Walimu, wanafunzi wachangiana matundu manne ya vyoo kwa miaka miwili Kyela

January 30, 2019 1:34 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Tundu moja la choo linatumiwa na wastani wa watoto 209 kwa wavulana na wasichana.
  •  Wanafunzi na walimu watumia matundu manne kwa miaka miwili. 
  • Malumbano ya kisiasa ya kwamisha choo kipya kukamilika kwa wakati.

Kyela. Ni Saa sita mchana jua likiwa utosini wakati naingia shule ya msingi Mpanda iliyopo kata ya Ipyana wilayani Kyela katika mkoa wa Mbeya.  

Mazingira ya shule yaliyozungukwa na miti  mirefu, inayotoa kivuli kikubwa katika eneo hilo, ni tulivu kwa kuwa walimwanaendelea kufundisha madarasani.

Hata wakati masomo yakiendelea, wanafunzi hawaishi kutoka na kuingia madarasani. Wengi wanakimbilia katika jengo dogo lenye vyumba viwili  mita chache kutoka kwenye madarasa hayo.

Baada ya kulisogelea nabaini kuwa jengo hilo ni choo chenye matundu manne yanayotumiwa na walimu na wanafunzi wa shule hiyo kwa zamu. 

Kila chumba kina matundu mawili na kufanya watu wawili waingie kwa pamoja. Kila jinsi imegawiwa matundu mawili ili kupunguza adha.

Nje ya choo kuna ndoo kubwa iliyo wazi yenye maji kwenye mlango wa kuingilia. Kila mtu anayeingia katika moja ya vyumba hivyo huchota maji kwa kutumia kidumu kidogo kilichokatwa mdomoni kwa ajili ya kwenda kujisaidia.

Mwanafunzi wa darasa la sita katika shule hiyo, Joyce Mwabwagilo (13) anasema kwenye masomo wanafanya vizuri  changamoto kubwa ni upungufu wa  vyoo ambao hufanya kuingia msalani kwa foleni.

Uongozi wa shule unaeleza kuwa walimu 13 nao hutumia vyoo hivyo hivyo ,pamoja na wanafunzi 832 wa kuanzia darasa la awali hadi la saba. 

Kwa idadi hiyo ya wanafunzi, tundu moja la choo linatumiwa na wastani wa watoto 209 kwa wavulana na wasichana.  

Uwiano sahihi uliowekwa na serikali ni  tundu moja la choo  kwa  wasichana 20 (1:20) na kwa wavulana 25 (1:25). Kwa muktadha huo, Mpanda  ina upungufu wa matundu  34 yakiwemo 19 ya wasichana.

Awali choo hicho kilikuwa kimejengwa kwa ajili ya walimu pekee lakini kutokana na kutitia kwa choo cha wanafunzi chenye matundu 18 mwaka 2016 uongozi wa shule hiyo uliamua kitumike na jumuiya nzima.

“Tulijenga vyoo vya muda kwanza, vyoo vya kawaida lakini ni vichache matundu yako manne; mawili wasichana na mawili wavulana. Ni vile vya kuflashi, unamwaga maji,” anasema Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Hilder Kajubili.

Uchache wa vyoo hauwazuii walimu na wanafunzi kuzingatia usafi wakati wote watumiapo vyoo hivyo kwasababu wanatumia maji ya kisima kilichopo pembeni  ya shule hiyo.

“Kwasababu kuna kisima, maji yanawekwa kila siku kwenye majaba wanatumia na vibuyu chirizi tumetengeneza wananawa baada ya kutoka chooni,” amesema Mwalimu Hilder.

Pamoja na kwamba nje ya choo hicho kuna vibuyu chirizi vya plastiki  vilivyoning’inizwa kwenye kamba ambavyo hutumika kunawia mikono, Nukta imebaini kuwa siyo wanafunzi wote hunawa na sabuni.

“Hali ya huduma ya choo mara ya kwanza ilikuwa nzuri, tulikuwa na matundu 18 ambayo yalititia na mvua mwaka juzi 2016. Serikali kupitia Halmashauri (ya Kyela) ilitoa Sh200,000 tukajenga matundu manne ambayo yako mpaka sasa hivi yanatumika,” anasema Mwalimu Hilder.

Hali hiyo haitofautiani sana na shule zingine wilayani Kyela ambazo nazo zinakabiliwa na upungufu mkubwa wa vyoo. 

