Wakulima wa miwa Morogoro kunufaika na fursa za mikopo, soko

December 8, 2018 5:46 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link

Serikali imeanzisha Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kwa lengo la kuwasaidia wakulima wakiwemo wa miwa wapate mitaji ili waongeze tija katika shughuli zao. Picha| IPP Media.


  • Watazipata baada ya kuanza kuuza miwa katika viwanda viwili katika maeneo ya Mkulazi wilayani Ngerengere na Mbigiri wilayani Mvomero katika mkoa wa Morogoro ili kupunguza tatizo la upungufu wa sukari nchini. 
  • Wakuu wa wilaya za Kilosa na Mvomero mkoani Morogoro watakiwa kuwahamasisha wananchi katika maeneo yao kuchangamkia fursa ya kilimo cha miwa.
  • Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) nayo kuwaunga mkono wapate mitaji ya kuongeza tija katika shughuli zao.

Dar es Salaam. Wakulima wa miwa katika kijiji cha Mbigiri wilayani Mvomero mkoa wa Morogoro wako mbioni kufaidika na fursa za mikopo na soko la zao hilo kutokana na uwepo wa kiwanda cha Mkulazi II kinachotarajiwa kujengwa katika eneo hilo ili kupunguza tatizo la upungufu wa sukari nchini.  

Mkulazi, ambayo ni kampuni hodhi iliyoanzishwa kwa ubia baina ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa Taifa  (NSSF) na Mfuko wa Pensheni wa Mashirika ya Umma (PPF) Septemba 2016, imepanga kujenga viwanda viwili katika maeneo ya Mkulazi wilayani Ngerengere na Mbigiri wilayani Mvomero katika mkoa wa Morogoro. Viwanda hivyo kwa pamoja vitakapokamilika vinatarajiwa kuzalisha wastani wa tani 250,000 za sukari kwa mwaka.

Ili kufanikisha azma hiyo, Mkulazi iliandaa utaratibu chini ya Mpango wa wakulima wa nje wa miwa (Mkulazi Sugarcane Out growers Scheme) ili kuwawezesha wananchi kupata mitaji na teknolojia ya kisasa ya  kulima miwa na kuviuzia viwanda vitakavyojengwa katika maeneo yao.

Jana jioni (Desemba 7, 2018) Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliwataka wakuu wa wilaya za Kilosa na Mvomero mkoani Morogoro wahahakikishe wanawahamasisha wananchi katika maeneo yao kuchangamkia fursa ya kilimo cha miwa.

Wakulima hao watasaidia kuongeza uzalishaji sambamba na mashamba mengine yanayomilikiwa na Serikali katika eneo hilo ili kuhakikisha miwa inapatikana muda wote katika viwanda.

Sambamba na hilo Majaliwa amesema Serikali imeanzisha Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kwa lengo la kuwasaidia wakulima wakiwemo wa miwa wapate mitaji ili waongeze tija katika shughuli zao.

Majaliwa aliyasema hayo wakati ametembelea shamba la miwa Mkulazi na Mbigiri mkoani Morogoro alipokuwa njiani kwenda Jiijini Dodoma na kubainisha mashamba hayo yameanzishwa ili kuhakikisha mahitaji ya sukari nchini yanafikiwa katika kiwango kinachohitajika.

Amesema Serikali imepanga kuzalisha sukari itakayotosheleza mahitaji na njia pekee  ni kuboresha kilimo cha miwa, kujenga viwanda vitakavyozalisha sukari ya kutosha.

“Nataka shamba hili lisimamiwe kitaalamu, uzalishaji uwe wa kitaalamu na liwe mfano na mashamba mengine, tusishindwe na watu binafsi,” amesema Majaliwa katika taarifa iliyotumwa na ofisi yake kwa wanahabari.


Zinazohusiana: Mkulazi kuwawezesha wakulima wadogo kuzalisha sukari Morogoro


Hadi sasa Nukta kupitia taarifa ya Wizara ya Biashara,Viwanda na Uwekezaji inatambua kwamba, viwanda vya ndani vinazalisha wastani wa tani 300,000 kwa mwaka wakati mahitaji halisi ni takribani tani 420,000 kwa mwaka, hivyo kuwepo kwa pengo la tani 120,000. 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Jenista Mhagama amesema shamba la Mkulazi II ni miongoni mwa mashamba mawili yanayomilikiwa na wabia wawili yaani NSSF na Jeshi la Magereza.

Amesema walikubaliana wao na Magereza wafanye kazi kwa kuongozwa na uzalendo, maadili ya utendaji wa kazi, uaminifu ili mwisho wa siku mradi huo uwe na tija na uweze kuwafikisha katika malengo yaliyokusudiwa.

Ikiwa mpango huo wa uzalishaji miwa na ujenzi wa viwanda vya sukari utatekelezwa kikamilifu, huenda ukasaidia kuondoa changamoto za uagizaji sukari nje ya nchi ili kufidia upungufu unaojitokeza kila mwaka. 

Kujengwa kwa viwanda hivyo, kutaufanya mkoa wa Morogoro kuwa na viwanda vinne ukilinganisha na viwili vilivyopo sasa vya Mtibwa na Kilombero. Viwanda vingine ni Kagera Sugar cha mkoani Kagera na TPC – KIlimanjaro.  

Enable Notifications OK No thanks