Wanawake msisubiri kubebwa fursa za teknolojia – Wadau
- Washauriwa kukubali kuumia kwa muda mfupi ili waweze kufanikiwa katika ujasiriamali kwenye teknolojia mbalimbali.
- Wanawake washauriwa kujihusisha katika mahusiano na watu watakaowaruhusu kuweza kufanya kazi yao ya teknolojia vizuri.
Dar es Salaam. Wanawake wanaosubiri kubebwa ili kupata fursa za kiubunifu kwenye teknolojia huenda wakatumia muda mrefu kufanikiwa baada ya wadau kueleza kuwa mafanikio katika tasnia hiyo yanahitaji juhudi binafsi na mapenzi ya dhati katika ubunifu wa teknolojia na siyo upendeleo.
Hayo yamebainishwa leo (Januari 30,2018) na baadhi ya wawezeshaji wa Tamasha la Wanawake katika Teknolojia mwaka 2019 linaloendelea jijini hapa kwa siku mbili.
Tamasha hilo, linalofanyika kwa mara ya pili sasa, limehusisha wanawake ambao ni vijana au wanaochipukia katika teknolojia mpya zinazotazamiwa kuja kufanya kazi miaka ijayo kama miundombinu ya kuwezesha miamala na fedha au kutunza nyaraka mtandaoni ya ‘Blockchain’ ambayo inatazimiwa kuwa mfumo wa tatu wa kimapinduzi katika miamala ya pesa.
Ili wafanikiwe zaidi katika teknolojia, wanawake wanapaswa kujiamini, kujituma na kujitanua zaidi katika masula ya ubunifu wa teknolojia.
“Blockchain ni mwendelezo wa kidijitali katika manunuzi ya bidhaa au uhifadhi wa nyaraka mbalimbali kwa njia ya mtandao bila kumtumia mtu au kitu kama kiunganishi baina ya mtoaji na mpokeaji,” anasema Sandra Chogo mwanzilishi wa Blockchain Tanzania Community, taasisi inayojihusisha na masuala ya teknolojia hiyo.
Chogo amesema ndani ya miaka michache mbeleni watu watatumia mfumo huo wa blockchain hivyo anaona ni fursa ya wanawake kujifunza na kujua inavyofanya kazi ili waweze kujifungulia fursa zilizojificha nyuma ya teknolojia hii mpya.
Wanawake wazidi kuongezeka katika sekta ya ubunifu wa teknolojia ambalo ni jambo zuri zaidi. Picha| Buni Divaz
Mihayo Wilmore, mwanzilishi mwenza wa kampuni ya Twiga Alpha ambaye alikuwa mmoja wa washiriki katika jopo la wachokoza mada, amewaambia wanawake waache kujitofautisha na wanaume hasa katika suala la teknolojia.
Ili kufanikiwa zaidi katika nyanja hizo, amesema wanawake wanatakiwa kujifunza kuhakikisha wanakuwa na uvumilivu na uthubutu wa kufanya chochote ili wafanikiwe.
“Kama utakubali kuacha mahusiano, kukosa usingizi na kupoteza vingi ili kuwa mjasiriamali katika teknolojia basi utaweza kufanikiwa ila ukisema mimi mwanamke siwezi kufanya hivyo sahau kufanikiwa,” amesema Wilmore.
Hata hivyo, bado washiriki wengine wameona ni wakati mwafaka wa wanawake wanaopenda masuala ya teknolojia kuhakikisha wanajihusisha na watu wanye nia kama yao katika kuleta maendeleo kupitia teknolojia ili waweze kufika mbali zaidi.
Maoni ya wadau wengi ni kwamba wabunifu wengi wa teknolojia hasa wanawake wanapoteza mwelekeo na kuacha fani hiyo pindi wanapoolewa kutokana na shinikizo la familia au mume wake.
Zinazohusiana: Matumizi ya intaneti yanavyofichua fursa zilizojificha kwenye ‘smartphones’
Uhaba wa wanawake sekta ya teknolojia wakwamisha utekelezaji wa ajenda za maendeleo
“Ushauri wangu kwa wanawake katika kuchagua kazi na jamii inayokuzunguka, chagua kazi kwani haiwezi kukuacha,” amesema Wilmore.
Hata hivyo, Leah Buzuka mmoja wa wataalam wa programu za kompyuta amewataka wanawake kutokata tamaa hasa kwenye masomo ya sayansi na wanachopenda kufanya.
Licha ya yeye kuwa na ndoto ya kuwa rubani, Buzuka amesema hakufanikiwa lakini amekuwa mtaalamu wa programu za kompyuta na amejiajiri mwenyewe bila kutegemea mtu mwingine.
“Kazi za teknolojia hazihitaji ofisi inahitaji tu kompyuta yako, umeme na intaneti tu hivyo kama mwanamke unapenda kufanya kazi hizi hakikisha unajitoa na kutumia muda wako kuhakikisha unakuwa bora,” amesema Buzuka.
Pamoja na hayo Buzuka ameweka wazi kuwa sio kazi rahisi kupata mafanikio ya haraka hivyo wanawake wajiimarishe katika kutafuta masoko kipindi wanabuni programu zao ambazo zitasaidia kuleta msaada kwenye jamii na kutokukubali kukatishwa tamaa na watu wengine.