Washitakiwa 57 kati ya 61 wa kesi ya uhaini waachiwa huru Mwanza
- Ni baada ya upande wa mashtaka kuonyesha kutokuwa na nia ya kuendelea na mashitaka dhidi yao.
Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Ilemela, mkoani Mwanza imewaacha huru washitakiwa 57 kati ya 61 waliokuwa wanakabiliwa na kesi ya uhaini namba 26641/2025, baada ya upande wa mashtaka kuonesha kutokuwa na nia ya kuendelea na mashitaka dhidi yao.
Uamuzi huo umefikiwa leo Novemba 24, 2025 baada ya Wakili wa Serikali Mwandamizi wa Wilaya ya Ilemela, Safi Amani, akishirikiana na Mwanahawa Changale, na Clara Mhando kuwasilisha taarifa mahakamani kuwa mashitaka dhidi ya washitakiwa hao yanaondolewa.
Kufuatia Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kuonyesha kutokuwa na nia ya kuendelea na kesi hiyo kwao washatkiwa hao wameachiwa kwa kuzingatia Kifungu 92(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), Sura ya 20, marekebisho ya mwaka 2023,
Akitoa uamuzi huo, Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Ilemela, Stella Kiama, amesema kuwa pamoja na washtakiwa 57 kuachiliwa washitakiwa wengine wanne, Fredy Mabelele, Rwspochius Mwombeki, Toba Agustino pamoja na Costantine Sebastian, wanaendelea kubakia kwenye mashtaka hayo na kuendelea kusubiri kesi hiyo wakiwa mahabusu katika Gereza Kuu Butimba hadi Desemba 1, 2025, kesi itakapotajwa tena.
Aidha, kufuatai uamuzi huo baadhi ya wananchi wakiongozwa na wakili upande wa utetezi Amri Linus wameipongeza Serikali kwa uamzi huo na kueleza kuwa hatua hiyo inatoa mwanzo wa maisha ya mapya kwa vijana hao waliokuwa wameshitakiwa.
Hata hivyo, mbali na Mahakama ya Ilemela kuwaachia washitakiwa hao, Mahakama ya Nyamagana imewaachia washtakiwa wengine 63 wa makosa ya uhaini.
Itakumbukwa kuwa Novemba mwaka huu, wakati akilihutubia Bunge, Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, alimuomba Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) kuwafutia mashtaka ya uhaini vijana walioonekana kufuata mkumbo katika maandamano yaliyosababisha matukio ya uvunjifu wa amani Oktoba 29 mwaka huu.
“Natambua kuna vijana wengi wamekamatwa kwa kushtakiwa kwa makosa ya uhaini hawakujua wanachokifanya na wengine wamefuata mkumbo, nikiwa kama mama navielekeza vyombo vya kisheria kuangalia makosa yaliyofanywa na vijana wetu.
…Kwa wale ambao walifanya mambo kwa kufuata mkumbo na hawakudhamiria kufanya uhalifu wawafutie makosa yao,” alisema Rais Samia.
Jana Novemba 23, Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa aliwaambia wanahabari kuwa ombi hilo la Rais limeanza kufanyiwa kazi na wapo baadhi ya watuhumiwa wanaoachiliwa.
Imeandikwa na Kelvin Makwinya, nyongeza na Mariam John.