Veronica Sarungi: TO anayeishi ndoto, taaluma ya ualimu
- Alikuwa mwanafunzi bora kitaifa katika mtihani wa kidato cha nne mwaka 1988.
- Anajivunia kuitwa mwalimu hasa kufundisha somo la hisabati ili kuwawezesha wanafunzi kupenda masomo ya sayansi.
- Licha ya elimu aliyonayo, usawa na utu ndiyo nguzo ya maisha yake.
Dar es Salaam. Hapendi makuu, mcha Mungu, mcheshi na mtu anayejivunia kuitwa mwalimu.
Hivyo ndivyo unavyoweza kumtambua Veronica Sarungi, Mhadhiri wa taasisi ya Kuendeleza Elimu ya Afrika Mashariki (IED) katika Chuo Kikuu cha Aga Khan aliyebobea kufundisha somo la hisabati.
Ni mtoto wa aliyewahi kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa, Prof Philemon Sarungi katika Serikali ya awamu ya tatu iliyokuwa ikiongozwa na rais mstaafu Benjamin Mkapa na kushika nyadhifa mbalimbali serikalini.
Kwa wasiomfahamu Veronica, alikuwa mwanafunzi bora kitaifa katika mtihani wa kidato cha nne mwaka 1988 akisomea masomo ya sayansi katika Shule ya Sekondari Zanaki ya Jijini Dar es Salaam.
Veronica ambaye ana shahada mbili za Uzamili ikiwemo ya programu za kompyuta iliyoipata katika Chuo Kikuu cha Eotvos Lorand jijini Budapest, Hungary ni tofauti na wahadhiri wengine wa vyuo vikuu, yeye hupenda kujiita mwalimu na anajivunia kufundisha somo la hisabati, ndoto aliyokuwa nayo tangu akiwa mdogo.
“Mimi ni mwalimu wa hisabati, napenda sana kuwasaidia watu wapende kujifunza masomo yote lakini hasa hisabati,” anasema Veronica.
Uwezo wa kiakili wa Veronica ulianza tangu alipoanza kusoma darasa la kwanza katika shule ya msingi Bunge mwaka 1978 na baadaye alikwenda kumalizia masomo yake shule ya msingi Osterbay zote za jijini hapa.
Baada ya kuhitimu elimu ya msingi alijiunga na shule ya sekondari ya Zanaki, mchepuo wa sayansi na kumaliza kidato cha nne mwaka 1988 na kupata daraja la kwanza katika masomo yake.
Ufaulu huo ulimuwezesha kujiunga na masomo ya kidato cha V na VI katika shule ya sekondari ya wasichana ya Jangwani ya jijini Dar es Salaam katika mchepuo wa fizikia, kemia na bailojia.
Veronica Sarungi (pichani) ndiye aliyeibuka mwanafunzi bora kitaifa katika mtihani wa kidato cha nne mwaka 1988 lakini kwasasa anafurahia kuitwa Mwalimu wa hisabati. Picha| Daniel Samson.
Huko nako alitoboa katika mtihani wa kidato cha sita mwaka 1991 na kupata ufadhili wa kwenda kusoma katika Chuo Kikuu cha Eotvos Lorand, Budapest, Hungary ambapo huko alipata shahada ya kwanza na ya pili ya programu za kompyuta na Hisabati na kurejea nchini mwaka 1997.
Hata aliporejea nchini, Veronica hakukimbilia kazi zenye maslahi makubwa ukilinganisha na fursa na elimu aliyokuwa nayo, alienda kuwa mwalimu katika shule ya sekondari ya Loyola ya jijini hapa akitazamia kutimiza ndoto yake ya kuwa mwalimu wa hisabati.
“Mimi binafsi napenda hesabu, katika miaka ya 1990 walisema kwasababu umefanya vizuri basi chagua kitu ambacho kinalipa.
“Programu ya kompyuta naipenda kwasababu inafikirisha kama hisabati lakini nikasema hapana mimi sipendi ‘programming’ kwa sababu unakaa mwenyewe hukutani na watu hivyo baadaye nikafikiria niwe mwalimu wa msingi,” anasema Veronica.
Kutokana na mapenzi aliyonayo kwenye fani ya ualimu, alijiendeleza kielimu na kujiunga na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) na kupata Diploma ya Juu ya Elimu mwaka 2008 na baadaye alikwenda katika Chuo Kikuu cha Aga Khan na kupata shahada ya Uzamili ya Ualimu mwaka 2012.
Mwaka 2013 aliajiriwa katika chuo hicho kama Mhadhiri aliyebobea katika somo la hisabati akidhamiria kuwajengea uwezo walimu kutumia njia rahisi za kufundisha na kuwafanya wanafunzi kupenda somo hilo.
