Vigogo wawili maabara ya Taifa wasimamishwa kazi, kamati ya uchunguzi yaundwa

May 4, 2020 11:39 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni Mkurugenzi wa Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii, Dk Nyambura Moremi na Meneja Udhibiti wa Ubora, Jacob Lusekelo.
  • Ni baada ya Rais kusema hana imani na maabara kuu katika upimaji wa sampuli za Corona.
  • Waziri Ummy aunda kamati ya wataalam 10 kuchunguza maabara hiyo. 

Dar es Salaam. Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu ameelekeza kusimamishwa kazi mara moja kwa Mkurugenzi wa Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii, Dk Nyambura Moremi na Meneja Udhibiti wa Ubora, Jacob Lusekelo kupisha uchunguzi.  

Hatua hiyo imekuja baada ya Rais John Magufuli kuagiza kuchunguzwa kwa maabara hiyo kwa kile alichoeleza kuwa kuna madudu katika upimaji wa virusi vya corona.

Magufuli alitoa maagizo hayo jana (Mei 3, 2020) Chato mkoani Geita wakati akimuapisha Waziri mpya wa Katiba na Sheria Mwigulu Lameck Nchemba. 

Dk Magufuli alisema kuwa hivi karibuni Katibu Mkuu mpya wa Wizara ya Afya Prof Mabula Mchembe, timu yake na vyombo vya ulinzi na usalama walipenyeza baadhi ya sampuli zisizo kama oili ya gari, fenesi, mbuzi, kondo, paipai, kwale na nyinginezo katika maabara hiyo na kuzipa majina ya binadamu bila wahusika kujua lakini majibu yalionyesha baadhi ya sampuli hizo zina corona.

Taarifa ya Wizara ya Afya iliyotolewa leo imesema wanatekeleza agizo la Rais la kuwasimamisha watumishi hao wawili wa afya ili wapishe uchunguzi. 


Soma zaidi: 


Aidha, Waziri Ummy ameunda kamati ya wataalam 10 wabobezi kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa mwenendo wa Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii ikiwemo mfumo mzima wa ukusanyaji na upimaji wa sampuli za COVID-19. 

“Kamati hii itaanza kazi mara moja na itatakiwa kuwasilisha taarifa yao kwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kabla ya Mei 13, 2020,” imeeleza sehemu taarifa hiyo. 

Kamati hiyo inaongozwa na Profesa Eligius Lyamuya kutoka Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS). 

Wajumbe wa kamati hiyo ni Prof. Said Aboud (MUHAS), Prof. Gabriel Shirima (Chuo Kikuu cha Nelson Mandela-NMIST), Prof Steven Mshana (Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Bugando-CUHAS) na Prof. Rudovick Kazwala (Chuo Kikuu cha Kilimo-SUA).

Wengine ni Dk Thoman Marandu (Chuo Kikuu cha Dar es Salaam-UDSM), Dk Mabula Kasubi (Hospitali ya Taifa Muhimbili-MNH), Danstan Hipolite (Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba-TMDA), Viola Msangi (Mtaalam wa Maabara Mstaafu) na Jaffer Sufi (Mtaalam wa Maabara Mstaafu)

Hata hivyo, Ummy amesema sambamba na uchunguzi wa kamati hiyo, upimaji wa sampuli katika maabara hiyo unaendelea kama kawaida.

Mpaka sasa Tanzania imeripoti kuwa na wagonjwa 480 wa Corona, 16 kati yao wamefariki dunia huku 167 wakipona.  

Enable Notifications OK No thanks