Wafahamu wanawake wenye miguu yenye thamani zaidi duniani

December 10, 2021 8:14 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Orodha hii inaongozwa na Mariah Carey ambaye ameiwekea bima miguu yake kwa zaidi ya Sh trilioni moja.
  • Watu wengine ni wanamuziki na wana mitindo.
  • Siyo miguu tu, wapo waliokatia bima ndevu na ndimi zao.

Ukipewa Dola za Marekani milioni 100 sawa na zaidi ya Sh230 bilioni utafanyia nini? Wapo ambao watawaza kujenga nyumba, watakao waza utalii na wengine watahisi kuusahau umasikini.

Hata hivyo, pesa hiyo ni bima ya miguu kwa baadhi ya watu maarufu ulimwenguni wakiwemo wasanii wa muziki na waigizaji wa filamu.

Wakati sehemu kubwa katika jamii zetu wakishindwa kumudu gharama za kukata bima kwa ajili ya afya na mali zao kama magari, nyumba, ofisi na viwanja, unaweza kushangazwa na watu maarufu ambao wameamua kukatia miguu yao bima tena kwa mamilioni ya fedha.

Bima ya sehemu ya mwili/ viungo vya mwili kwa mujibu wa tovuti ya Fox Business, hukatwa ili kufidia gharama za matibabu kwa mtu ambaye miguu yake itapata changamoto yoyote ikiwemo ajali, ulemavu na hata makovu. 

Bado upo njia panda? Ifuatayo ni kati ya miguu ambayo thamani ya bima yake huenda ikakujengea nyumba na hata kukufanya uuage umaskini.

Mariah Carey: Sh2.3 trilioni

Unaweza kumfahamu mwanamke huyu kwa sauti yake iliyowahi kuwakosha wengi kiasi cha kujiuliza iwapo ni mwanadamu wa kawaida au ameshushwa. Kwenye nyimbo kama “Emotions”, “Holy Night” na nyingine nyingi, mwanadada huyu ameonyesha utaalamu wa muziki ambao ni wachache duniani wanaweza kuufikia.

Mbali na hayo, huenda ni kawaida kumuona mwanamuziki huyu akiwa amevalia vijivazi vinavyoacha miguu yake nje. Miguu hiyo imewahi kukatiwa bima ya Dola za Marekani, bilioni moja sawa na Sh2.3 trilioni.

Mwaka 2006, Carey alitwaa tuzo ya miguu bora nchini Marekani kutoka Gillete Venus, kampuni inayotengeneza nyembe za kunyolea. Mguu yake hiyo ilipata sanamu ya futi 16 iliyowekwa New York kwenye holi la muziki la Radio City.

Mariah Carey amewahi kutwaa tuzo ya mwanamke mwenye miguu mizuri zaidi nchini Marekani. Picha| Globo.

Taylor Swift: Sh92.8 bilioni

Ni kawaida kumuona Swift na vijigauni ama vibukta vifupi, hivyo sio haba kufahamu kuwa miguu hiyo anayoionyesha ina thamani kuliko ulivyodhani.

Mwaka 2015, Swift alikuwa na ziara ya kimuziki iliyojulikana kama “1984”. Mwanadada huyo aliikatia bima miguu yake kwa thamani ya Dola za Marekani milioni 40 (Sh92.8 bilioni). Ikiwa ni hatua ya kuhakikisha show zake zinakamilika hata pale atakapopata shida yoyote.

Tina Turner: Sh7.4 bilioni

Kwa miondoko ya mwanamuziki huyu akiwa stejini inaweza ikawa moja ya chachu iliyomfanya aikatie miguu yake bima. Tina Turner ambaye wimbo wa “Whats love” ulikita kwenye mamilioni ya spika nyingi ulimwenguni, hutambulishwa na mtindo wa nywele zake na miguu yake ambayo amekuwa akiionyesha kwenye vijigauni vya kung’ara akiwa stejini. 

Turner (81) amewahi kuikatia miguu yake bima yenye thamani ya Dola za Marekani, 3.2 milioni (Sh7.4 bilioni) na mwaka 1994 alitunga wimbo wa “Legs” kwa ajili ya kudadavua kazi ya miguu yake.

Tina alikosha nyoyo za mashabizi wake kwa sauti, miondoko akiwa jukwaani na miguu yake. Picha| Today Tix

Heidi Klum: Sh4.6 bilioni

Unaweza kumfahamu Klum kama unafuatilia masuala ya mitindo almaarufu kama “Fashion” kwa kuwa ameacha alama kwa muondoko wake kama twiga awapo nyikani.

Pia, mwanadada huyu ni miongoni mwa majaji wa muda mrefu kwenye mashindano ya kusaka vipaji nchini Marekani, “America’s got Talent” akiwa na nguli wengine kama Mel B kutoka Spice Girls na Simon Cowel.

Miguu ya Klum iliwahi kukatiwa bima yenye thamani ya Dola za Marekani 2 milioni (Sh4.6 bilioni) kuhakikisha kuwa ipo salama wakati wote hata akitembea kwenye viatu virefu kwenye majukwaa mbalimbali.

Wanaume wakatia bima hadi ndevu

Wanaume nao hawajaachwa nyuma katika kukatia bima. Mwana soka Christiano Ronaldo amekatia bima miguu yake kwa Sh333.9 bilioni huku David Beckham akikatia bima miguu na uso wake kwa gharama ya Sh452.2 bilioni kwa mujibu wa orodha ya tovuti ya CNBC.

Unaweza staajabu hayo lakini wapo watu wengine maarufu ambao wameweka bima kwenye mambo mbalimbali. 

Msanii JLo (Jennifer Lopez) aliwahi kuweka bima yenye thamni ya Sh39.4 bilioni kwa ajili ya makalio yake ikiwa ni kwa mujibu wa gazeti la mitindo, Elle

Wapo wengine waliokatia bima ya ndevu akiwemo mchezaji wa “Cricket” Merv Hughes, tabasamu (muigizaji Julia Roberts) na hata ulimi (mwanamuziki wa miondoko ya “Rock”, Gene Simmons) na vidole gumba kama dereva wa mbio za magari Fernando Alonso). Wewe bima yako umekatia nini? Endelea kufuatilia Nukta habari.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW