Wadau wa Tehama wanavyozikuza, kuziimarisha ‘startups’ za Tanzania
- Wanatumia programu za mafunzo ya vitendo chini ya wakufunzi waliobobea kwenye ujasiriamali wa teknolojia.
- Vijana wenye mawazo bunifu wapania kuyaendeleza ili kuifikia jamii kwa upana.
- Changamoto za kodi na uanzishaji wa kampuni bado ni kikwazo kwa startups kukua.
Dar es Salaam. Vijana wa Tanzania hawajabaki nyuma, wanakwenda na wakati na mabadiliko ya sayansi na teknolojia.
Kama ilivyo kwa wenzao duniani, nao kila siku wanatafuta njia za kutatua changamoto za jamii kwa kutumia ubunifu na uvumbuzi wa teknolojia.
Licha ya kuwekeza muda wao katika kuisaidia jamii kwa kutumia teknolojia kupata huduma na bidhaa kuboresha maisha, bado wanakabiliwa na changamoto ya kupata jukwaa au sehemu ya kuonyesha na kuendeleza mawazo yao bunifu.
Lakini kampuni ya uwekezaji na uendelezaji wa ujasiriamali wa teknolojia ya Seedspace ya jijini Dar es Salaam wameamua kukaa mstari wa mbele ili kuwasaidia vijana wenye mawazo bunifu kuyaendeleza ili kuleta matokeo yaliyokusudiwa katika jamii.
Hivi karibu iliandaa mafunzo ya kuzijengea uwezo kampuni 11 zinazoibukia (startups) chini ya program ya #AndelaTechLeadersProgram ili kuhakikisha zinasimama na mawazo yao yanawekwa katika mfumo wa soko unaoweza kuleta matokeo chanya katika jamii.
Meneja Mafunzo wa Seedspace, Mohammed Shellimoh anasema katika programu hiyo wamezijengea uwezo startups hizo ili zijiendeshe kibiashara na kuwa na mfumo wa taasisi kuweza kutekeleza mawazo yao katika soko la bidhaa na huduma.
“Tunawasaidia kuanzia mwanzo wa mawazo yao hadi pale mawazo yao yanapofanikiwa kuisaidia jamii ya watanzania” anasema Shellimoh.
Baada ya mafunzo hayo yaliyodumu kwa takriban siku tano, startups tano zilizofanikiwa kuchaguliwa kuendelea na programu nyingine ya miezi mitatu itakayoanza Julai mwaka huu ili kunolewa zaidi katika sekta ya teknolojia.
Startups zilizofanikiwa kupenya ni ‘Code Lady’, ‘Smart Elimu’, ‘Msafiri App’, ‘Smart book’ na ‘Seedys’ ambazo mikakati yake inafaa kuendelezwa ili kuifikia jamii kwa upana zaidi.
Soma zaidi:
- Mambo muhimu yatakayozisaidia kampuni zinazochipukia Tanzania kukua
- Startups za Tanzania zilizotamba mwaka 2018
Baadhi washiriki wa mafunzo hayo wameiambia www.nukta.co.tz kuwa ilikuwa ni fursa adhimu ya kukutana na wakufunzi waliobobea katika ujasiriamali wa teknolojia.
Pia wamepata nguvu ya kuboresha mawazo yao ili kuvutia wawekezaji wenye nia ya kuwekeza katika kampuni zinazochipukia.
Simon Mduma ambaye ni mwanzilishi wa Msafiri App amesema programu hiyo ni mahususi kutatua changamoto ya foleni katika vituo vya kukatia tiketi za mabasi yaendayo kasi ambapo mtu anaweza kukata tiketi mtandaoni bila kwenda kituoni.
Amesema App hiyo inakusudia kumaliza tatizo la kukaa muda mrefu katika foleni ya kukata tiketi kwenye vituo vya mabasi ya mwendo kasi.
Hata hivyo, wanahitaji mafunzo zaidi na kushirikiana na wadau wa usafiri ili kuangalia namna watakavyoboresha wazo hilo na kuwafikia watoa huduma wengi wa tiketi za kielektroniki za usafiri.
Washiriki wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kukamilisha mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kuyaendeleza mawazo bunifu katika teknolojia. Picha|Seedspace Dar es Salaam.
Rafia Ramadhani ambaye aliwawakilisha wenzake kubuni wazo la Code Lady anasema lengo la program hiyo ya simu ni kuwaunganisha vijana na watu ambao wamefanikiwa katika fani mbalimbali ambao watawasaidia kimawazo.
“Kwa kupitia mtandao huu, mwanafunzi wa sekondari na chuo anaweza kutupatia taarifa zake na kisha baada ya siku mbili anaweza kuunganishwa na mtu ambaye amefanikiwa katika fani inayowiana na malengo ya mwanafunzi huyo,” anasema Rafia.
Programu hiyo ambayo inafanya kazi kama jukwaa la mtandaoni imekuja kuondoa tatizo la vijana kufanya maamuzi pasipo kuzingatia ushauri wa kitaalam katika fani wanazosomea au mambo wanayoyafanya katika jamii.
Wakati Code Lady wakiwalenga vijana, wenzao wa App ya simu ya Seedys ambayo iko mbioni kutengenezwa wameamua kuwasaidia wakulima wa Tanzania kutumia simu zao kubaini mbegu bora na sizo na ubora.
“Kupitia Seedys mkulima akinunua mbegu ataweza kuithibitisha kama ni mbegu halali au laa kupitia simu yake ya mkononi. Atahitajika kufuata maelekezo mafupi tu ambayo yatakua kwenye kifungashio cha mbegu hiyo,” anasema Nasibu Msangi, mmoja wa waanzilishi wa App hiyo ambayo iko kwenye majaribio.
Hata hivyo, startups hizo zitakuwa na kibarua kigumu cha kujinoa zaidi ili kusimama na kuhakikisha mawazo waliyonayo yanapenya katika jamii.
Shellimoh anasema watahakikisha startups hizo tano zinasimama na kuzifungulia fursa mbalimbali ikiwemo kuzipatia eneo la ofisi na wakufunzi wa kuwashauri.