Viongozi wa dini watoa ya moyoni sheria bima ya afya kwa wote
- Washauri wananchi waelimishwe umuhimu wake.
- Sheria ya bima ya afya kwa wote iharakishwe.
- Vitita vya gharama za bima viboreshwe kulingana na hali ya uchumi.
Mwanza. Viongozi wa dini nchini Tanzania wameshauri Serikali ijikite katika kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa bima ya afya ili wananchi waweze kujiunga na kuongeza wigo wa kuwa na mfumo imara wa matibabu.
Mwenyekiti wa kamati ya viongozi wa dini (ISCEJIC) Askofu Nelson Kisare amesema pia Serikali itenge fedha za kutosha kwa ajili ya kuratibu na kuelimisha watu kuhusu bima.
Askofu Kisare alikuwa akizungumza leo Desemba 20, 2021 jijini Mwanza katika mkutano wa uongezaji uwezo na taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu mapendekezo ya viongozi wa dini Tanzania ya umuhimu wa kupitishwa kwa sheria ya bima ya afya kwa wote.
Amesema wananchi wakielimishwa watapa hamasa ya kujiunga na bima ya afya kwa wote ambayo Serikali iko mboni kutunga sheria yake.
Serikali imeshatenga zaidi ya Sh149 bilioni kuratibu zoezi hilo ikiwemo kuandaa sheria maalu kusimamia bima hiyo ili kulinda afya za Watanzania.
Ameiomba Serikali kuweka kipaumbele endelevu cha kiwango cha fedha kitakachokuwa kinachangiwa na Serikali katika kuendesha bima ya afya kwa wote kiwango hicho pia kitachangiwa na wananchi.
“Hatutegemei Serikali kuchangia suala la bima ya afya kwa asilimia 100, bado kuna Watanzania ambao wana uwezo wa kuchangia,” amesema Askofu Kisare.
Endapo, Tanzania itapitisha sheria hiyo, Watanzania wahakikishiwa usalama wa afya zao kwa sababu watakuwa wameingia katika mfumo rasmi ya bima ya afya na hivyo kuwapunguzia gharama za matibabu.
Mwenyekiti mwenza wa ISCEJIC, Sheikh Khamis Mataka amesema dini zote zinaamini kwamba jamii yenye afya njema ni jamii yenye imani thabiti.
Amesema mwaka 2017 ISCEJIC ilijikita katika kampeni ya hifadhi ya jamii hasa katika afya ambayo ilitanguliwa na utafiti ulioitwa ‘Make it Possible ‘ ikimaanisha kufanya afya kwa wote kuwa kitu kinachowezekana.
“Viongozi wa dini walitoa mapendekezo yao kutokana na matokeo ya utafiti huo ikiwemo bajeti ya kugharamia afya isichukuliwe kama gharama bali ichukuliwe kama uwekezaji katika maendeleo ya mwanadamu ambayo ndiyo msingi wa kila kitu,” amesema Sheikh Mataka
Kwa mujibu wa kiongozi huyo, bado wanakumbana na kesi nyingi za waumini wao ambao hawana uwezo wa kugharamia matibabu kwa fedha taslimu, hivyo mchakato wa bima ya afya kwa wote uarakishwe ili kuwapunguzia wananchi maumivu.
“Muumini mwenye afya ni bora kuliko dhaifu kwakuwa ana nafasi ya kuchangia maendeleo ya nchi na familia yake na mtu dhaifu ni mzigo kwa jamii hivyo suala la bima ya afya kwa wote litetekelezwe na sheria iharakishwe ili wananchi waweze kutekeleza,” amesema Sheikh Mataka
Ameitaka Serikali kuboresha kitita cha huduma ya bima ya afya ili kiendane na malipo na bei ya soko ili kuondoa changamoto katika utoaji wa huduma na kuwa na maeneo maalum ya kodi ambayo itasaidia katika kuboresha sekta ya afya.
Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Hassan Kabeke amesema mpango wa bima unapaswa kuungwa mkono kwakuwa hakuna jambo kubwa kama afya na kuiomba Serikali kulifanyia kazi jambo hilo kwa haraka.
Mratibu wa kamati ya amani mkoa wa Mwanza, Sheikh Twaha Bakari amemuomba Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kutumia tozo za miamala ya huduma za kifedha za mitandao ya simu angalau za miezi miwili kwa ajili ya bima kwa wote.
Latest
