Visababishi na matibabu ya bawasiri
- Ni pamoja na ubebaji wa vitu vizito na kutumia choo cha kukaa kwa muda mrefu.
- Inashauriwa kuwa na mlo mkamili na kunywa maji ya kutosha.
- Bawasiri zinatibika kwa dawa au kwa njia ya upasuaji.
Dar es Salaam. Ugonjwa huu ni kati ya magonjwa ambayo huongelewa kwa nadra sana licha ya kuwa takribani asilimia 75 ya watu duniani kukadiriwa kuupata ikiwa ni kwa mujibu wa tovuti ya masuala ya afya ya WebMd.
Bawasiri ambayo huwapata wanaume na wanawake husababishwa na vitu mbalimbali ikiwemo kutumia choo cha kukaa kwa muda mrefu pamoja na mtindo wako wa kukaa au kusimama.
Visababishi vingine ni kukaa kwa muda mrefu na kuwa na mfululizo wa kuhara.
Kwa mujibu wa Mtaalamu wa masuala ya afya kutoka Kituo cha Afya cha Ahmadiyya kilichopo mkoani Morogoro, Dk Joshua Sultan, bawasiri ni uvimbe kwenye sehemu ya haja kubwa unaosababishwa na damu inayorudi kutoka kwenye mishipa midogo baada ya kushindwa kusafirishwa kama inavyotakiwa.
Dk Sultan amesema hali hiyo inaweza kusababishwa na kupata ugumu wakati wa haja kubwa au kutumia nguvu nyingi kusukuma haja kubwa.
“Wakati mwingine inaweza kusababishwa na ujauzito lakini mtu hurudi kwenye hali yake ya kawaida baada ya kujifungua,” amesema Dk Sultan.
Mtaalamu huyo wa afya amesema sababu nyingine ni pamoja na kujamiiana kinyume na maumbile pamoja na unene uliopitiliza.
Unaweza kuanza kufuatilia matibabu pale utakapoamza kupata muwasho sehemu ya haja kubwa na kinyesi kuwa na damu.
Kwa wanaume, chanzo cha kupata bawasiri kinaweza kuwa ubebaji wa vitu vizito ikiwemo vyuma kwenye sehemu za kufanyia mazoezi (gym), begi lenye vitu vizito au shughuli yoyote inayohitaji mtu kutumia nguvu ya ziada inayosababisha presha kwenye eneo la puru (rectum).
Unashauriwa kunywa maji ya kutosha na kuepuka matumizi ya choo cha kukaa kwa muda mrefu. Picha| MedicalNet.
Unawezaje kutibu bawasiri?
Dk Sultan amesema matibabu ya bawasiri yanategemeana na vile yanaathiri maisha ya mgonjwa na inaweza kuhitaji upasuaji au isihitaji upasuaji.
Uvimbe wa bawasiri unaweza kuwa wa ndani ya mrija wa haja kubwa au nje.
“Inaweza kuhitaji upasuaji au laa. Inategemeana na hali yake,” amesema Dk Sultan.
Tovuti ya Web MD imeandika, unaweza kutibu Bawasiri ukiwa nyumbani lakini inashauriwa hayo maelekezo yatolewe na mtaalamu wa afya.
Kwa nyumbani, unaweza kukaa kwenye maji ya uvuguvugu kwa dakika 15 kadri uwezavyo na hasa baada ya kwenda haja kubwa. Itasidia kuondoa uvimbe na kuipatia ahueni mishipa ya eneo hilo.
Pia, mgonjwa anashauriwa kuvalia nguo zisizobana na kuhakikisha anakula chakula kilicho na nyuzi nyuzi (fibre) ikiwemo matunda na mboga za majani.
“Unaweza kutumia vyakula vinavyolainisha choo,” imeandikwa na WebMd ambayo pia imeshauri kunywa maji ya kutosha.
Hata hivyo, endapo utapatiwa matibabu iwe ya upasuaji au dawa na wewe kutokubadili mlo (diet) wako, unaweza kupata tena ugonjwa huo.
Latest
