Watoto wawekewa kibano michezo ya mtandaoni China
- Wanaruhusiwa kucheza michezo hiyo saa tatu kwa wiki.
- China yaema itaka kulinda afya na elimu ya watoto.
- Hatua hiyo inaweza kupunguza mapato ya kampuni zinazotoa huduma hiyo.
Dar es Salaam. Serikali ya China imetangaza kuzuia watoto wadogo kucheza michezo ya video ya mtandaoni katikati ya wiki, hatua inayotajwa kuwa itaathiri utendaji wa kampuni za teknolojia nchini humo.
Kwa mujibu wa kanuni mpya zilizotolewa na Shirika la Taifa la Habari na Usimamizi wa Uchapishaji (NPPA) Agosti 30, 2021, watoto walio chini ya umri wa miaka 18 hawataruhusiwa kucheza michezo ya video kuanzia Jumatatu hadi Alhamisi.
Wataruhusiwa kucheza michezo hiyo siku za Ijumaa, Jumamosi na Jumapili kuanzia saa 8 mchana hadi saa 9 jioni ambayo ni sawa na saa tatu kwa wiki.
Sera hiyo itahusu michezo ya mtandaoni pekee na watumiaji wanatakiwa kujisajili kwa kutumia majina yao halisi pamoja na kitambulisho cha Serikali.
NPPA imeeleza kuwa hatua hizo zimechukuliwa ili kuzuia urahibu wa michezo hiyo kwa watoto na kuhakikisha wanakuwa na afya bora ili kufikia ndoto zao kielimu.
Hiyo siyo mara ya kwanza kwa China kuweka udhibiti wa watoto kucheza michezo hiyo. Mwanza 2019, ilipiga marufuku watoto kucheza michezo hiyo baada ya saa 10 jioni na hawakutakiwa kuzidisha dakika 90 kwa siku.
Hata hivyo, mwezi uliopita vyombo vya habari vinavyoendeshwa na Serikali vilitaja michezo hiyo kama “kasumba ya kiroho” na kusababisha kushuka kwa bei za hisa za Tencent, kampuni kubwa ya michezo ya kubahatisha nchini humo.
Aidha, kwa kanuni hizo mpya za michezo ya video ya mtandaoni huenda zikaathiri kampuni hiyo ambayo ni kampuni kubwa zaidi ya michezo ya kubahatisha ulimwenguni kwa mapato.
Pia kampuni hiyo inamiliki programu tumishi ya WeChat na ina nafasi kubwa ya ushindani katika soko la michezo ya kubahatisha la Amerika.
Latest