Takwimu kutoka Ofisi ya Afisa Elimu Takwimu wa Wilaya ya Kyela zinaonyesha kuwa hadi kufikia mwaka 2017, wilaya hiyo ilikuwa na wanafunzi 55,821 wa shule za msingi ambao walikuwa na  mahitaji ya matundu 2,470 lakini yaliyokuwepo ni 1,761 tu. Hali hiyo imefanya shule za halmashauri hiyo kuwa na upungufu wa matundu 709.

Hata hivyo, hali hiyo ni nafuu ikilinganishwa na miaka mitano iliyopita hasa mwaka 2013 ambapo kulikuwa na uhaba wa matundu 1,411 ikilinganishwa na mahitaji ya matundu 2,393.

Choo chenye matundu manne kilichokuwa kinatumiwa na walimu 13 na wanafunzi 832 wa shule ya msingi Mpanda wilayani Kyela, jambo lililokuwa linahatarisha afya zao na utoaji wa elimu bora. Picha| Daniel Samson.

 

Kutokana na upungufu wa madarasa na vyoo uliopo shuleni hapo, uongozi wa shule hiyo ulilazimika  kuwagawa wanafunzi  katika mikondo miwili ambapo wanafunzi  wa darasa la awali, I, II na VII wanaingia asubuhi na wale wa darasa la III, IV. V, VI wanaingia mchana ili kuhakikisha vyoo vilivyopo vinatumika vizuri kuwaepusha wanafunzi na magonjwa ya mlipuko.

Mwalimu Douglas Mwalukasa wa shule hiyo anasema uwepo wa mikondo ya asubuhi na mchana umesaidia katika utumiaji wa matundu hayo manne. 

Hatua nyingine wanayochukua ni kulinda afya za wanafunzi kwa kutoa mafunzo ya usafi na kujikinga na magonjwa wanapotumia vyoo. 

Kutokana na udogo wa wanafunzi wao, mwalimu huyo anaeleza kuwa wameweka usimamizi madhubuti wa usafi wa mazingira ya choo na matumizi ya maji safi na salama wakati wote wanafunzi wanapokuwa shuleni.

Kwanini wametumia matundu manne kwa muda mrefu?

Wanafunzi na walimu hao wasingekuwa wanataabika kwa miaka miwili sasa iwapo ujenzi wa choo kingine chenye matundu 12 ungekamilika kwa wakati.

 “Baada ya choo cha awali kutitia tulipewa hela na Mbunge wetu ambaye pia ni Waziri wa Habari, Sanaa, Michezo na Utamaduni Dk Harrison Mwakyembe kupitia mfuko wa jimbo Sh5.28 milioni ili tujenge vyoo. 

“Mpaka sasa hivi tulishajenga tumeezeka lakini bado havijaanza kutumika kwa sababu bado umaliziaji,” anasema Mwalimu Hilder.

Ujenzi wa choo hicho umekwama kutokana na uwepo wa  malumbano ya wanasiasa  ambao wanadaiwa kuwakataza  wazazi kuchangia fedha kwaajili ya uboreshaji mazingira ya kusomea shuleni hapo.

“Michango inasuasua ya wananchi kwasababu sielewi mambo ya kisiasa. Mambo ya siasa hayo nina wasiwasi nayo, wananchi wako tayari kufanya kazi hata kutoa hela ukipata mtu ambaye siyo mhamasishaji hawawezi kufanya,” amesema Mwalimu Hilder na kuongeza kuwa,

“Huko mwanzoni tulikuwa tunatumia kamati za shule tulikuwa tunakaa na ndio maana unaona mambo mengine yamefanyika.”

Baadhi ya wakazi wa maeneo hayo kwa sasa hawajishughulishi tena kuchangia maendeleo ya shule zao baada ya Serikali kutangaza Elimu Bure.

Mkazi wa Kijiji cha Mpanda ilipo shule hiyo, Japhary Mhando, anasema tangu serikali izuie michango yote shuleni wazazi hawajishughulishi tena na  masuala ya uboreshaji miundombinu ya shule. 

“Sera ya elimu bure imeleta changamoto kwa wazazi kuchangia maendeleo ya shule. Wengine wako tayari kuchangia lakini uhamasishaji umekuwa mdogo hapa kijijini,” anasema Japhary na kuongeza kuwa wazazi waweke kando itikadi za kisiasa na waungane katika maendeleo ya shule.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mpanda, Gibonce Mwambije (Chadema) anatuhumiwa kuhamasisha wananchi kutochangia maendeleo ya ujenzi wa choo hicho kiasi cha kufanya mradi uchelewe.

