Watanzania watatu watajwa orodha ya vijana 100 wenye ushawishi Afrika

October 2, 2019 1:59 pm · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Vijana hao ni Kennedy Mmari, Dk Felix Manyogote na Petrider Paul
  • Mwanaharakati wa usawa wa kijinsia, Petrider Paul ndiye mwanamke pekee kutoka Tanzania aliyepenya katika tuzo hizo. 
  • Kati ya vijana 100 wenye ushawishi, 52 ni wanawake. 

Dar es Salaam. Tamaduni ya kusheherekea mafanikio ya vijana imekuwa ni chachu ya kuibua vipaji, mawazo na taasisi au kampuni ambazo zinaboresha maisha ya jamii. 

Tuzo za vijana maarufa kama “Africa Youth Awards” imetoa majina ya vijan 100 wa Afrika wenye ushawishi zaidi katika bara hilo katika sekta mbalimbali za maendeleo. 

Tuzo hizo ambazo hutolewa kila mwaka kwa vijana ambao wanagusa maisha ya watu kwa elimu, shughuli na vipaji na kufanya Afrika kuwa sehemu bora kwa kila mtu kuishi. 

Kati ya vijana hao 100, wapo waandishi wa habari, wanamuziki, wanaharakati, viongozi, wanamitindo na wamiliki wa kampuni mbalimbali.

Katika orodha iliyotoka mwaka huu, vijana 15 wametoka Nigeria, Afrika Kusini (11), Kenya (9) na Ghana (8), na Tanzania haijabaki nyuma kwani vijana watatu wametajwa kwenye orodha hiyo.

Watanzania hao waliotajwa katika tuzo hizo zilizoanza kutolewa mwaka 2014 ni Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Serengeti Bytes; Dk Felix Manyogote kutoka taasisi ya MaMa Afya Initiative  na Mwanaharaki wa masuala ya jinsia. 

Kennedy Mmari

Mmari ni Mtaalam wa masuala ya mahusiano ya umma na mitandao ya kijamii ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Serengeti Bytes ambayo inajishughulisha zaidi na mawasiliano na mahusiano na kutoa ushauri wa mawasiliano ya umma.

Septemba 2019, tovuti ya Marekani inayofanya tafiti na kuhuisha viwango ya “Clutch” iliitaja Serengeti Bytes kuwa kati ya kampuni 20 bora zinazofanya vizuri Afrika.

Mmari ameweza kupenya katika tuzo hizo kutoka na una umahiri wake katika shughuli za mawasiliano na mitandao ya kijamii ambazo zimekuwa zikigusa maisha ya Watanzania hasa vijana.

Amewahi kufanya kazi na shirika la Raleigh International  ambalo linahamasisha vijana kwa ajili ya mabadiliko chanya kwa maendeleo endelevu.

Akiwa Raleigh, Mmari alisimamia kazi za mawasiliano ikiwa ni pamoja na kuandaa makala mbalimbali na kusimamia mitandao ya kijamii. Baadhi ya makala zake zimeonekana kwenye gazeti la The Guardian (UK) pamoja na magazeti ya hapa nchini.

Mmari amekuwa akijishughulisha na masuala ya kuboresha elimu ya wanafunzi wa Tanzania. Picha|Mtandao. 

Dk Felix Manyogote

Huyu ni kijana mwenye kasi ya tofauti. Yeye anajihusisha na kutoa elimu kwa wanaume kujihusisha katika masuala ya afya ya uzazi, mama na mtoto. 

Manyogote ni mzaliwa wa Tanzania aliyebobea katika shughuli za udaktari wa binadamu. 

Akiwa kama Meneja Mipango katika taasisi ya Mama Afya Initiative, anawajibika katika kuandaa programu kwa ajili ya kutoa elimu ya bure kwa wakina mama wajawazito na kuandaa mafunzo kwenye shule za vijijini.

Kupitia kazi yake, alinyakua tuzo mwaka 2017 kwenye kitengo cha “Leave No One Behind” (usimuache mtu nyuma) iliyotolewa na Umoja wa Mataifa (UN). Amekuwa akitumia vizuri vipaji vyake kuwaongoza na kuleta mabadiliko katika sekta ya afya hasa kwa watu wasiofikiwa na huduma bora. 


Zinazohusiana:


Petrider Paul

Huyu ni Mwanaharakati wa masuala ya jinsia. Kama msichana pekee kutoka Tanzania aliyeingia katika orodha hiyo, Paul amefanikiwa kuwafikia watu zaidi ya 200 na kuwawejengea uwezo kuwa wadau muhimu wa kupigani usawa wa kijinsia nchini.

Yeye ni kiongozi wa mpango wa kupambana dhidi ya unyanyapaa wa kijinsia (Voice Out Against Gender-Based Violence Initiative) nchini. Kiu yake kubwa ni kuona vijana wanahusika kwenye kufanya maamuzi yanayoathiri jamii zao.

Kupitia mpango huo anadhamiria kuwawezesha wahanga wa ukatili wa kijinsia kusikika na hatua dhidi ya wahusika kuchukuliwa. 

Paul alichaguliwa na Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AU), Moussa Faki Mahamat kuwa mshauri wa vijana na kutajwa kuwa miongoni mwa wanawake 100 katika orodha ya “Tanzania Sheroes”. 

Pamoja na hayo amewahi chukua tuzo kutoka kwa Malkia Elizabeth wa Uingereza  ikiwa ni baada ya kazi yake ya kupambana dhidi ya ukatilili wa kijinsia kuonekana duniani.

Petreder anadhamiria kuwawezesha wahanga wa ukatili wa kijinsia kusikika na hatua dhidi ya wahusika kuchukuliwa. Picha|Mtandao. 

Mwasisi wa Africa Youth Awards, Prince Akpah amesema orodha ya mwaka huu (2019) imevunja rekodi kwani kati ya vijana 100, wasichana wapo 52 na wanaume 48. Hiyo ni sawa nakusema wanawake wameamka na wanafanya mambo makubwa katika bara la Afrika. 

“Hiyo ni ishara nzuri ya kumuhusisha mtoto wa kike katika shughuli za maendeleo,” amesema Akpah katika taarifa ya kutangazwa vijana hao. .

Orodha hiyo imehusisha watu wengine mashughuri akiwemo Mke wa Rais wa Sierra Leone, Fatima Maada, Mwanaharakati wa Sudan, Alaa Salah na wasanii kama Davido na Mr Eazi.

Enable Notifications OK No thanks