Wanahabari, wabunifu wapania kuinua teknolojia Tanzania
- Wametakiwa kushughulikia changamoto za uwekezaji na kuelewa kwa undani mazingira ya utendaji wa kila upande
- Wanahabari wapewa changamoto ya kubobea katika habari za masuala na kuachana kuripoti matukio.
Dar es salaam. Wadau wa masuala ya teknolojia wamevitaka vyombo vya habari na wabunifu nchini kuongeza ushirikiano ili kuiwezesha jamii kufahamu na kutumia kazi za ubunifu katika shughuli zao za maendeleo.
Wadau hao ambao wameshiriki mjadala ulioandaliwa na kampuni ya Nukta Africa kuhusu wa mchango wa vyombo vya habari katika kukuza ubunifu Tanzania uliofanyika leo (Machi 27,2019) jijini Dar es Salaam, wamesema wabunifu na Wanahabari wakifanya kazi kwa pamoja na kuondoa changamoto zinazowazunguka watatoa mchango muhimu wa kukuza ubunifu Tanzania.
Akiongoza majadiliano hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Nukta Africa, Nuzulack Dausen amesema bado fursa ni nyingi kwa Wanahabari kupata vyanzo vya habari za uhakika na wabunifu wa teknolojia wanaweza kuwa mahali sahihi kupata vyanzo hivyo.
“Wanahabari tunapaswa kuangalia mambo yaliyojificha ambayo tukijenga ukaribu na wabunifu tutapata vitu vingi vipya vya kurepoti kwa jamii,” amesema Dausen.
Mjadala huo uliondaliwa na Nukta Africa ni sehemu ya mfululizo wa matukio na mikutano ya wadau wa teknolojia wanaokutana katika maadhimisho ya Wiki Ya Ubunifu 2019 yaliyoandaliwa na Mfuko wa Ubunifu wa Maendeleo ya Watu (HDIF) na Tume ya Sayansi na Teknolojia yanayofanyika Machi 25-30, 2019.
Wadau wengine wamesema katika kukuza na kuimarisha ushirikiano kati ya vyombo vya habari na wabunifu wa teknolojia, kuna haja kila pande kushughulikia changamoto zake ikiwemo vyombo vya habari kuongeza uwekezaji na kutumia mifumo ya teknolojia ili kuweka mazingira yatakayovutia wabunifu kuzungumza lugha moja ya maendeleo.
“Uwekezaji katika vyombo vya habari uko chini sana hali inayosababisha waandishi wa habari kujikita katika uandishi wa kujiingizia kipato kuliko kuripoti mambo mapya kila siku,” amesema Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya Tai Tanzania, Ian Tarimo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Nukta Africa, Nuzulack Dausen akizungumza katika mjadala wa vyombo vya habari katika kukuza ubunifu Tanzania iliofanyika sambamba na Wiki ya Ubunifu 2019. Picha|Daniel Samson.
Katika hatua nyingine, Msimamizi wa kituo cha ubunifu cha Buni Hub, Paul Madela amesema uwekezaji wa vyombo vya habari uende sambamba na kuwaandaa Wanahabari waliobobea katika kuandika habari za teknolojia na sayansi ili kuwasaidia kuripoti habari kwa undani na kuachana na dhana ya kuripoti matukio ya kila siku ambayo huelezea zaidi matokeo kuliko mchakato na undani wa kazi za kibunifu.
“Waandishi wa habari wanatakiwa kuhakikisha wanaripoti sio tu matukio bali kwa kuzingatia ujuzi wa mambo zaidi,” amesema Madela.
Soma zaidi:
- Mgawanyo usio sawa wa vituo vya ubunifu unavyoathiri ukuaji wa teknolojia Tanzania
- Apps za elimu zinazoweza kuwaelimisha watoto wadogo kabla ya kwenda shule
- Wiki Ya Ubunifu inavyoangaziwa kuleta mabadiliko Tanzania
Wachangaiaji wengine akiwemo Cynthia Bavo kutoka taasisi ya Startup Grind Dar amesema ili wabunifu wapate fursa ya kusikika kwenye vyombo vya habari wanapaswa kuelewa utendaji wa vyombo hivyo na kujiandaa vizuri ili kuifikishia jamii habari iliyokamilika yenye kuleta matokeo chanya.
Naye Mwanahabari Mwandamizi kutoka kampuni ya Clouds Media Group (CMG) Joyce Shebe amesema Wanahabari wako tayari kufanya kazi na wabunifu, jambo la muhimu ni kujenga muunganiko au jukwaa litakawaleta pamoja ili kuangalia maeneo yanayopaswa kupewa kipaumbele.