Vijana, wanawake walemavu wanavyowezeshwa kujitegemea kiuchumi

April 5, 2019 1:54 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link

Ili kuhakikisha watu wenye ulemavu wanawezeshwa kiuchumi, amesema Serikali inatoa mikopo ya asilimia mbili zinazotokana na mapato ya ndani ya halmashauri ambapo mipango yote ya uwezeshaji kiuchumi inawajumuisha pia watu wenye ulemavu. Picha|Mtandao.


  • Imesema katika kuhakikisha inawawezesha vijana na wanawake wenye ulemavu kiuchumi, inaendelea kuwajengea uwezo kwa kuwapa elimu, mafunzo, mikopo na kuwaondolewa kodi katika baadhi ya vifaa saidizi.
  • Pia imewaondolewa kodi katika baadhi ya vifaa saidizi ili kuwapunguzia gharama za ununuzi.

Dar es Salaam. Serikali imesema katika kuhakikisha inawawezesha vijana na wanawake wenye ulemavu kiuchumi, inaendelea kuwajengea uwezo kwa kuwapa elimu, mafunzo, mikopo na kuwaondolewa kodi katika baadhi ya vifaa saidizi. 

Naibu Waziri  Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi , Vijana, Ajira na Wenye ulemavu anayeshughulikia watu wenye ulemavu,  Stella Ikupa ametoa ufafanuzi huo leo (Aprili 5, 2019) bungeni ambapo amesema Serikali itahakikisha vijana na wanawake wenye ulemavu hawaachwi nyuma katika nyanja mbalimbali za maendeleo ikiwemo kuwapatia elimu na kuwaondolewa changamoto zinazowakabili katika maisha yao ya kila siku.

Ikupa alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Kinondoni (CCM)  Maulid Mtulia ambaye alitaka kujua Serikali  ina mpango gani mahususi wa kuwajengea uwezo watu wenye ulemavu wa kujitegemea hasa vijana na watoto.

“Katika kuhakikisha watu wote wenye ulemavu hasa vijana, watoto na wanawake hawaachwi nyuma kiuchumi, Serikali inaendelea kuwajengea uwezo kuhakikisha watoto wote ikiwa ni pamoja na walemavu wanapata elimu ya msingi na sekondari ili kuwajengea uwezo wa kujitegemea,” amesema Ikupa.

Hatua nyingine ni kutoa elimu ya mafunzo na ufundi stadi kwa makundi ya vijana, wanawake wenye ulemavu kupitia vyuo vya watu wenye ulemavu na programu ya kukuza ujuzi hapa nchini. Mafunzo ya stadi za kazi kwa wanafunzi wenye ulemavu yanatolewa katika vyuo vya Singida na Yombo – Dar es Salaam.

Ili kuhakikisha watu wenye ulemavu wanawezeshwa kiuchumi, amesema Serikali inatoa mikopo ya asilimia mbili zinazotokana na mapato ya ndani ya halmashauri ambapo mipango yote ya uwezeshaji kiuchumi inawajumuisha pia watu wenye ulemavu. 

Hata hivyo, amebainisha kuwa Serikali inakamilisha uanzishwaji wa regista ambayo itasaidia kupata takwimu sahihi ya watu wenye ulemavu katika maeneo yote ya mjini na vijijini itakayosaidia katika mipango na maamuzi ya kisera yanayolenga kuwafikia katika maeneo yao na kuboresha maisha yao.

“Faida nyingine ya kuanzisha regista hizi zitatusaidia kutambua sababu za kuongezeka ulemavu katika kila eneo na changamoto zinazowakabili,” amesema Ikupa.


Soma zaidi:


Naye Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Faustine Ndugulile amesema Serikali imeondoa kodi katika baadhi ya  vifaa saidizi ili kuwapunguzia gharama za manunuzi na kuhakikisha vinapatikana kwa wakati vinapohitajika, jambo linalosaidia kuboresha maisha ya walemavu na kuwawezesha kujitegemea katika shughuli za kiuchumi. 

Amesema kuanzia mwezi huu Aprili hospitali ya mifupa Moi wataanza zoezi la upimaji na kutoa vifaa vya viungo bandia kwa baadhi ya walemavu ambao wanavihitaji ambapo ni fursa nyingine ya kuwajali na kuboresha hali zao.

“Kwahiyo nilikuwa naomba wabunge kwa watu wao ambao wanahitaji viungo bandia kufika katika hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya kupata vifaa hivyo lakini katika vifaa vya usikivu tumekuwa tunaendelea na  kampeni katika hospitali ya Taifa Muhimbili ya kupandikiza vifaa vya usikivu lakini kutoa vifaa saidizi kwa walemavu wanaohitaji vifaa hivyo,” amesema Dk Ndungulile. 

 Vifaa vilivyotolewa ni pamoja na viti mwendo, fimbo nyeupe, magongo ya kutembelea, viti maalum vya kuogea, miwani maalum, kofia pana, vifaa vya kukuzia maandishi, mafuta kinga kwa ajili ya watu wenye Ualbino na mashine za kuchapia maandishi ya nukta nundu kwa wasioona.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema katika mwaka 2019/2020, Serikali itafanya mapitio ya Sheria ya Watu Wenye Ulemavu amba tisa ya mwaka 2010 ili iweze kwenda na mabadiliko ya kiuchumi na kijamii, kukusanya maoni na mapendekezo ya uendeshwaji wa Mfuko wa Taifa kwa Watu Wenye Ulemavu pamoja na kuratibu uendeshaji wa shughuli za Baraza la Ushauri la Taifa kwa Watu wenye Ulemavu.

Enable Notifications OK No thanks