‘Vanguard’: Filamu inayokusindikiza kumaliza mwaka 2020
- Inamuhusisha nyota wa filamu kutoka China, Jackie Chan.
- Filamu hiyo inahusu kundi la ‘Vanguard’ ambalo linajitoa kumlinda Qin anayetafutwa na magaidi kutoa taarifa za mali za mtu aliyeaga dunia.
- Hata baada ya kufanikiwa, wanapata kibarua cha kumlinda mtoto wa Qin ambaye yupo barani Afrika.
Dar es Salaam. Ni kitambo tangu mcheza filamu wa China, Jackie Chan atuburudishe kupitia televisheni na skrini zetu kwa filamu mbalimbali.
Mara ya mwisho alionekana katika filamu ya “Journey to China” aliyoshirikiana na Arnold Schwarzenegger iliyotoka Agosti, 2020. Nguli huyo wa vichekesho na vichapo anaufunga mwaka 2020 katika filamu nyingine ijulikanayo kama “Vanguard”.
Kwanini uitazame filamu hii?
Tang Huanting (Jackie Chan) ni kamanda wa kikosi kazi cha “Vanguard” ambacho ni sehemu ya kampuni ya ulinzi iliyo na jina hilo hilo. Kazi yao ya kwanza, ni kumlinda Qin Guoli ambaye aliwahi kulazimishwa na gaidi Maasym kuratibu biashara zake na kuwa chanzo cha kifo cha gaidi huyo.
Kifo cha Maasym kinamuacha nyuma Omar ambaye ni mtoto wa gaidi huyo akiwa na lengo la kufukuzia mali za marehemu baba yake na bahati mbaya anayefahamu kuhusu mali hizo ni Qin peke yake.
Omar anaajiri kikundi cha kufanya oparesheni ya kumteka Qin na mke wake Meiwei bila kujali penzi changa walilokuwa nalo wawili hao kwani ndiyo kwanza wamefunga ndoa. Wanafanikiwa.
Hata baada ya Vanguard chini ya uongozi wa Jackie Chan kufanikiwa kumkomboa Qin, wanapata kazi nyingine ya kumfuata Fareeda mtoto wa Qin ambaye yupo Afrika kabla Omar hajamtumia kama ndoano ya kumpata.
Soma zaidi:
- Ni kweli wachawi wapo? Tazama filamu hii
- Unyanyasaji wachangia kuwakimbiza wasichana kwenye mitandao ya kijamii
- Tafakari haya kabla ya kuingia kwenye ujasiriamali
Safari ya Afrika inapoanza ndipo utamu unapokolea
Kupotezana wakati wa jitihada za kumkomboa Fareeda, fedha kubadilishwa thamani na kuwa magari ya dhahabu, mkono wa kukuvunja mbavu na uhasama ni kati ya vitu utakavyoviona ndani ya filamu hii inayoonyeshwa katika kumbi za kuangalizia filamu za MlimaniCity, AuraMall na ofisi zote za Century Cinemax kwa gharama ya Sh10,000 tu.
Unaachaje kuangalia filamu ya Chan ambaye hajawahi kukuboa?
Hata hivyo, bado tunasubiri kwa hamu ujio wa filamu kabambe na uvumilivu unatushinda ikiwemo filamu ya “No Time To Die” yake James Bond maarufu kama Agent 007.
Latest
