Vietnam iko tayari kununua korosho, pamba ya Tanzania
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Naibu Waziri Mkuu wa Vietnam, Trinh Dinh Dung, katika mazungumzo ya faragha yaliyofanyika ofisini kwa Waziri Mkuu, Magogoni jijini Dar es salaam, Julai 12, 2019. Picha| na Ofisi ya Waziri Mkuu.
- Naibu Waziri Mkuu wa Vietnum, Trinh Dinh Dung amesema itanunua mazao hayo ili kuyaongezea thamani kwenye viwanda vyake.
- Wakulima wa mazao hayo kupata ahueni ya bei na soko la kimataifa.
- Serikali yawahakikishia mazingira mazuri wawekezaji wa nchi hiyo.
Dar es Salaam. Naibu Waziri Mkuu wa Vietnam, Trinh Dinh Dung amesema nchi yake iko yatari kununua mazao ya kilimo ya Tanzania ikiwemo korosho na pamba ili kuyaongezea thamani kwenye viwanda vyake, jambo litakalokuza biashara baina ya nchi hizo mbili.
Dung amesema Tanzania na Vietnam zimekuwa na ushirikiano wa muda mrefu na ni vema uimarishwe zaidi katika sekta za kilimo, biashara na uvuvi.
Kutokana na Vietnam kujikita zaidi katika uwekezaji wa kilimo biashara, Naibu Waziri Mkuu huyo amebainisha kuwa nchi yake iko tayari kununu korosho na pamba ya Tanzania ili kuongeza thamani na kutengeneza bidhaa mbalimbali zitakazouzwa katika masoko ya kimataifa.
Amesema lengo la Serikali yake ni kuhakikisha kuwa biashara kati ya Tanzania na Vietnam inafikia dola za Marekani bilioni 1 (takriban Sh2.3 trilioni) ifikapo 2020.
Alikuwa akizungumza jana (Julai 12, 2019) alipokutana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Magogoni, jijini Dar es salaam, ambapo ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano iliyompa katika ziara yake nchini na ameomba ushirikiano huo uimarishwe kupitia ziara za viongozi na wakuu wa nchi hizo mbili.
Naibu Waziri Mkuu huyo wa Jamhuri ya Kisoshalisti ya Vietnam, amemuhakikishia Majaliwa kuwa Serikali yake itazidi kuimarisha uhusiano wake na Tanzania.
Uamuzi wa Vietnam kununua korosho na pamba ya Tanzania unaweza kuleta ahueni kwa wakulima wa mazao hayo ikizingatiwa kuwa wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya bei na upatikanaji wa masoko ya uhakika nje ya nchi.
Zinazohusiana:
- Mnada wa kahawa kuwanufaisha wakulima?
- Kwanini ufuatilie mjadala wa bei ya korosho?
- Serikali yatoa maagizo mazito kwa wanunuzi wa korosho
Majaliwa ametumia mazungumzo hayo kuwakaribisha wawekezaji kutoka Vietnam waje kuwekeza kwenye maeneo mbalimbali yakiwemo ya mipango miji, madini, bandari, usafiri wa anga, ufundi stadi, kilimo pamoja na uvuvi.
Amesema anatambua kuwa Vietnam inafanya vema katika kilimobiashara ambapo amezialika kampuni za Vietnam zenye teknolojia mahsusi katika maeneo tajwa zishirikiane na Tanzania katika mikakati yake ya kuendeleza kilimo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Tanzania itaendelea kuimarisha uhusiano wake na Vietnam kwa manufaa ya watu wa nchi hizo mbili.
“Nawakaribisha sana wawekezaji kutoka Vietnam kuja kuwekeza Tanzania kwani kwa kufanya hivyo hawatojutia uamuzi wao wa kuwekeza Tanzania,” amesema Majaliwa katika taarifa hiyo.