Balozi Juma Mwapachu afariki dunia, wanasiasa wamlilia

March 29, 2025 1:28 pm · Esau Ng'umbi
Share
Tweet
Copy Link
  • Anatarajiwa kuzikwa Machi 29,2025 jijini Tanga.

Arusha. Mwanasiasa mashuhuri nchini Tanzania Balozi Juma Mwapachu, amefariki dunia Machi 28, 2025 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu.

Taarifa za kifo cha Mwanasiasa huyo aliyeshika nyadhifa mbalimbali za kitaifa na kimataifa zilianza kuripotiwa jana Machi 28 mwaka huu akitarajiwa kusafishwa kwenda Kijiji cha Pande, Kiomoni, Tanga kwa ajili ya mazishi yatakayofanyika Jumapili Machi 30, 2025.

Mwapachu ambaye alikuwa mwanachama wa Chama cha Mapinduzi  (CCM)  amewahi kushika nyadhifa mbalimbali katika sekta za benki, maendeleo vijijini, diplomasia, na sekta binafsi kabla ya kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Nyadhifa nyingine alizowahi kushika Mwapachu ambaye pia ni  mwanasheria kitaaluma ni pamoja na kuhudumu katika Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kati ya mwaka 2002 na 2006 na baadae kuteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa. 

Mwapachu pia amewahi kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) pamoja na kuwa Mwenyekiti wa Bodi za Mashirika ya Umma ikiwa ni pamoja na Benki ya Uwekezaji Tanzania, pia alihudumu kama Kamishna wa Tume ya Rais ya Marekebisho ya Sekta ya Mashirika ya Umma.

Katika sekta ya biashara na viwanda, Balozi Mwapachu alikuwa Mwenyekiti wa Shirikisho la Viwanda Tanzania na Baraza la Biashara la Afrika Mashariki, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Biashara ya Nje na Baraza la Usimamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, mjumbe wa Baraza la Usimamizi wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kimataifa na kushiriki katika tume kadhaa za Rais.

Aidha, alikuwa miongoni mwa waandishi wa Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2025 akichangia mawazo katika kuunda mwelekeo wa maendeleo ya taifa. Uzoefu wake katika nyanja mbalimbali za utawala, biashara na diplomasia umechangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya Tanzania katika sekta tofauti.

Pamoja na alama hizo alizoacha kwenye uongozi, Watanzania hususan waliopo katika ulimwengu wa siasa hawawezi kusahau Mwanasiasa huyo alivyokikacha Chama cha Mapinduzi  Oktoba 2015 na kuunga mkono safari ya matumaini ya aliyekuwa mgombea wa Urais Edward Lowassa na baadae kurejea katika chama hicho mwaka 2016 ikiwa ni miezi mitano baada ya uchaguzi kumalizika.

Baada ya taarifa ya kifo chake baadhi ya wanasiasa akiwemo Mbunge wa Bumbuli January Makamba ametuma salamu za rambirambi akimuelezea kama kiongozi shupavu aliyeacha alama miongoni mwa wengi.

“Alikuwa mtaalamu wa umma asiyejitangaza sana. Aliishi maisha yaliyojaa mafanikio, yanayostahili kusherehekewa. Ameacha alama isiyofutika mioyoni mwa wale aliowagusa na akilini mwa wale aliowafundisha.

Leo ameanza safari ambayo sote tutaiendea siku moja. Roho yake na ipumzike kwa amani ya milele,” ameandika January Makamba kupitia ukurasa wake wa X.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks