Wafahamu vinara wa haki za binadamu
- Vinara hao ni Pili Mkemi, Bonny Matto na Zainab Mire.
- Kwa pamoja wamesaidia upatikananji wa haki za binadamu kwenye mikoa ya Mara, Kilwa na Dar es Salaam.
Dar es Salaam. Kituo Cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimewapa tuzo vinara watatu wa kutetea haki za binadamu nchini Tanzania ili kutoa hamasa watu kupigania na kunufaika na haki hizo katika maisha yao ya kila siku.
Mkurugenzi wa Ujengaji Uwezo na Uwajibikaji wa LHRC, Felista Mauya amesema mashujaa hao ni Pili Mkemi, Bonny Mato na Zainab Mire.
Vinara hao wanafanya kazi kubwa ya utetezi wa haki za binadamu ikiwemo kupinga vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto kwenye jamii zao.
“Pili Kuliwa alijenga uelewa miongoni mwa wanawake katika mji wake (Kilwa mkoani Lindi) kuhusu vitendo vya ukatili wa kijinsia na mila mbaya ikiwemo unyago,” amesema mkurugenzi huyo wakati wa kutoa wasifu wa vinara hao kwenye maadhimisho ya siku ya haki za binadamu yaliyofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam.
Tangu alipojiunga na kituo hicho mwaka 2003, Kuliwa amefanya mengi kwenye jamii yake ikiwemo kuchagiza mabadiliko katika kituo cha polisi kilichopo kwenye mji wa Kilwa ambacho kilikuwa kinachanganya wanawake, wanaume na watoto kwenye chumba kimoja, jambo ambalo ni kinyume na haki za binadamu.
“Pili pamoja na wanawake wenzake walitoa uelewa kwa polisi na wananijiji kuhusu suala hilo kuwa ni kinyume na mahitaji ya kijinsia na sasa watuhumiwa hawachanganywi tena,” amesema Mauya.

Pili Kuliwa (kushoto) akipokea tuzo kutoka kwa Mkurugenzi wa haki za binadamu Wizara ya Katiba na Sheria, Ngasory Sarakikya(kulia) baada ya kutajwa kama kinara wa kutetea haki za binadamu. Picha| LHRC.
Shujaa huyo hakuishia hapo mwaka 2016 aliunda jukwaa ambalo liliwaleta pamoja wanawake wenzake kwenye mji anaoishi ili kuunganisha nguvu kutetea haki za wanawake na kuwakomboa kiuchumi.
Kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo mamlaka za Serikali za mitaa na halmashauri Pili ameweza kuwasaidia wanawake kupata mikopo unao wawezesha wanawake kwenye Jukwaa hilo ambalo kwa kwa sasa lina wananchama 525.
Kinara mwingine aliyetambuliwa kwenye maadhimisho hayo ni Bonny Matto. Ni msomi wa Stashahada ya Uhasibu anayehamasisha haki za binadamu mkoani Mara.
Licha ya usomi wake amekuwa msaada mkubwa wilayani Tarime ambapo huwasaidia wananchi dhidi ya madhila mbalimbali wanayoyapata hasa kutoka kwa wawekezaji wa madini.
“Bonny Matto ni msaada mkubwa kwa jamii yake ya Tarime… mwaka 2013 alisaidia watu 40 kupata fidia baada ya kupata madhara yaliyotokana na mgodi wa north mara,” amesema Mauya.
Kijana huyo pia ni kinara wa kuripoti matukio ya uvunjwaji wa haki za binadamu kupitia mfumo wa kidigitali wa shirika hilo ‘Haki Kiganjani’ unaotumiwa kukusanya matukio ya uvunjwaji wa haki za binadamu.
Zinazohusiana
-
Shughulikieni changamoto zinazorudisha nyuma haki za binadamu
-
Lhrc yaeleza sababu kuendelea kwa mauaji ya wanawake, ikitoa suluhu
Mathalan, mwaka 2022, Matto aliripoti matukio 81 ya uvunjwaji wa haki za binadamu. Kati ya hayo asilimia 50 ni matukio ya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake.
Hata baada ya kuripoti matukio ya uvunjwaji wa haki za binadamu kinara huyo hufanya kazi ya ziada kuhakikisha watuhumiwa wanafikishwa mahakamani na haki inapatikana.
“Bonny Matto amekuwa akienda mbali zaidi baada ya kuripoti huwasaidia wahanga na kuhakikisha watuhumiwa wanahukumiwa na haki inapatikana,” ameongeza Mauya.

Bonny Matto amekuwa ni miongoni mwa wapigania haki za binadamu nchini Tanzania huku akilenga kuinua maisha ya watu waishio maeneo ya migodini. Picha | LHRC).
Kinara wa tatu ni Zainab Mire, daktari wa kujitolea hospitali ya Aga Khan aliye na shahada ya utabibu anayewasaidia wanajamii kipitia misaada ya hisani na huduma za jamii.
Kutokana na kukosekana kwa usawa wa kijinsia kwenye jamii yake, binti huyo hutumia kila fursa kuwapigania na kuwajengea wanawake uwezo wa kujitambua.
“Zainab hutumia kila fursa kusaidia na kuwapigania wanawake, kuunga mkono uongozi wa vijana na kusaidia kufadhili, na kuwajengea uwezo wanawake, “ amesema mkurugenzi huyo akimalizia kusoma wasifu wa vinara hao.
Latest