Mfahamu Khaby, kijana aliyepata utajiri kupitia TikTok
- Akaunti yake ilianza kukua baada ya kupoteza kazi kutokana na Corona.
- Khaby anashika nafasi ya pili kwa kuwa na wafuasi wengi katika mtandao huo.
- Maudhui anayoweka TikTok yamemuingia Sh4.6 bilioni.
Dar es Salaam. Mitandaoni kuna mambo mengi na huenda ni sawa kusema unaweza kupata maudhui ya kila aina kulingana na uhitaji wako.
Unaweza kupata maudhui ya kukuvunja mbavu, tamthilia za kukutoa machozi bila kusahau dondoo za kukusaidia kuboresha maisha.
Licha ya mitandao ya kijamii kutumika kama majukwaa ya kuwasiliana na kuburudika, kwa wengine ni biashara inayowaingizia fedha za kuendesha maisha yao. Huwezi kutenganisha mafanikio yao na mitandao ya kijamii.
Miongoni mwa watu hao ni kijana Khaby Lame, mtumiaji mashuhuri wa mtandao wa TikTok anayeingiza mpunga mrefu kupitia mtandao huo.
Unaweza kumfahamu Khaby kama una tabia ya kuperuzi mitandaoni ambapo umaarufu wake umeibuka kwa kukosoa video za watu ambao huonyesha dondoo za kurahisisha kazi zisizo na kichwa wala miguu.
Hadi sasa Khaby anashika nafasi ya pili kwa kuwa mtu mwenye wafuasi wengi zaidi katika mtandao wa TikTok. Picha| NTN24.
Unaweza kufikiri ni vichekesho vya mtandaoni lakini alichopata Khaby kutokana na video hizo fupi za hadi dakika moja, kinaweza kukushanganza.
“Ni sura yangu na lugha yangu ya uso inayowafanya watu wacheke,” alisema Khaby wakati akiongea na moja ya vyombo vya habari vya kimataifa.
Kijana huyo, mzaliwa wa Senegal anayeishi Italia anatumia kamera ya simu yake kutengeneza video hizo ambazo zimekuwa kivutio kikubwa kwa watumiaji wa TikTok na kumuingizia kitita cha kutosha.
Kupitia akaunti yake ya TikTok, Khaby amejipatia utajiri wa Dola za Marekani milioni 2 sawa na Sh4.6 bilioni.
Mtandao wa TikTok hulipa watumiaji wake ambao wamekidhi vigezo ya mfumo wa malipo wa “TikTok Fund”. Kati ya vigezo hivyo ni kuwa na wafuasi zaidi ya 10,000 na video kuwa na watazamaji walau 100,000 ndani ya siku 30.
Kwa wafuasi zaidi ya milioni 90 na watazamaji zaidi ya milioni 40 wa Khaby, bila shaka anavuta mpunga wa kutosha.
Kwa mujibu wa tovuti ya kufuatilia mwenendo wa mitandao ya kijamii, Social Tracker, Khaby (21) anashika nafasi ya pili kwa kuwa na wafuasi wengi katika mtandao huo tangu alipoanza kuutumia Machi, 2020.
Hadi leo (Agosti,9 2021) kijana huyo ana wafuasi milioni 99.7 akiwa chini Charli D’amelio, mcheza muziki (dancer) wa Marekani ambaye ana wafuasi milioni 121.9.
Khaby ana jumla ya video 938 katika mtandao huo huku zikiwa na “like” bilioni 1.5 bilioni. Wastani wa kutazamwa kwa kila video ya Khaby ni watu milioni 48.
Kwa mujibu wa tovuti ya takwimu za mitandao ya kijamii ya SocialBlade ukuaji wa akaunti ya Khaby unaweza kumfanya kuwa mwana TikTok anayefuatiliwa zaidi kama mwenendo wa ukuaji wa wafuasi ikiendelea kama ilivyo sasa.
Akaunti ya Khaby inakua mara nane zaidi ya akaunti ya D’amelio huku ndani ya siku 30 akiwa amejitwalia wafuasi wapya milioni 13, SocialBlade imeeleza.
Khaby ni nani?
Kabla ya kuingia kwenye mitandao ya kijamii, Khaby alikuwa mwajiriwa kiwandani huko kaskazini mwa Italia. Ugonjwa wa Corona ndiyo sababu ya kijana huyu kupoteza kazi yake kwa mujibu wa tovuti ya habari ya Insider.
Mbali na mizizi yake kukua katika mtandao wa TikTok, Khaby ni mpenzi wa soka anayeshabikia klabu ya Juventus ya Italia na kwa upande wa watu wanaompatia hamasa, Khaby amewataja wachekeshaji na waigizaji Eddie Murphy pamoja na Will Smith.
Matumaini ya Khaby, ni kufikia kiwango chao cha uchekeshaji siku moja.
@khaby.lame It’s better to give for who can’t afford it! Guys don’t do this! Dalla a chi ne ha bisogno ##learnfromkhaby
##learnwithtiktok
##imparacontiktok
Unatuamiaje mtandao? Weka maudhui yanayoweza kukukidhi mahitaji ya wafuasi wako ambayo yatakayokusaidia kupata kipato kwa ajili ya kuboresha maisha.
Latest



