Vyakula vinavyoongeza ufanisi wa kazi ofisini

February 1, 2021 1:31 pm · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni pamoja na kutumia mlo ulio na uwiano wa vyakula
  • Hakikisha kuna uwiano kati ya mafuta mazuri, wanga na protini unazingatiwa 
  • Epuka vyakula ambavyo siyo asilia vikiwemo maziwa yaliyotiwa ladha na vyakula vya madukani (processed).

Dar es Salaam. Wapo watu ambao baada ya chai tu, wanaanza kusinzia. Kwa wengi huweza kufikiri kuwa huenda hawajapumzika vya kutosha na hivyo bado wana uchovu lakini husababisha na vyakula wanavyokula asubuhi kabla ya kuanza kazi. 

Mtaalamu wa lishe Filbert Mwakilambo amesema yapo mengi ya kuangaliwa wakati wa kuchagua chakula cha kutumia wakati wa kifungua kinywa lakini muhimu ni umri, hali ya hewa ya eneo husika, hali ya afya ya mtu. Pia aina ya kazi/ shughuli anazofanya mtu (Kazi inayohitaji nguvu kidogo kwa watu wa maofisini au kazi inayohitaji nguvu nyingi).

Mwakilambo amesema “muhimu kifungua kinywa kizingatie uwepo wa vyakula kutoka angalau mafungu matano ya chakula ikiwemo nafaka, mizizi, ndizi mbichi, nyama, kunde na vyakula vitokanavyo na wanyama mfano mayai na maziwa.”

Pia vyakula kama mboga mboga, matunda, sukari, asali na maji ya kunywa havipaswi kukosekana.

Kuchagua kifungua kinywa kinachoendana na umri

Mwakilambo amesema watoto wanahitaji kifungua kinywa kilicho na makundi matano ya chakula lakini virutubisho vya protini, wanga, vitamini na madini vikiwa katika kiwango kikubwa kwa sababu watoto wanahitaji protini kuendelea kukua na wanga kuwapa nguvu huku vitamini vikiimarisha kinga ya mwili.

“Vijana wanahitaji kifungua kinywa kilicho na vyakula vya kuupa mwili nguvu kwa wingi. Wazee wanahitaji kifungua kinywa kilicho na vyakula laini lakini vinavyokupa mwili nguvu na kuongeza kinga ya mwili,” amesema Mwakilambo. 

Kifungua kinywa kinachoendana na aina ya kazi yako

Kwa mujibu wa tovuti ya afya ya gocontractor.com, kifungua kinywa cha mtu anayefanya kazi nzito ni tofauti na kile cha anayefanya kazi nyepesi.

Watu wa maofisini (mtu anaekaa muda mwingi) anahitaji kifungua kinywa chepesi na kilicho na vyakula vingi vya mbogamboga na matunda kwa wingi, protini na wanga kwa kiwango kidogo tofauti na wale ambao kazi zao zinahitaji nguvu nyingi.

Kifungua kinywa kulingana na hali ya kiafya

Kifungua kinywa pia hutofautiana kulingana na hali ya kiafya aliyonayo mtu. Matahalan, chakula ambacho mtu anayeumwa kisukari ni tofauti na chakula anachotakiwa kula mtu ambaye hana changamoto za kiafya.

Mwakilambo amesema mtu mwenye kisukari lazima azingatie uchaguzi wa kifungua kinywa kisichokuwa na sukari kwa kiwango kikubwa. 

Pia, mtu mwenye Kiliba tumbo (Uzito uliozidi) atazingatia kuwepo kwa kiwango kidogo cha wanga na kuweka mboga mboga na matunda kwa kiasi kikubwa.


Soma zaidi:


Baridi, joto nalo linahitaji kifungua kinywa chake

Uchaguzi wa kifungua kinywa pia huathiriwa na eneo ambalo mtu anaishi. Mfano kwa mtu anayeishi katika eneo la baridi kama Njombe lazima atakuwa na machaguo tofauti na mtu anayeishi katika sehemu ya joto kama jiji la Dar es Salaam.

Kwenye baridi unaweza tumia kinywaji kama chai ama  supu pamoja na vyakula vingine lakini kwenye joto unaweza tumia juisi na vyakula vingine kwa ajili ya kifungua kinywa chako.

Enable Notifications OK No thanks