Gwajima aagiza anayedai kuteka watoto kuchukuliwa hatua za kisheria

September 29, 2025 3:07 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Asema kitendo hicho ni kinyume na Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009 na marekebisho yake ya mwaka 2019.
  • Aonya wazazi na watengeneza maudhui ya watoto kuzingatia sheria.

Dar es Salaam. Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dorothy Gwajima ameagiza hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya kijana aliyechapisha maudhui yanayodai amewateka watoto ili apate Sh 10  milioni.

Maudhui hayo ya picha jongefu (video) yamesambaa kupitia mitandao ya kijamii kuanzia Septemba 27, mwaka huu jambo lililozua mijadala na watu kutaka hatua zichukuliwe kwa mhusika .

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na wizara yake leo, Septemba 29, 2025, Dk Gwajima amesema kitendo hicho ni uvunjifu wa Sheria za Ulinzi wa Mtoto.

“Hivi wewe kijana unayewanyooshea mkono hao watoto hapo, je, unacho kibali cha kuwatumia kwa namna hiyo au umewakusanya tu ukaanza ‘content creation’?. Unajua kuwa watoto wanalindwa na sheria kuhusu matumizi ya mitandaoni?,” amehoji Dk Gwajima.

Aidha, Gwajima ameongeza kuwa, wananchi wanapaswa kushirikiana katika kumtambua kijana huyo na kumfikisha katika vyombo vya dola ili hatua stahiki zichukuliwe akisisitiza Watanzania kuzingatia sheria za nchi ikiwemo ya mtoto na ile ya makosa mtandaoni.

Kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 na marekebisho yake ya mwaka 2019,ni marufuku kuchapisha au kusambaza taarifa yoyote inayoweza kumdhuru mtoto au kumdhalilisha, ikiwemo jina, picha, au taarifa zinazoweza kumtambulisha

Sheria hiyo, inalenga kulinda haki, hadhi na ustawi wa kila mtoto dhidi ya aina zote za ukatili, unyanyasaji na matumizi mabaya, ikiwemo kwenye mitandao. 

Hata hivyo, marekebisho ya karibuni kupitia The Child Protection Laws (Miscellaneous Amendments) Act, 2024 yameimarisha ulinzi huo kwa kuongeza vifungu vinavyoadhibu vikali vitendo vya udhalilishaji au matumizi holela ya watoto katika maudhui ya kidigitali.

Sanjari na hilo , Dk Gwajima amewaonya wazazi na walezi kutowaruhusu watoto wao kutumika katika maudhui ya mitandaoni bila kibali cha kisheria, akisisitiza kuwa Serikali haitasita kuchukua hatua kwa yeyote atakayekiuka sheria za ulinzi wa mtoto.

Kwa mujibu wa maelekezo yake, yeyote mwenye taarifa sahihi kuhusu kijana huyo anatakiwa kuwasiliana kwa kutuma ujumbe mfupi wa maandishi kupitia namba 0765 345777 au kuwasiliana moja kwa moja na Jeshi la Polisi kupitia namba 0699 998899.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks