Watuhumiwa 283 wakamatwa kwa wizi, ubakaji, ulawiti Arusha
- Ni pamoja na watuhumiwa wa makosa ya wizi, ubakaji, ulawiti na kujihusisha na madawa ya kulevya.
- Lawatahka wanaojihusisha na vitendo vya kihalifu kuacha mara moja.
Arusha. Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha limewakamata watuhumiwa 283 kwa uhalifu wa makosa mbalimbali ikiwemo ubakaji, kujihusisha na madawa ya kulevya pamoja na unyanyasaji wa kijinsia kwa kipindi cha miezi miwili iliyopita.
Taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Justine Masejo iliyotolewa leo Februari 17, 2025 inabainisha kuwa watuhumiwa hao walikamatwa baada ya kufanyika kwa operesheni maalum maalum dhidi ya uhalifu ndani ya mkoa huo kuanzia Januari hadi sasa.
“Tulifanya operesheni dhidi ya uhalifu na wahalifu na kufanikiwa kukamata watuhumiwa mbalimbali na kuwafikishwa Mahakamani. Kwa upande wa makosa ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia, tulifanikiwa kuwakamata watuhumiwa 15 na kuwafikisha mahakamani” inaeleza taarifa ya Masejo.
Taarifa hiyo inafafanua kuwa watuhumiwa 10 kati ya waliokamatwa kwa tuhuma za unyanyasaji wa kijinsia walifanya kosa la ubakaji na watano wanatuhumiwa kufanya ulawiti.
Baada ya kufikishwa mahakamani watuhumiwa watatu wa ubakaji walihukumiwa kfungo vya maisha, mtuhumiwa mmoja kifungo cha miaka 30 huku mwingine mmoja wa kosa la ulawiti akihukumiwa kifungo cha maisha mwingine kifungo cha miaka 30 ambapo watuhumiwa wengine kesi zao zipo katika hatua mbalimbali.
Katika hatua nyingine jeshi hilo pia lilifanya msako dhidi ya dawa za kulevya na kufanikiwa kukamata watuhumiwa 26 wakiwa na mirungi Kilogramu 196.4, watuhumiwa 22 wakiwa na bangi kilogramu 32 pamoja na kuteketeza zaidi ya hekari 10 za bangi.
“Watuhumiwa wote wa Dawa za kulevya tayari wamefikishwa Mahakamani na kesi zao zipo katika hatua mbalimbali,” imesema taarifa ya Masejo.
Kwa upande wa mapambano dhidi ya ujangili, jeshi hilo limekamata watuhumiwa 202 wa makosa ya wizi pamoja na wengine wawili wakiwa na nyama ya nungunungu kilogramu 20 ambapo tayari wamefikishwa mahakamani na kesi zao zipo katika hatua mbalimbali.
Mbali na hao, watuhumiwa wengine 38 wamekamatwa wakiwa na pombe ya moshi lita 172 na mitambo minne ya kutengenezea pombe hiyo ambapo watuhumiwa wote tayari wameshafikishwa mahakamani kwa taratibu za kisheria.
Sambamba na taarifa hiyo, Jeshi hilo limewataka wanaojihusisha na vitendo vya kihalifu kuacha mara moja kwa kuwa watakamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria dhidi yao.
Latest