Hata hivyo, Mwambije amepinga vikali tuhuma hizo na kueleza kuwa anaendelea kuhamasisha wakazi wa eneo hilo watoe fedha kiasi cha Sh2,000 kila kaya ili kumalizia ujenzi wa choo hicho.

Wiki moja baada ya Nukta kutembelea shule, mwandishi wetu amejulishwa kuwa Dk Mwakyembe ameshaingiza Sh1.5 milioni kwenye akaunti ya shule hiyo kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa choo hicho.

Licha ya shule Msingi Mpanda kukabiliwa na changamoto ya upungufu wa matundu ya vyoo kwa miaka miwili mfululizo, bado walimu wameendelea kufundisha kwa moyo  na kuifanya shule hiyo kuwa miongoni mwa shule zinazofanya vizuri katika matokeo ya darasa la saba wilayani Kyela.

Katika matokeo ya mwaka 2016, wakati choo cha wanafunzi kinatitia, shule hiyo ilishika nafasi ya nane kiwilaya na mwaka uliofuata wa 2017 ilipanda na kushika nafasi ya 3  kati ya shule 102.

Wakati wanafunzi na walimu wa shule ya msingi Mpanda wilayani Kyela wakikabiliana na kukabiliwa na upungufu wa vyoo, shule yao pia ina uchakavu na madarasa jambo linalowafanya wanafunzi kusoma kwa kupokezana. Picha|Daniel Samson.

Katibu wa Chama Cha Walimu (CWT) wilaya ya Kyela, Obby Kimbale ameishauri serikali kuboresha mazingira ya shule ikiwemo ujenzi wa vyoo ili kuwawezesha walimu kufundisha bila vikwazo na kuhakikisha wanafunzi wanapata maarifa yaliyokusudiwa.

“Vitu tunavyozingumza ni kuboresha mazingira kwa ujumla ya shule maana choo ni mazingira kwahiyo tunasisitiza mahali pa kazi panatakiwa kuwa panavutia kwa maana ya kupata huduma zote ikiwemo huduma ya choo,” anasema Kimbale. 

 Asasi ya kiraia ya HakiElimu inabainisha kuwa uhaba wa matundu ya vyoo ni changamoto inayozikabili shule nyingi za msingi hapa nchini hali inayosababisha wanafunzi, katika baadhi ya shule, kujisaidia kwa kupanga foleni na huku baadhi ya shule zikiwa hazina kabisa huduma ya choo na hivyo kulazimu wanafunzi kujisaidia vichakani.

Halmashauri yatafuna ‘mfupa’ mdogo mdogo

Mratibu Elimu wa kata ya Kyela, Hezron Mwaikinda ambaye alikuwa anasimamia kata ya Ipyana ilipo shule hiyo  amekiri kuwa shule nyingi zina upungufu wa vyoo na  mikakati iliyopo ni kujenga madarasa na vyoo ili kukabiliana na ongezeko la wanafunzi linalotokana na elimu bila malipo.

“Tunayo mipango kazi inayoainisha mambo ambayo yamepewa kipaumbele kwa mwaka huu. Jukumu tulilonalo ni kuwaomba wadau mbalimbali watusaidie katika kuchangia ujenzi wa vyoo, wananchi wamekuwa wakichangia ipo michango ambayo imekuwa inapita kupata msaada ili vyoo viwe vimekamilika,” anasema Mwaikinda.

Afisa Elimu wa Mkoa wa Mbeya, Paulina Ndigeza amewataka wananchi kuwajibika na uboreshaji wa miundombinu ya shule ikiwemo vyoo katika maeneo waliyopo.

Anasema Serikali ina sehemu yake ya kufanya lakini pia jamii  ina sehemu yake. 

“Katika waraka wa Elimu namba tatu wa mwaka 2016  una kipengele kinachotaka jamii kutumia nguvu zake kuboresha miundombinu na mahitaji mengine ya shule,” anasema Ndigeza.

Anabainisha kuwa ujenzi wa vyoo unategemea mipango ya Halmashauri katika kupanga vipaumbele katika elimu kulingana na fedha wanazopokea kutoka serikali kuu.

Enable Notifications OK No thanks