Wanahabari wa mitandaoni sasa ruksa kushiriki tuzo za EJAT

September 20, 2018 10:38 am · TULINAGWE ALSON
Share
Tweet
Copy Link
  • Itakuwa mara ya kwanza kwa tuzo za EJAT kutoa fursa kwa wanahabari wa habari za mtandaoni tangu zilizopoanzishwa mwaka 2009.
  • Katika tuzo za mwaka huu kuna ongezeko la makundi mapya matatu na kutengeneza jumla ya makundi 19 yatakayoshindaniwa tofauti na mwaka jana.
  • Wanaoruhusiwa kuingia kwenye tuzo hizo ni wale waliosajiliwa TCRA.

Dar-es-Salaam. Kwa mara ya kwanza Baraza la Habari Tanzania (MCT) llimetoa nafasi kwa Wanahabari wa habari za mtandaoni kushiriki katika Tuzo za Umahiri za Uandishi wa Habari Tanzania (EJAT) za mwaka huu wa 2018.

Tuzo zilizokuwa zikitolewa hapo awali zilihusu wanahabari kutoka katika vyombo vya habari vya redio, magazeti na runinga pekee, lakini safari hii blogu, tovuti, redio na runinga za mtandaoni (Online Tv) za habari zitakuwa sehemu ya tuzo hizo.

Akizungumza katika uzinduzi wa tuzo za EJAT leo Jijini Dar es Salaam, Meneja Programu wa MCT, Pili Mtambalike amesema tuzo hizo zinafungua mlango wa fursa kwa kazi za wanahabari nchi kutambuliwa kulingana na makundi wanayotoka. 

“Waandishi wa habari kupitia mtandao walete stori zao zikiwa zimesajiliwa na kufuata vigezo vilivyowekwa kwa kila kipengele husika,” amesema Mtambalike.

Amebainisha kuwa wanahabari wa habari za mtandaoni wanaopaswa kushiriki tuzo hizo ni wale tu waliosajiliwa na kupewa cheti cha uhakiki kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA). 

Huenda hii ikawa ni fursa adhimu kwa vyombo vya habari vya mtandaoni kutambuliwa na kupewa heshima kwa mchango wao wanaoutoa kwenye shughuli mbalimbali za maendeleo nchini.

Aidha, katika tuzo za mwaka huu kuna ongezeko la makundi mapya matatu na kutengeneza jumla ya makundi 19 yatakayoshindaniwa tofauti na mwaka jana ambapo kulikua na makundi 16.

Makundi yaliyoongezwa ni ya habari za Uandishi wa habari za watoto, Uandishi wa habari za gesi, mafuta na uchimbaji madini na Uandishi wa habari za usalama na ubora wa chakula, dawa na vipodozi.

Makundi mengine ya habari yatakayozingatiwa katika tuzo za EJAT ni uandishi wa habari za biashara, uchumi na fedha; michezo na utamaduni; afya; kilimo na kilimobiashara; elimu na habari za utalii na uhifadhi.

Waandishi wa habari wa mitandaoni waliosajiliwa sasa ruksa kushiriki tuzo EJAT.| Picha na Tulinagwe Malopa.

Itakua ni mara ya kumi kwa kamati ya maandalizi ya EJAT kuandaa mashindano hayo ambayo kwa mara ya kwanza yalifanyika mwaka 2009. Tuzo hizi za juu na heshima zaidi kwa tasnia ya habari nchini huwatambua na kuwatunza waandishi wa habari wanaofanya kazi zao vizuri katika makundi mbalimbali.

Katika tuzo za mwaka 2017, kazi za kihabari 545 zilitumwa katika makundi 16 na kazi 49 tu zilichaguliwa kuingia kwenye kinyang’anyiro cha tuzo hizo.

Kati ya wateule hao 49, wateule 30 walitoka katika magazeti ambapo mmoja wao ni Mhariri Mkuu wa kampuni ya Nukta Africa Limited, Nuzulack Dausen aliyeshinda tuzo za mwanahabari bora wa habari za takwimu kwa upande wa magazeti. Awali Dausen alikuwa Mhariri wa Habari za Takwimu wa kampuni ya Mwananchi Communications Ltd inayochapisha magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti. Waliotoka redioni walikuwa 10 na runinga ni tisa.

Enable Notifications OK No thanks