Wanafunzi wasioona tabasamu tupu, Serikali ikizindua vitabu vya nukta nundu

February 27, 2020 2:27 pm · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni baada ya kuzindua na kuanza kugawa vitabu vya nukta nundu, maandishi makubwa na vitabu vya kiada vyenye ithibati ya Serikali
  • Uzinduzi huo utaenda kutengeneza ndoto mpya za kisayansi kwa wanafunzi wasioona na wenye uoni hafifu katika shule za msingi na sekondari.
  • Bado vitabu vya nukta nundu vya darasa la sita na saba havijakamilika, pia elimu ya juu ya sekondari (advance) haijafikiwa.

Dar es Salaam. Huenda wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari wasioona na wenye uoni hafifu nchini Tanzania wakapata ahueni na kuongeza ufaulu katika masomo yao, baada ya wadau wa elimu kuzindua vitabu vinavyoendana na hali zao. 

Uzinduzi wa vitabu hivyo vya nukta nundu uliaratibiwa na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) umefanyika leo (Februari 27, 2020) jijini Dar es Salaam ambapo vitasambazwa katika shule mbalimbali ambazo zina wanafunzi wenye matatizo ya kuona. 

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wiliam Ole Nasha aliyekuwa akizungumza katika uzinduzi huo amesema kuchapishwa kwa vitabu hivyo ni hatua ya kumfikia kila mtoto na kukamilisha azmio la elimu kwa watoto wote bila kujali hali zao za kiuchumi na kimwili.

“Moyo wa elimu upo kwenye maudhui. Hatutaishia katika kujenga majengo tu, kutoa elimu bure na kuajiri waalimu, Serikali utahakikisha wanafunzi wainapata vitabu na vitendea kazi ili kuboresha elimu,” amesema Ole Nasha.

Vitabu hivyo vya nukta nundu vitawanufaisha wanafunzi wa darasa la kwanza hadi la tano kwa shule za msingi huku wale wa sekondari vitawafikia wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha nne ambavyo vinajumuisha masomo ya sayansi ya fizikia, kemia na biashara (Commrce).

Hata hivyo, Ole Nasha ameitaka TET kutengeneza vitabu vya nukta nundu kwa ajili ya darasa la sita na la saba vikamilike mapema kuwanufaisha wanafunzi hao wasioona. 

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wiliam Ole Nasha aliyekuwa akizungumza katika uzinduzi huo amesema kuchapishwa kwa vitabu hivyo ni hatua ya kumfikia kila mtoto na kukamilisha azmio la elimu kwa watoto wote bila kujali hali zao za kiuchumi na kimwili.Picha| Rodgers George.

Wakati wanafunzi hao wakipata vitabu kupata maarifa na ujuzi, wenzao wa kidato cha tano na sita watalazimika kusubiri mpaka Serikali na wadau wa elimu watengeneze vitabu vya nukta nundu kwa ajili yao. 

Uzinduzi huo pia umeenda sambamba na uzinduzi wa vitabu vya kiada  kwaajili ya shule zinazofundhisha kwa lugha ya Kiingereza (English Medium). 

Vitabu vya kiada vilivyozinduliwa ni vya masomo sita vya darasa la kwanza na pili, vitabu vya masomo yote vya darasa la nne hadi la tano ambavyo  vyote ni mahususi kwa ajili ya shule hizo.

Mkurugenzi Mtendaji wa TET, Dk Aneth Komba amesema hadi sasa zaidi ya nakala milini 1.3 zimechapishwa na zinapatikana katika ofisi za kanda, mawakala na ofisi za TET na mdau yeyote wa elimu anaweza kuzipata kwa utaratibu uliowekwa.

“Vitabu vya nukta nundu 38,200 ambavyo vinagawiwa kwa uwiano wa kitabu kimoja kwa mwanafunzi mmoja kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu,” amesema Dk Komba akizungumzia vitabu hivyo vitakavyogawiwa bure kwa wanafunzi na  shule.


Zinazohusiana


Neema yawashukia walimu na wanafunzi wasioona

Walimu na wanafunzi wasioona walioongea na Nukta (www.nukta.co.tz) wamesema hiyo ni hatua kubwa katika kuwaboreshea mazingira ya kujifunzia na itakuwa na mchango mkubwa katika kuinua elimu ya wanafunzi wasioona Tanzania

Mwalimu anayefundisha wanafunzi wasioona katika Shule ya  Sekondari Lugoba iliyopo Chalinze mkoani Pwani, Fabian Simai amesema uzinduzi wa vitabu hivyo ambavyo vinahusisha vitabu vya masomo ya sayansi ni faraja kubwa kwa walimu na wanafunzi hao kwa sababu kwa muda mrefu walikuwa hawana vitabu vya nuktanundu.

Licha ya kuwepo kwa vitabu vingine kama “Song of Lawino” na Joka la Mdimu, mwalimu huyo amesema havikuwepo vitabu maalumu kwaajili ya masomo ya kiada ya darasani kwa wanafunzi hao wa kundi maalumu.

“Vilikuwa havipo. Mbadala wake tulikuwa tukitumia njia mbalimbali. “Kuja kwa vitabu hivi, vimekuwa ni muarobaini. Itasaidia kwa kiasi kikubwa watoto hawa kupata notsi kwa wakati,” amesema mwalimu huyo ambaye alitaja kati ya njia hizo ni kuwaomba wanafunzi wenzao wawasomee au walimu wa vitengo kuwasomea wanafunzi wasioona notsi zao ili wanafunzi hao waandike kwa lugha wanayoielewa.

Hata hivyo, njia hiyo haikuwa ya uhakika kwa sababu wanafunzi wasioona waliishia kupata notsi ambazo hazina uhalisia na hali zao.

“Imenipa morali ya kufanya vizuri kwenye masomo yangu kwani sasa nitakuwa nasoma kitabu changu huku wenzangu wakiwa wanasoma vitabu vyao,” amesema Joyce. Picha| Rodgers George.

Hata baada ya kuthibitisha vitabu hivyo, Mwanafunzi wa kidato cha nne kutoka shule ya Sekondari ya Lugoba mwenye matatizo ya kutokuona, Joyce Salum amesema “sasa nina uhakika wa kufaulu masomo yangu.”

Akianisha changamoto zinazomkumba kwenye elimu yake, Joyce amesema kusubiria mwanafunzi mwingine amsomee ndipo aandike ni changamoto kubwa kwani inamlazimu kutumia muda mwingi wa kupata maarifa sahihi.

“Imenipa morali ya kufanya vizuri kwenye masomo yangu kwani sasa nitakuwa nasoma kitabu changu huku wenzangu wakiwa wanasoma vitabu vyao,” amesema Joyce aliyeonekana kuwa na furaha ya kipekee.

Akiwakilisha wanafunzi wa shule za English Medium, mwanafunzi wa darasa la saba kutoka shule ya Fountain Gate Academy, Noreen John amesema licha ya kwamba vitabu vya darasa lake havijamalizika kwa sasa ana uhakika kuwa wadogo zake wa madarasa ya chini hawatopata shida kama alizozipitia yeye.

“Kwa masomo kama ya baiolojia, maneno magumu sana yanatumika kiasi cha kulazimika kuwa na kamusi ya Kiingereza ikiwa unasoma vitabu lakini naamini vitabu hivi vimeandikwa kwa lugha rahisi na wadogo zangu hawatolazimika kutafuta maana ya maneno ambayo siyo ya lazima,” amesema Noreen.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW