thanks