“Sisi zamani tulikuwa hatujui kama kuna ‘Tanzania One’, enzi zetu ulikuwa unasoma ufanye vizuri. Hata mimi walipokuja wakaniambia nina “Division One ya point 7”(Daraja la I) watu walishangaa kwa sababu ilikuwa kitu cha maajabu lakini tulikuwa tunasoma ili ufanye vizuri,”-Veronica Sarungi.
Anajali thamani ya utu na usawa
Licha ya kuwa baadhi ya walimu vijana wanaiona kazi yao kama ajira, Veronica hataki makuu au umaarufu katika jamii ambapo mawazo yake yote ni kuwasaidia watu kujifunza na kupata maarifa.
“Wakati baba yangu akiwa Waziri wa Ulinzi mwaka 2002/2003 wakati nikifanya kazi Loyola mimi nilikuwa napanda daladala naenda kazini, nini hasa cha kushangaza! Kwa sababu mimi niko kawaida najua wakiniona watajua Veronica niko tofauti,” anasema Veronica huku akishangaa baadhi ya watu kujivuna kwa vyeo vyao.
Msingi wa kujiona yuko sawa na watanzania aliupata wakati akiwa shuleni hata alipotangazwa kuwa mwanafunzi bora kitaifa hakubadilika na kujiona tofauti na wengine aliendelea kuamini kuwa mafanikio ya jamii yanatokana na kuhimiza usawa na haki kwa watu wote.
“Sisi zamani tulikuwa hatujui kama kuna ‘Tanzania One’ (Mwanafunzi bora), enzi zetu ulikuwa unasoma ufanye vizuri. Hata mimi walipokuja wakaniambia nina “Division One ya point 7”(Daraja la I) watu walishangaa kwa sababu ilikuwa kitu cha maajabu lakini tulikuwa tunasoma ili ufanye vizuri,” anasema.
Zinazohusiana:
- Matumaini waliyobeba wanafunzi bora Tanzania
- Mfahamu Given Edward, mtanzania aliyeshinda tuzo mbili za kimataifa katika sekta ya elimu
- Emanuel Feruz: Mtaalam wa Tehama aliyegeukia ujasirimali wa kupigaji picha
- Rahma Bajun: Mjasiriamali anayetamba kimataifa
Elimu yake ina manufaa kwenye jamii?
Mtazamo wa Veronica kuhusu jamii yake bado haujabadilika. Usiku na mchana anatafuta namna ya kuwasaidia wanafunzi kupata maarifa bora hasa katika somo la hisabati ili kuacha alama kwa vizazi vinavyokuja.
“Kwa sifa nilizonazo mimi, nina ‘masters’ mbili (Shahada za Uzamili), hela ninayopewa hata kama nifanya kazi kwenye chuo binafsi kwa mtu ambaye tumemaliza naye anapata hela zaidi.
“Kwa hiyo hela hata siku moja haitaweza kukutosha kwa sababu kazi unayofanya kama mwalimu ni kubwa sana kuliko mshahara unaopata,” anasema Veronica huku akitabasamu kuonyesha kuridhika na maisha yake.
Kupitia taasisi ya IED amekuwa akitumia fursa mbalimbali anazopata kuwafundisha walimu wa shule za msingi na sekondari kutumia njia rahisi za kufikisha maarifa kwa wanafunzi kwa sababu anaamini kuwa wanafunzi wote wana akili isipokuwa tu njia zinazotumiwa kufundisha ndiyo zina changamoto.
Pia Veronica Sarungi amekuwa mstari wa mbele kutoa mada za kitaaluma katika majukwaa mbalimbali ya elimu. Picha| AFLA.
Mbali na shughuli za kitaaluma, Veronica ambaye ni dada wa Mwanaharakati na mwanzilishi wa kampeni ya mtandaoni ya “ChangeTanzania”, Maria Sarungi, ni mwimbaji wa nyimbo hasa kwaya za kanisani.
Alianza kuimba akiwa shule ya msingi na alipata nguvu zaidi ya kuwa mwimbaji akiwa kidato cha pili mwaka 1986 alipopata nafasi ya kutumbuiza kwa nyimbo na ngonjera katika Kituo cha Utamaduni cha Korea (Korean Cultural Centre) kilichokuwa kinaratibu shughuli zake jijini Dar es Salaam.
Ujumbe alionao kwa wanafunzi hasa wasichana ni kujiamini na kusimamia kile wanachokipenda hata kama watu wengine hawakifurahii.
“Lazima ujiamini ili upige hatua mbele na kufikiria namna ya kujiendeleza hata kama unafanya kitu kidogo namna gani. elimu haina chaguo,” anasema.