Uteuzi Dk Ndugulile WHO kuipaisha Tanzania kimataifa
- Ateuliwa kuwa Mkurugenzi wa Shirika la Afya (WHO), Kanda ya Afrika na kuwa mtu wa kwanza kutoka Afrika Mashariki kushika wadhifa huo.
- Mwanadiplomasia huyo huzungumza lugha zaidi ya moja.
Dar es Salaam. Tanzania imeendelea kung’aa katika anga za uongozi kimataifa mara baada ya Mbunge wa Jimbo la Kigamboni jijini Dar es Salaam Dk Faustine Ndugulile kuteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika.
Dk Ndungulile, ambaye ni daktari wa binadamu kitaaluma, sasa anaingia kwenye orodha ya wanadiplomasia mashuhuri Tanzania wanaoongoza taasisi za kimataifa katika ngazi ya dunia na kikanda.
Kiongozi huyo anakuwa wa kwanza kutoka ukanda wa Afrika Mashariki kuchukua kijiti hicho kutoka kwa Dk Mtashidiso Moeti ambaye amehudumu katika nafasi hiyo kwa kipindi cha miaka 10 tangu mwaka 2014.
Kwa mujibu wa WHO uteuzi Dk Ndugulile unatarajiwa kuridhiwa kwenye kikao cha 156 cha Bodi ya Utendaji wa WHO kitakachofanyika Februari, 2025 huko jijini Geneva, Uswizi ikiwa ndiyo mwanzo wa safari ya miaka mitano ya uongozi wa mtaalamu huyo wa afya.
Dk Ndugulile (55) mwenye Shahada ya udaktari wa madawa pamoja na shahada ya uzamili kwenye mikrobiolojia na chanjo katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) amewahi kushika nyazifa mbalimbali ndani ya Serikali ikiwemo ya unaibu waziri wa afya.
Ushindi huo wa Dk Ndugulile aliyekuwa akichuana na wataalamu wengine kutoka Rwanda, Niger na Senegal ni moja ya hatua muhimu kwa Tanzania kuendelea kuimarisha taswira yake katika nyanja za kimataifa hususan katika taasisi kuu za kufanya maamuzi duniani.
Nchi wanachama wa Afrika walimteua Dk Ndugulile jijini Brazzaville nchini Congo jambo ambalo amesema ni heshima kubwa kwake.
“Nia yangu ni kufanya kazi pamoja nanyi na naimani kwamba kwa pamoja tutaweza kujenga Afrika yenye afya bora,” amesema Dk Ndugulile.
Dk Ndugulile, aliyewahi kuwa Waziri wa zamani wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano alijunga na siasa tangu 2010 kupitia tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) huku akishikilia nyadhifa mbalimbali za uongozi kwenye sera za afya kutokana na uzoefu wake wa kazi.
Mtaalamu huyo wa afya ameongoza miradi mbalimbali katika huduma za afya nchini Tanzania na kuandika machapisho ya tafiti zinazohusu afya ya umma ambazo zimechangia katika maendeleo ya sera za afya inayolenga kuboresha afya ya wananchi.
“Dk Ndugulile amepata imani na uaminifu wa wanachama wa nchi wa kanda hii kwa kuchaguliwa kuwa Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika, hii ni heshima kubwa na jukumu kubwa sana…mimi na familia nzima ya WHO barani Afrika na duniani kote tutakusaidia katika kila hatua,” amebainisha Dk Ghebreyesus.
Hata hivyo, kuteuliwa kwake kama Mkurugenzi wa Shirika la Afya (WHO), Kanda ya Afrika ni hatua muhimu katika kufanikisha malengo ya afya kwa nchi za Afrika hii inathibitisha kutokana na uzoefu na utaalamu wake kwenye uwanja wa afya.
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan aliyekuwa akimpigia kampeni Dk Ndugulile alieleza kwenye mtandao wa X (zamani Twitter) kuwa kiongozi ameiheshimisha nchi na kwamba Afrika itanufaika na utaalamu wake.
“Nina imani kuwa ujuzi na uzoefu wako katika sekta ya afya utawezesha Afrika kuwa na sauti muhimu katika uwanja wa kimataifa katika kukabiliana na changamoto za kiafya kwa mamilioni ya watu katika bara letu,” amesema Rais Samia.