Watanzania milioni 2.1 wafikiwa na kampeni ya Samia Legal Aid
- Idadi hiyo ni sawa na asilimia 3.5 ya Watanzania wote.
- Serikali yaweka mikakati ya kuifanya kuwa endelevu.
Arusha. Waziri wa Katiba na Sheria Damas Ndumbaro amesema kampeni ya Msaada wa Kisheria ya mama Samia (Samia Legal Aid Campaign) imewafikia Watanzania milioni 2.1 jambo linaloendelea kuongeza uelewa wa sheria na utatuzi wa migogoro nchini.
Kampeni ya hiyo iliyozinduliwa Aprili 27, 2023 imeifikia mikoa 23 nchini ikiwemo Jiji la Arusha ambapo inatarajiwa kuwahudumia wakazi wa jiji hilo kwa siku 10.
Miongoni mwa mikoa ambayo imefikiwa na kampeni hiyo mpaka sasa ni Dodoma Manyara, Shinyanga, Ruvuma, Simiyu, Singida, Njombe Iringa, Mara, Songe, Morogoro, Kigoma, Katavi, Tabora Geita Mtwara, Kilimanjaro Mwanza, Pwani, Rukwa Lindi, Mbeya na Arusha.
Waziri Ndumbaro aliyekuwa akizungumza katika uzinduzi wa kampeni hiyo Jijini Arusha leo Machi 28, 2025 amesema kuwa zaidi ya nusu ya waliohudumiwa katika kampeni hiyo ni wanaume.
“Watanzania 2,192,372 kati ya hao wanaume ni 1,880,457 na wanawake 1,103,915, hawa ni wale ambao wamefikiwa mmoja mmoja kukaa nao kusikiliza na kuondoka changamoto zao,”amesema Waziri Ndumbaro.
Kwa takwimu hizo, ni sawa na kusema kuwa kampeni hiyo imefikia asilimia 3.5 ya Watanzania ndani ya miaka miwili kati ya Watanzania 61.7 waliopo nchini kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022.

Baadhi ya mabanda ya msaada wa kisheria tayari kwa ajili ya kuwahudumia wakazi wa Arusha Picha/Wizara ya Katiba na Sheria/X.
Hata hivyo, Ndumbaro amesema wamefikia Watanzania milioni 43 kupitia vyombo vya habari ambao wameweza kuwapatia elimu ya sheria na namna sahihi ya kutatua migogoro.
Kutokana na umuhimu wa kampeni hiyo Ndumbaro amesema kuwa wameandaa utaratibu wa kufanya iwe endelevu ikiwemo kufungua madawati ya sheria katika halmashauri, kuwatumia wasaidizi wa kisheria (paralegals) waliopo katika kila mkoa pamoja na kushirikiana na vyuo vikuu.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Makonda aliyekuwa mgeni rasmi katika uzinduzi huo amewataka watumishi wa kampeni hiyo kuwasaidia wananchi na kufanyia kazi changamoto zao.
“Tuwape muda tuwasililize vizuri tuwatendee haki wananchi hawa..migogoro hii haipaswi kuwa ya kwenye makaratasi tuzitatue shida za Wananchi tuwape majibu,” amesema Makonda.
Kampeni hiyo inafanyika kuanzia leo Machi 28 hadi April 7 mwaka huu ikiweka kambi katika halmashauri, wilaya, kata na vijiji vyote jijini humo.
Latest



