Watafiti wa afya watofautiana matumizi mashine za kukausha mikono
- Watafiti hao wanasema mashine hizo zisipotumiwa vizuri zinaweza kuwa chanzo cha kusambaa kwa bakteria wa magonjwa mbalimbali.
- Ni njia nzuri ya kutunza mazingira inayopunguza matumizi ya karatasi na ukataji wa miti.
- Kunawa mikono na kujifuta kwa kitambaa safi au karatasi laini inabaki kuwa njia nzuri zaidi ya kujikinga na bakteria.
Dar es Salam. Kutokana na ukuaji wa teknolojia, ni kawaida katika vyoo vya jumuiya kuwa na karatasi laini na mashine za kukaushia mikono ambazo hutumika mara baada ya watu kunawa mikono kwa maji.
Lakini matumizi ya mashine za kukaushia mikono kwa kiasi fulani yanatajwa kuwa sababu ya kusambaza bakteria wa magonjwa mbalimbali kutoka mtu mmoja kwenda mtu mwingine.
Mashine hizo hutoa upepo wenye hali ya joto kukausha mikono. Lakini wataalam wa afya wanasema upepo huo huchanganyika na hewa ya maliwatoni baada ya mtu kumaliza haja na hata mtu akikausha mikono anaweza kuondoka na bakteria wanaopatikana chooni.
Kulingana na utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Leeds, cha nchini Uingereza mwaka 2017 umebaini kuwa matumizi ya mashine za kukaushia mikono ni chanzo kimojawapo cha kupata bakteria wanaopatikana kwa njia ya hewa.
Utafiti huo ulilinganisha na kuangalia matumizi ya karatasi nyepesi na mashine za kukaushia mikono katika hospitali mbalimbali na kubaini kuwa bakteria wanaopatikana kwa kutumia mashine ya kukaushia mikono ni mara 27 ya kutumia karatasi.
Watafiti hao wanabainisha kuwa matumizi ya mashine hizo katika maeneo ya kutoa huduma za afya yanaweza yasiwe sahihi kutokana na kuwepo kwa bakteria wanaotokana na mwingiliano wa watu wenye magonjwa mbalimbali.
Inayohusiana:
Hata hivyo, watafiti wengine kutoka Chuo cha Connectcut wanaeleza kuwa bakteria hao wanaosambazwa kwa njia ya hewa hawana madhara makubwa katika afya za binadamu ikiwa mtu ana kingamwili ya kutosha kudhibiti magonjwa ya kuambukiza.
“Watu wenye kinga ya mwili imara wanaweza wasipate ugonjwa wowote” anasema, Dk Thomas Murray ambaye ni mmoja wa waandishi wa utafiti huo na mtaalam wa magonjwa ya kuambukiza.
Murray anafafanua kuwa utumiaji wa mashine hizo hauondoi dhana ya kuwa baadhi ya bakteria wanaweza kurudi mikononi mwa mtu na kumletea madhara.
Jinsi mashine zinazokausha mikono zinavyofanya kazi pindi uwekapo mkono.Picha| www.dealdey.com
Wataalamu wa afya nchini bado wanaamini mashine za kukaushia mikono ni teknolojia nzuri inayopunguza matumizi ya karatasi na kumuhakikishia mtu usalama wa afya yake kuliko kutokuwepo kabisa hasa katika maeneo yenye watu wengi.
Dk Victor Minja kutoka taasisi ya Health Promotion Tanzania (HPT) anasema mashine hizo zikitumika vizuri kuna uwezekano mkubwa wa kupunguza bakteria kama utajikausha kwa haraka na kutokushika sehemu nyingine baada ya kutoka maliwatoni.
“Uwezekano wa kupata magonjwa ni mdogo sana kama hutoshika sehemu nyingine, kwasababu mashine hizo zimetengenezwa kwa ustadi mkubwa,” anasema Dk Minja.
Hata hivyo, watafiti wanaamini kuwa kunawa mikono na kujifuta kwa kitambaa safi au karatasi laini (Tissues) ni njia nzuri zaidi ya kujikinga na bakteria.
“Kunawa mikono kunabaki kuwa njia nzuri ya kuondoa bakteria lakini kama hatutanawa mikono vizuri sehemu ya juu ya mikono na katikati ya vidole, unaweza kupata vidudu ndani ya sekunde 15 au 20,” anasema Dk Charles Gerba kutoka Chuo Kikuu cha Arizona nchini Marekani.