Uzalishaji, mauzo bidhaa za viwandani vyapaa
- Bidhaa hizo ambazo uzalishaji wake umeongezeka kwa kipindi cha mwaka mmoja ni bia, saruji, unga wa ngano, vinywaji baridi, mafuta ya kula na sukari.
- Pia zimechangia kuongezeka kwa mauzo ya bidhaa za viwandani nje ya nchi.
- Bado bidhaa asilia zinaendelea kuiingizia Tanzania mapato mengi.
Dar es Salaam. Licha ya thamani ya mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi kushuka, uzalishaji wa bidhaa sita za viwandani umeongezeka katika kipindi cha mwaka mmoja, jambo linafanya sekta hiyo kuendelea kuwa mchango mkubwa katika ukuaji wa sekta ya viwanda Tanzania.
Bidhaa hizo ambazo uzalishaji wake umeongezeka ni bia, saruji, unga wa ngano, vinywaji baridi, mafuta ya kula na sukari.
Ripoti ya takwimu za Hesabu za Taifa (National Accounts Statistics) ya mwaka 2018 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inaeleza kuwa thamani ya mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi ilishuka hadi kufikia Sh17.7 trilioni mwaka 2018 kutoka Sh17.9 trilioni mwaka 2017.
Sababu kubwa ya kushuka kwa thamani ya mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi kulichangiwa kwa sehemu kubwa na kupungua kwa bei katika soko la dunia kwa bidhaa asilia za kahawa, pamba, katani, chai na tumbaku, na kupungua kwa mauzo ya korosho katika soko la dunia.
Hata wakati thamani ya mauzo nje ya nchi ikipungua, uzalishaji wa bidhaa sita za viwandani umeongezeka kwa viwango tofauti katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.
Ripoti hiyo inaonyesha kuwa uzalishaji wa saruji inayotengenezwa na viwanda vya ndani imeongezeka kutoka tani milioni 4.5 mwaka 2017 hadi tani milioni 5 mwaka jana sawa na ongezeko la asilimia 11.2 katika kipindi cha mwaka mmoja.
Zinazohusiana:
- Kwanini ufuatilie mjadala wa bei ya korosho?
- Wakulima kuwezeshwa kuuza pamba kwa bei wanayotaka
- Megawati 300 za umeme wa upepo kuchagiza ukuaji wa uchumi wa viwanda Tanzania
Uzalishaji wa unga wa ngano umefikia tani milioni 743,000 mwaka jana kutoka tani milioni 699,000 mwaka 2017. Licha uzalishaji kuongezeka bado Tanzania inategemea kuagiza kwa kiasi kikubwa malighafi ya ngano kutoka nje ya nchi ili kukidhi mahitaji ya viwanda vya ndani.
Jana (Agosti 1, 2019) Rais John Magufuli aliagiza ngano ianzwe kulimwa kwa wingi nchini ili kupunguza gharama za uzalishaji, kuongeza ajira kwa wakulima na usafirishaji wa unga huo nje ya nchi huku akibainisha kuwa Serikali itaendelea kuwathamini wawekezaji wanaowekeza katika viwanda.
Bidhaa zingine ambazo uzalishaji wake umeongezeka ni pamoja na bia, sukari na vinywaji baridi kama soda na maji.
Kutokana na kuongezeka kwa uzalishaji wa bidhaa hizo kumechangia pia kuongezeka kwa thamani ya mauzo ya bidhaa za viwandani nje ya nchi hadi kufikia dola za Marekani milioni 794.6 (takribani Sh1.8 trilioni) kutoka dola milioni 693.7 (takriban Sh1.5 trilioni) mwaka 2017,
Ongezeko hilo ni sawa na asilimia 14.5 katika kipindi cha mwaka mmoja.
Licha ya kuongezeka kwa uzalishaji na mauzo ya bidhaa za viwandani, bado mchango wake katika mauzo ya nje ni wa kiwango cha chini ikizingatiwa kuwa Tanzania inategemea zaidi kupata mapato ya kigeni kupitia usafirishaji wa madini na bidhaa ghafi kama pamba, kahawa na korosho.
Mataifa yanayotegemea bidhaa ghafi huathiriwa na msukosuko wa bei kupanda na kushuka katika soko la dunia.
Latest