Rais Samia asisitiza amani zoezi la kupiga kura likiendelea Tanzania
- Awataka wananchi kukubaliana na matokeo ya uchaguzi huo pale yatakapotangazwa.
- Viongozi wa Serikali, vyama vya upinzani wajitokeza kupiga kura.
Arusha. Rais Samia Suluhu Hassan amewataka Watanzania kudumisha amani na utulivu wakati zoezi la kupiga kura kwa ajili ya kuwachagua viongozi wa Serikali za Mitaa likiendelea nchini.
Rais Samia ametoa maagizo hayo wakati akizungumza na wananchi leo Novemba 27, 2024 baada ya kupiga kura katika Katika Kijiji Cha Chamwino Jijini Dodoma ambapo amewataka wananchi kuhakikisha zoezi hilo linamalzika kwa amani.
“Ni matumaini yangu kwamba leo Watanzania watachagua viongozi wao katika ngazi za maeneo yao kwa salama na vizuri na watawachagua watu watakaowafanyia kazi zao,” amesema Rais Samia.
Pia Rais Samia amewataka wananchi kukubaliana na matokeo ya uchaguzi huo pale yatakapotangazwa na mamlaka husika.
Mbali na Rais Samia viongozi wengine wa Serikali na vyama vya upinzani wameshirki zoezi la Uchaguzi hao katika maeneo waliyojiandikisha wakitoa hamasa kwa wananchi wa maeneo hayo kujitokeza kushikiriki zoezi hilo la kidemokrasia.
Miongoni mwa viongozi hao ni Dk Philip Isdory Mpango pamoja na mke wake Mboni Mpaye Mapango waliopiga kura katika Kitongoji cha Kihanga Kijiji cha Kasumo Wilaya ya Buhigwe Mkoani Kigoma huku Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dk Doto Biteko akipiga kura katika kituo cha Shule ya Msingi Bulangwa wilayani Bukombe mkoani Geita.
Akizungumza na mara baada ya kupiga kura Dk Biteko amewasisitiza wananchi kujitokeza kushiriki zoezi hilo la kupiga kura wakizingatia amani na utulivu.
“Zoezi linakwenda vizuri niwaombe wananchi uchaguzi huu ufanyuke kwa amani na utulivu yule aliyeshinda atangazwe asiyeshindwa asitangazwe iwek haki bin haki kusitokee manunguniko mahali popote,”amesema Dk Biteko.
Jijini Mbeya Spika wa Bunge Dk Tulia Ackson amepiga kura katika kituo cha Uzunguni A, Kata ya Sisimba Jijini Mbeya ambapo amewataka wananchi kuendelea kujitokeza kwa wingi kushiriki zoezi hilo ili kupata viongozi bora.
Kwa upande wake Zitto Kabwe aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo amepiga kura katika Kitongoji cha Kibingo A mkoani Kigoma huku akifafanua umuhimu wa kushiriki zoezi hilo.
“Uchaguzi wa serikali za mitaa ni uchaguzi muhimu kwasababu ni uchaguzi wa viongozi wanaoshughulika na masuala ya kila siku ya wananchi…naomba watanzania wote wajitkeze kwa wingi,”amesema Kabwe.